23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Christine Lagarde: Kielelezo cha uwezo wa wanawake kuikomboa uchumi wa dunia

JOSEPH HIZA

KWA muda mrefu wanawake hawajawahi kudhaniwa kuwa watu sahihi wa shughuli kama vile uongozaji wa filamu pale Holly­wood, kufanya majadiliano mazito na mabwanyenye wa kifedha wa Wall Street au kuendesha maamuzi nyeti pale Washington.

‘Ni hatari sana, kuwaruhusu wanawake kushughulika na dili zinazohusisha bajeti kubwa,”walidai wanaume wengi waliotopea katika mfumo dume.

Lakini Christine Lagarde amewadhibitishia hawako sahihi kutokana na namna anavyoweza kuushikilia vyema uchumi wa dunia katika kiganja cha mkono wake.

Lagarde, mzaliwa wa Paris na mmoja wa wanamichezo wa zamani wa timu ya Taifa ya kuogelea Ufaransa, alikuwa mwanasheria kabla ya kujiunga na Serikali ya Ufaransa mwaka 2005.

Alitumikia kama waziri wa biashara na kilimo na uvuvi kabla ya kuwa waziri wa fedha na uchumi.

Mkurugenzi huyo mwenye umri wa miaka 63 wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF), ambaye ni mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo, kwa muda mrefu amekuwa akikosoa tabia ya kukosekana wanawake katika nyadhifa za juu za uongozi maeneo mengi duniani.

Anaamini kabisa wanawake ni kani ya ustaarabu yenye uwezo mkubwa wa kuokoa uchumi wa dunia, ambayo ikipewa nafasi italeta tofauti duniani.

Ukiachana na hayo, ni watu wachache katika safu ya juu ya duru la kifedha duniani, ambao huweza kufurahia maisha wakiwa na sifa nzuri zilizo mbali na kashfa kama, Christine Lagarde.

Ikiwa si kawaida kwa mtu wa hadhi yake, mkuu huyo wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF), anahesabiwa na wengi kama mtu safi, asiye na doa hasa wakati unapomweka katika mizania moja na mtangulizi wake, Dominique Strauss-Kahn.

Hadi anamrithi Strauss-Kahn mwaka 2011, akitangazwa kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa Ukurugenzi Mtendaji wa IMF, ambacho amekuwa akipokea kilikuwa dole tupu!.

Alielezwa kuwa kiongozi mwadilifu na mwenye uwezo mkubwa wa kazi.

Lagarde alikuwa mmoja wa mawaziri wachache wa fedha kuibuka kutoka kipindi kile kigumu cha mdororo wa uchumi huku sifa zao zikibaki pale pale imara bila doa.

Akiwa maarufu kwa staili yake ya mavazi, wepesi wa ucheshi awapo katika televisheni kana kwamba yu chumbani, Lagarde alikaribishwa kwa mikono miwili na IMF na wale ambao walikuwa wamechoshwa na wana uchumi wenye mikono michafu.

Kiuhalisia, kwa mtu yeyote aliyemwondoa mtu aliyekumbwa utitiri wa ‘skendo’ Dominique Strauss-Kahn, alipata ahueni kumpata mtu aliyeamini yu msafi.

Akiwa amezaliwa katika familia ya wasomi ya Paris, maisha ya awali ya Lagarde yalikulia katika kitongoji cha Le Havre, kabla ya kupata udhamini mwaka 1973 kusomea katika Shule ya Holton-Arms nchini Marekani.

Ni kipindi akiwa shuleni hapo alijipatia uzoefu wa kwanza wa dunia ya siasa, hali iliyoendelea wakati alipofanya kazi chini ya uangalizi wa Seneta wa Marekani William Cohen.

Mara baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Paris West na kujipatia shahada ya uzamili katika English na sheria, alirudi Marekani na kufanya kazi katika kampuni ya sheria ya Baker & Mackenzie huko Chicago.

Sehemu ya majukumu yake katika kampuni hiyo ilikuwa kushughulika pamoja na mambo mengine migogoro ya wafanyakazi, kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi.

Mafanikio hayo yakamzawadia ubia na kuwa mkuu wa kitengo cha kampuni hiyo barani Ulaya miaka sita tangu ajiunge nayo.

Kufikia mwaka 1999 aliteuliwa na kampuni hiyo kuwa mwenyekiti wake akiwa mwanamke wa kwanza kuiongoza.

Mwaka 2005 aliingia katika siasa kama Waziri wa Biashara wa Ufaransa chini ya aliyekuwa Rais Jacques Chirac, akiwa na jukumu la kuitafutia nchi yake masoko mapya kwa ajili ya mazao yake.

Alibakia serikalini baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 uliomwingiza madarakani Rais sharobaro wa mrengo wa kulia Nicholas Sarkozy.

Katika serikali hiyo, alitumikia kwa muda mfupi kama Waziri wa Kilimo kabla ya kuchaguliwa kuwa waziri wa kwanza mwanamke wa fedha wa Ufaransa.

Miaka minne ya kuitumikia nafasi hiyo ilishuhudia mafanikio, akikuza viwango vya mauzo ya nje na kumfanya atajwe kuwa waziri wa fedha bora kabisa barani Ulaya mwaka 2009 na jarida la kimataifa la Financial Times.

Akiwa anazuru studio za televisheni mara kwa mara na kushiriki mikutano mikubwa ya dunia akitoa mihadhara kwa duru za kibenki jinsi zilivyosababisha mgogoro wa kifedha, Lagarde alionwa kuwa mmoja wa mawaziri wachache wa fedha walioibuka kutoka mgogoro wa kifedha huku sifa zao zikibakia nzuri kiutendaji.

Hata hivyo, wakati wake kama waziri wa fedha nchini humo haukupita bila kutupiwa jicho la pili.

Mwaka 2010, alituma orodha ya wateja karibu 2,000 wa Kigiriki, ambao walikuwa na akaunti za siri katika tawi la Uswisi la Benki la HSBC kwa mamlaka za Ugiriki.

Hatua hiyo ililenga kuisaidia Serikali ya Ugiriki iliyokuwa ikitaabika kwa mzozo wa madeni, kuwabaini matajiri wakwepa kodi wa nchi hiyo.

Lakini orodha yake hiyo, ikaangukia mikononi mwa mwandishi Kostas Vaxevanis miaka miwili baadaye, ambaye  aliianika, akisema hakukuwa na hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao.

Mwandishi huyo akakamatwa kwa kukiuka sheria za usiri, ijapokuwa baadaye aliachiwa.

Pamoja na kuwa Lagarde hakuhusishwa na kashfa hiyo, baadhi walimkosoa.

Walisema Waziri wa Fedha wa Ufaransa hakupaswa kuingilia masuala yanayohusu raia wa Ugiriki wenye akaunti katika benki za Uswisi.

Nafasi yake ya Mkurugenzi wa IMF ni mnara wa uchumi wa dunia, ikibeba ushawishi na nguvu kubwa.

Majukumu yake pamoja na mambo mengine ni kuunganisha viongozi wa kifedha duniani, kuongoza chumi zinazotetereka na kushauri juu ya sera za baadaye.

Kwa kawaida raia wa Ulaya huishika nafasi hiyo huku wa Marekani akiiongoza Benki ya Dunia (WB).

Hata hivyo, mataifa manne yanayokuja juu kiuchumi ya BRIC (Brazil, Russia, India, China) kabla ya kujiunga kwa Afrika Kusini na kutengeneza ‘BRICS’ yalikuwa yakipinga vikali utamaduni huo.

Mataifa hayo yalitaka uwakilishi zaidi katika uchaguzi wa kiongozi wa vyombo hivyo, kitu ambacho, hata hivyo kilipuuzwa wakati wa uteuzi wa Lagarde.

Wakati kashfa ya ubakaji ya dhidi ya Mfaransa mwenzake, Strauss-Kahn ilipoibuka mwaka 2011, Lagarde alikuwa mwepesi kutamka wazi  kuitaka nafasi hiyo.

Akiwa mgombea maarufu zaidi, alipokea uungwaji mkono kutoka serikali nyingi duniani ikiwamo za Marekani, Uingereza, India, China na Ujerumani.

Hiyo, ilimaanisha India na China wanachama wa BRIC pia walichotwa na ‘uchawi’ wa Lagarde, hivyo wakaweka kando madai yao, bila kujali mshirika wao Brazil alikuwa kwa udi na uvumba akiitaka nafasi hiyo.

Hata hivyo, bado baadhi walieleza kutofurahishwa kuwa alikuwa mgombea mwingine kutoka Ufaransa– ukizingatia mabosi watano kati ya 11 waliowahi kuiongoza IMF walikuwa Wafaransa.

Hata hivyo, sifa na hadhi kubwa aliyokuwa nayo, zilikuwa zenye kushawishi mno, kiasi kwamba hata mataifa lalamishi hayakuwa na nguvu ya kumpinga.

Kufikia mwisho mwa Juni mwaka huo, mwezi mmoja baada ya kutangaza kwake kugombea nafasi hiyo, alipigiwa kura kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa IMF, akianza kile ambacho kinakuwa miaka mitano ya awali katika chombo hicho.

Pamoja na mwitikio hasi kutoka wengi walio nje ya Ulaya, uamuzi wa kumchagua ulipokelewa vyema na watunga sera wa kifedha.

Waziri wa zamani wa Fedha wa Marekani, Timothy Geithner, kwa mfano alimwelezea Lagarde hivi. “Wepesi wake wa kufikiri, ucheshi wa asili na uwezo wa kutibu mgawanyiko wakati huo huo akibakia mwaminifu kwa masilahi ya Ufaransa umekuwa chanzo cha pongezi hii.”

Hata hivyo, pamoja na kukaribishwa kwa staili ya aina yake, kipindi cha Lagarde hakijapita bila dhoruba.

Ni hizi kashfa zinazorudi nyuma wakati akiwa Waziri wa fedha wa Ufaransa, akidaiwa alifanya upendeleo wa kisiasa kwa ajili ya Bernard Tapie.

Tapie ni mfanyabiashara maarufu nchini Ufaransa, ambaye ametupiwa na jicho la umma mara nyingi kwa mabaya kwa zaidi miongo miwili.

Akituhumiwa kupanga matokeo wakati akimiliki Klabu ya Mpira wa Miguu ya Olympique de Marseille, mwaka 1993 Tapie alienda jela kwa rushwa na kutishia mashahidi.

Hilo limamshuhudia akienda kuitumikia miezi sita nyuma ya nondo!

Hata hivyo, pamoja na kukwaruzana na mikono ya sheria katika miaka ya 1990, Tapie hakukoma, kitu ambacho moja kwa moja kilimwingiza Lagarde matatani.

Pamoja na kuwa awali alitumikia kama waziri katika serikali ya Kisoshalisti, Tapie alimuunga mkono kwa nguvu rafiki yake sharobaro, Sarkozy wa chama cha Union for a Popular Movement (UMP) katika uchaguzi wa rais mwaka 2007.

Hatua hiyo, iliangaliwa kwa shaka na wengi, ikizusha maswali kwanini mtu mwenye itikadi iliyoegemea mno kushoto achague kumuunga mkono mgombea mpenda biashara.

Ikaja bainika kuwa Tapie alikuwa akihaha kutatua kesi kadhaa kuhusu kodi zilizokuwa zikimkabili, ambazo Sarkozy – na hasa Lagarde – wanatuhumiwa kuahidi kumsaidia kuzitatua wakati watakapochaguliwa.

Tapie alikuwa katika mgogoro wa muda mrefu na Benki ya Mikopo ya Ufaransa, Credit Lyonnais juu ya mauzo ya kampuni yake ya utengenezaji wa vifaa vya michezo ya Adidas ya Ujerumani mwaka 1993.

Mwaka 1990, wakati Tapie akiwa mmoja wa wafanyabiashara maarufu kabisa nchini Ufaransa huku akiimiliki Olympique Marseille – akawa mwanahisa namba moja wa Adidas.

Hivyo, miaka mitatu baadaye, aliingia makubaliano na benki ya mikopo ya Ufaransa, Crédit Lyonnais, sasa sehemu ya Crédit Agricole, kuuza hisa zake kwa faida.

Kwa mujibu wa makubaliano, benki hiyo ya umma, hata hivyo haikuruhusiwa kujinunulia hisa wala kunufaika na faida kutokana na mauzo ya hisa hizo.

Lakini hicho ndicho, ambacho benki hiyo ilifanya, kwa mujibu wa madai ya Tapie, hali iliyosababisha afungue kesi.

Crédit Lyonnais ilijipatia hisa kwa karibu faranga bilioni mbili (fedha ya Ufaransa wakati huo) na kuziuza tena ndani ya miezi mitatu kwa bei karibu maradufu.

Baada ya miaka 15 ya mvutano wa kisheria baina ya mfanyabiashara huyo na taasisi ya fedha huku umma ukielekea kushinda, Lagarde aliingilia kati.

Akiwa waziri wa fedha chini ya Nicholas Sarkozy, Lagarde aliliwasilisha suala hilo kwa jopo la usuluhishi la watu watatu katika harakati za kuumaliza mgogoro huo mara moja kwa ‘faida ya wote.’

Mwishowe, Jopo hilo likapitisha uamuzi wa kumzawadia Tapie dola milioni 527, fedha za umma kama fidia ikihusisha pamoja na riba.

Inadaiwa kuwa Lagarde aliingilia kati kwa amri ya Sarkozy.

Kitendo cha kesi hiyo kumpendelea mfanyabiashara huyo kikaelezwa ni zawadi kwa Tapie kwa kumuunga mkono Sarkozy wakati wa kampeni ya urais mwaka 2007.

Lagarde pia anakosolewa kuwa akiwa waziri wa fedha hakupaswa kuingilia kati kwa niaba ya mtu, ambaye ni hivi karibuni tu alisaidia kukiingiza madarakani chama chake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles