26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Chris Brown aweka heshima Mombasa

Chris Brown
Chris Brown

NA JOSEPH SHALUWA, MOMBASA

STAA wa muziki wa RnB kutoka nchini Marekani, Chris Brown ameweka historia baada ya kufanya shoo yenye ujazo wa juu katika onesho lililopewa jina la Mombasa Rocks Music Festival iliyofanyika juzi Jumamosi jijini hapa.

Onesho hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Mombasa Rocks Music lilifanyika katika Viwanja vya Nyali Mombasa Golf Club na kuhudhuriwa na mamia ya mashabiki kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Mombasa.

Chris Brown maarufu Breezy alijua namna ya kutumia vyema jukwaa hilo na kupagawisha mashabiki ambao walikuwa wakimshangilia muda wote aliokuwa akifanya vitu vyake jukwaani.

Msanii huyo alipanda jukwaani mishale ya saa 6:30 usiku na kufanya kazi ya kuwaburudisha mashabiki mpaka saa 9 kasoro za usiku ambapo shangwe ilitawala viwanjani hapo.

Mbali na msanii huyo kuonyesha ufundi mkubwa katika kuimba na kucheza, madansa wake wawili waliokuwa naye beneti muda wote, walinogesha onesho hilo kwa staili yao ya kucheza huku kivutio kikubwa kikiwa ni kupiga muziki live.

Kwa zaidi ya dakika 90, Brown alipiga shoo mfululizo ingawa alitumia dakika tatu katikati ya shoo kwa ajili ya kubadilisha mavazi.

Kabla ya Brown kupanda, alisafishiwa njia na wasanii wengine wa Afrika huku wa mwisho kabla ya yeye kupanda akiwa ni mkali wa Bongo Fleva, Ali Kiba.

Wa kwanza kupanda jukwaani alikuwa ni mkongwe wa Dancehall nchini Kenya, Naazizi Hirji ambaye alipagawisha mashabiki kwa nyimbo zake za zamani kama Let’s Get Down na Kenyan Girl Kenyan Boy zilizoamsha shangwe kwa mashabiki.

Baada ya Nazizi kushuka jukwaani, msanii Nadio kutoka Uganda alipanda kufanya yake kabla ya kupokelewa na mtoto mzuri kutoka Bongo Fleva, Vanessa Mdee ‘V – Money’ ambaye alipiga shoo matata.

Vanessa hakufanya makosa, aliamsha mashabiki pale alipoimba nyimbo zake maarufu Nobody But Me, Niroge na Siri.

Wa mwisho kupanda jukwaani kabla ya Ali Kiba kumpisha Breezy alikuwa ni mkali kutoka Nigeria, Wiz Kid ambaye alitumia muda mwingi kucheza juu ya spika zilipokuwa pande mbili za jukwaa kuu.

Hii ni mara ya tano sasa, Wiz Kid anapata shavu la kupafomu jukwaa moja na mkali huyo kutoka Marekani na hivyo kuweka rekodi ya peke yake kuwa mwenye bahati ya kupiga naye kazi jukwaani mara nyingi.

Mapema Juni, mwaka huu Breezy alimpa Wiz Kid mchongo wa kushiriki kwenye Tamasha la One Hell of a Nite lililofanyika mjini Amsterdam, Uholanzi.

Kabla ya hapo walishakutana kwa nyakati tofauti kwenye shoo nyingine tatu zilizofanyika nchini Nigeria na nyingine Ghana.

ALI KIBA

Mbali na Chris Brown, staa aliyekuwa na mvuto mkubwa zaidi katika onesho hilo ni Ali Kiba ambaye alipanda jukwaani na kuimba kwa ustadi wa hali ya juu.

Kiba aliimba nyimbo zake Aje na Mwana ambazo aliimba na mashabiki huku wakimshangilia.

Mishale ya saa 6 usiku, baada ya kuimba nyimbo hizo mbili pekee, Kiba aliaga mashabiki ambao wengi waliamini alikuwa akitania, maana wasanii wote waliotangulia waliimba zaidi ya nyimbo tatu.

“Thank you and goodbye (nawashukuru sana, kwaherini),” alisema Kiba kisha zikafuata kelele za mashabiki.

Tofauti na matarajio ya wengi, Kiba alikuwa hatanii, alirudi hadi mwisho wa jukwaa, kisha akafuata njia ya kushuka akiongozana na madensa wake.

“Kibaaa arudiiii, Kiba aje… Kiba, Kiba….,” kelele hizo kutoka kwa mashabiki zilisika.

CHRIS BROWN HESHIMA

Breezy hakufanya makosa, katika muda wote aliokuwa jukwaani alitumia vizuri kila sekunde yake kwa kuangusha shoo ya nguvu.

Akiwa na madensa wake, Breezy aliimba nyimbo zake maarufu kama With You, Kiss Kiss, Don’t Wake Me Up, Next To You, Internation Love na Love More zilizowainua mashabiki pande zote za viwanja hivyo.

Mashabiki wa kike walichanganyikiwa na kupiga kelele pale msanii huyo alipovua tisheti yake na kubaki kifua wazi, ambacho sehemu kubwa alikuwa amechora tattoo.

TAMASHA LA BEI MBAYA

Tamasha la juzi mjini hapa, licha ya kuwa na kiingilio kikubwa sana, wahudhuriaji walikuwa wengi kiasi katika eneo la kawaida, lakini upande wa VIP na VVIP eneo lote lilifurika watu.

Kiingilio cha chini katika onesho hilo kilikuwa ni Shilingi 10,000 za Kenya (karibu 220,000 za Tanzania), VIP Shilingi 20,000 (karibu 440,000) huku wale wa VVIP wakilipa Shilingi 50,000 (karibu 1,100,000).

Siku mbili kabla ya onesho hilo, watayarishaji wa shoo hiyo walitoa ofa kwa wateja kununua tiketi kwa elekroniki kwa punguzo la Shilingi 5,000 (karibu 110,000 za Tanzania) lakini baada ya muda mfupi sana ziliisha.

Wakazi wa hapa Mombasa wanaeleza kuwa, ilikuwa miongoni mwa maonesho machache yenye viingilio vikubwa kupata kufanyika mjini hapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles