*Faida lukuki za uwekezaji huo zatajwa, kinaachoendelea ni wivu tu
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kwani mbali na kuongeza mapato pia utachochea ajira ikiwamo ufanisi wa bandari hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Jumapili Julai 30, 2023 jijini Mwanza na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, katika mkutano wa nane wa Chama hicho kutoa elimu kuhusu mktaba wa uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai.
Pamoja na Chongolo, wengine walioshiriki mkutano huo ni mawaziri na wabunge wa chama hicho ambao wamebainisha faida na manufaa ambayo taifa na Watanzania watayapata kupitia uwekezaji huo.
Chongolo amesema katika uwekezaji huo baadhi ya watu wametoa maoni ya aina mbalimbali yakiwemo ya msingi na tija ambapo Chama hicho kimeiagiza Serikali kupitia mambo ya msingi kuruhusu yaingie na kufanya uboreshaji ili kupata tija zaidi kwa sababu mkataba siyo biblia wala msaafu.
“Niseme kwamba tunasisitiza uwekezaji lakini kama kuna jambo la kuongeza tija kwenye mkataba na mtu ana maoni juu ya hilo lichukuliwe na liongezwe, lakini kuna watu hawana nia njema wanataka kutukwamisha sisi hatuko tayari tuliahidi lazima ilani yetu itekelezwe kwa kiwango tulichoahidi.
“Sasa wanaanza kutoa matusi, ndugu zangu niwaombe sana hiki chama ni kikubwa chenye heshima kubwa tusiingie kujibizana nao tusihangaike na matusi wanayoyatoa lazima tusimame imara tunyooshe mguu tufikie kile tulichowaahidi Watanzania,” amesema Chongolo.
Amesema ukosoaji unaoendelea wameshauzoea kwani walipata upinzani kama huo walipotaka kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme mto Malagalasi, mradi wa umeme bwawa la Kihansi, mradi wa Bomba la Mafuta, Bwawa la Mwalimu Nyerere na reli ya Kisasa kwani wakosoaji wengi hawataki taifa lipige hatua za maendeleo ili waendelee kulinyonya.
“Wenzangu wamesema kuhusu bandari na mimi nataka niseme na nisisitize hapo, ndugu zangu hili la bandari msimamo wa CCM kasi ya utekekezaji wake iongezwe ili tuanze kupata matunda tunayoyategemea, kwenye utekelezaji wa ilani mtu yeyote anayejaribu kutukwamisha lazima tusimame pamoja tumetembea kwenye maeneo mbalimbali msukumo wa kuliunga hili ulikuwa mkubwa, wana CCM wameonyesha uhitaji mkubwa wa mabadiliko,” amesema Chongolo.
Mwanza wapo tayari kwa uwekezaji
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla akizungumza kwaniaba ya Wakuu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, amesema:
“Sisi wakazi wa Kanda ya Ziwa tunaunga mkono uborehaji na uwekezaji unaofanyika bandari ya Dar es Salaam, tunaipongeza Serikali kinachoendelea kwa sasa ni wivu tu wa maendeleo na siasa, uongo ukiachwa unakuwa ukweli kwahiyo tunawajibu,” amesema Makalla.
Mawaziri nao wafunguka
Awali,
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula amewatoa wasiwasi Watanzania na kuwahakikishia kuwa uwekezaji huo ni salama na ardhi ya Watanzania itaendelea kuwa salama kwani haitomilikishwa kwa mwekezaji yoyote huku akiwataka kuukubali na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan.
“Rais ameshaweka mlango wazi wale ambao wameshaelewa wataelimishwa na ambao bado wataendelea kuelimishwa, ardhi ya Tanzania iko salama na watanzania wako salama fungueni mioyo yenu kwa ajili ya uwekezaji na taifa letu lisonge mbele,” amesema Mabula.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali na bunge walizingatia maoni na wasiwasi wa watanzania hivyo uwekezaji huo ni salama kwani taifa lina uzoefu wa kutosha wa kushughukikia mambo ya uwekezaji na inao wataalam wanaohakikisha mara zote maslahi ya nchi yanazingatiwa.
“Wabunge tulipitisha jambo hili baada ya kulifanyia tafakuri ya kutosha baada ya kujiridhisha kwamba lina manufaa kwa nchi, wananchi na kwenye majimbo yetu. Faida yake ni kwamba tunachangamsha shughuli za kiuchumi nchini, kuongeza mapato ya serikali, tunaongeza uwezo wa kushusha na kupakia mizigo na kushawishi nchi jirani kutumia bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuongeza ajira na idadi ya Watanzania wanaofaidika katika sekta ya usafirishaji,” amesema Prof. Mkumbo
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhil Maganya amesema kuwa: “Wananchi wenzangu wa Kanda ya Ziwa tumuombee Rais, tumtie moyo, tumpe faraja aendeleze nchi yetu bandari ni yetu ni kwa ajili ya uchumi wetu na sasa asitokee mtu mwingine akatutoa kwenye reli. Mlioko hapa mtapata elimu na mtaendelea kupata elimu ili mkawe mabalozi,”
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi anayesimamia Uchukuzi, Godfrey Mwakibete amesema hakuna bandari yoyote inayobinafsishwa bali itapangishwa hususan bandari ya Dar es Salaam peke yake, bandari nyingine na zile zilizopo Ziwa Viktoria zitakuwepo na hazitoguswa, ambapo bandari hiyi lazima iboreshwe kutokana na ushindani uliopo kati yake na bandari za Mombasa na Durban.
“Tunataka kuhakikisha mizigo yote tani milioni 60 ambayo hatuipati ipite kwetu, kwa sasa hatuna teknolijia ya kisasa pale bandarini, hatuna vifaa vya kisasa, mifumo haiwasiliani, lazima tumpate mwekezaji ambaye atakuwa na uwezo mkubwa zaidi atakayetatua hizo changamoto,”
“Bandari ya Dar es Salaam ikiboreshwa Kanda ya Ziwa imeboreshwa, bandari ya Dar es Salaam ikiboreshwa bandari za kanda ya ziwa zimeboreshwa na shughuli za kiuchumi zitaimarika, ili tuingize fedha nyingi lazima tuwekeze bandari ya Dar es Salaam,” amesema Mwakibete