Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameitaka Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) kuanza kuwakata fedha wakandarasi wanaochelewa kukamilisha ujenzi wa barabara za mikoa kama zilivyoainishwa kwenye mikataba ya ujenzi iwe fundisho kwa wengine.
Chongolo ametoa agizo hilo jana katika Kata ya Mwaniko Kijiji cha Vuchama wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mwanga- Kikweni- Vuchama inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 28.9.
Akikagua barabara hiyo inayojengwa na wakandarasi tofauti akiwemo M.S/Builders Limes works, Chongolo alisikitishwa na kasi ndogo ya mkandarasi anayejenga sehemu ya kipande cha barabara hiyo ambayo ujenzi wake unapaswa kukamilika Agosti 8, mwaka huu.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi huo, Meneja Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando alisema barabara hiyo ni ya hadhi ya mkoa na ina urefu wa kilometa 28.9.
Alisema utekelezaji wa ujenzi unaendelea lakini mkandarasi anajenga kwa kusuasua na kutoa sababu mbalimbali kama vile uwapo wa mvua.
“Mkandarasi alitoa sababu kwa mradi kutokamilika awali na tukamuongezea muda hadi Agosti 8, mwaka huu na baada ya hapo tutaanza kumkata fedha asilimia kwa sababu amekiuka makubaliano ya mkataba wa ujenzi,” alisema Kyando.
Akizungumzia ujenzi huo, Chongolo alisema: “Ifikapo Agosti 8, siku ambayo anatakiwa kazi iwe imekamilika, kama itakuwa bado anzeni kumkata fedha na hii ifanyeni kwa wakandarasi wote nchini ambao wanachelewesha kukamilisha kazi kulingana na mikataba yao.
Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo (CCM) alisema ujenzi wa barabara hiyo ni ahadi ya rais wa awamu ya nne na hadi sasa ujenzi wake bado unasuasua.