24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

CHOMBO: WATALII KILIMANJARO HUKUMBWA NA UGONJWA WA CELEBRE EDEMA

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


SEKTA ya utalii nchini imekuwa ikichangia asilimia 17.5 katika pato la Taifa kwa mwaka.

Juhudi za uchangiaji huo zimefanywa na Serikali, mashirika yanayosimamia sekta hiyo kama TANAPA, Ngorogoro, kampuni binafsi na wadau mbalimbali wakiwamo waongoza watalii (Guide tourists) na wapagazi (Porters).

Kama ilivyo kwa biashara nyingine, utalii nao ni bidhaa inayohitaji kuuzwa ndani na nje ya nchi kwa kuutangaza, kutoa huduma nzuri na mambo mengine yatakayofanya mteja avutiwe ili arudi au alete watu wengine.

Katika mahojiano na MTANZANIA hivi karibuni, Kiongozi Mkuu wa Watalii, Faustine Chombo, anayefanya kazi na Kampuni ya Utalii ya Zara ya mjini Moshi anasema, kazi hiyo inahitaji kutanguliza diplomasia.

“Unapokuwa kiongozi wa watalii unatakiwa kuwa mwana diplomasia wa hali ya juu, kwani nje ya hapo unaweza ukaharibu kila kitu kuanzia kazi uliyonayo mpaka taswira ya taifa lako,” anasema Chombo.

Anatoa mfano wa tukio la mgeni mmoja aliyekuwa amefika kituo cha Gilman’s akielekea Stella hatimaye Uhuru Peark alijikuta akishikwa maradhi yanayopatikana katika miinuko mikubwa.

Anasema ugonjwa huo unaoitwa “Celebre edema”  hukimbilia zaidi kwenye kichwa cha mtu na hivyo kujikuta mtalii akitaka kukushambulia kwa ngumi.

“Ukiwa mlimani juu, unaweza kushangaa mgeni akitaka kukupiga ngumi, sasa kama hayajui maradhi ya aina hiyo unaweza kuamua kuzikunja kumbe mwenzako ameathirika.

“Hii imenitokea mara tatu, ya kwanza nilikuwa na watalii saba tukiwa kituo cha Gillman’s niliona dalili za ugonjwa huo kwa mgeni mmoja.

 “Nilimshauri arudi, cha ajabu aliniambia kama sitamruhusu kuendelea akishuka atawasilisha malalamiko yake na atahitaji afidiwe fedha,” anasema Chombo mwenye uzoezi wa miaka 20 katika kazi hiyo.

Chombo aliyefika kileleni Mlima Kilimanjaro zaidi ya mara 400 anasema, kuugua kwa mtalii huyo kulimpa wakati mgumu hasa akichukulia angeweza kupoteza uhai wake.

Kutokana na uzoefu wake, anasema alilazimika kumueleza ukweli kwamba yupo tayari akadai fedha kuliko afie mlimani akiwa chini yake.

“Kwa kweli tulibishana na tatizo wageni wanapolalamikia kuhusu rejesho la fedha kampuni zetu huwa zinawasikiliza bila kujua mazingira yaliyosababisha.

 “Nilitoa kalamu na karatasi nikampa aweke saini yake juu ya lolote litakalompata huko tuendako kwamba litakuwa juu yake.

“Wageni wengine waliniunga mkono tukaendelea mpaka Uhuru Peark. Sasa wakati wa kurudi yule mtalii alianza kukinga ngumi akitaka kunishambulia, nilifanya juhudi za kumkamata lakini akaponyoka na kukimbia kwa kasi.

 “Hapo tulikuwa tukitoka Uhuru Peark kwenda Stella, kwa bahati nzuri alikuwa akianguka kwenye miamba katika kumkimbiza nikiwa na wenzangu tulimkamata na kumfunga mikono kwa nyuma,” anasema Chombo.

 

Anasema mara baada ya kufanikiwa kumkamata kadri walivyokuwa wakimshusha chini ndivyo naye alivyozidi kupata nafuu na kujisikia vizuri tofauti na mwanzo.

 “Tulipofika kambini mwenyewe alijua amefanya kosa hivyo alikuja kuomba msahama. Sasa kama huna uzoefu wa kazi na kuongozwa na diplomasia unaweza kuvuruga kila kitu,” anasema na kuongeza:

 

“Kazi ya kuongoza watalii si jambo dogo, kwasababu ‘guide’ huwa tunakutana na wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kumbuka kila mtu huwa anakuwa na tabia zake,” anasema.

Anazitaja dalili za ugonjwa kwa mtalii ni kuonekana kama mtu aliyetumia kilevi ambapo akiulizwa swali au kuonyeshwa vidole huwa hana uwezo wa kutoa jibu kwa wakati huku mazungumzo yake yakiwa tofauti.

Chombo anamshukuru Mungu kumuwezesha kufanya kazi hiyo bila kupoteza mgeni licha kuwa na historia kubwa ya kuongoza lilikuwa la wageni kutoka Marekani.

“Kundi langu kubwa kabisa kuliongoza lilikuwa na watalii 85 hawa niliwaongoza kwa mara moja na kati yao 82 tulifika nao kileleni kwa wakati mmoja,” anasema Chombo.  

Chombo anajivunia kuongoza viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwamo wastaafu kupanda Mlima Kilimanjaro.

Akiwa katika kazi hiyo, anasema anafarijika kupandisha mlimani watu wenye vyeo na elimu kuliko yeye ambao hulazimika kumsikiliza yeye na timu yake.

“Kwanza ni haki yangu ya msingi kwa sababu ndio eneo ninalolifanyia kazi,” anasema Chombo huku akitaja baadhi ya viongozi aliowahi kuwapandisha Mlima Kilimanjaro.

 

Anawataja kuwa ni pamoja na Mkuu wa Majeshi wa zamani Meja Jeneral mstaafu, George Waitara. Wengine ni kundi la waliokuwa mabalozi wa Tanzania akiwamo Balozi Adadi Rajabu, Batilda Burian, Rajabu Mwingi na wengineo.

Chombo anasema bahati nyingine kwake ni kitendo cha kumuongoza Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kupanda Mlima Kilimanjaro ambapo kwake  ilikuwa historia zaidi.

 

“Mwaka 2012 tukiwa na kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Geita tulipita njia ya Machame nikiwa naongoza ugeni huo na Mzee Mwinyi, sikuwahi kutegemea kama ingetokea katika maisha yangu ya kazi hii.

“Yote hayo ni mipango ya Mungu naamini ipo siku pengine hata Rais Dk. John Magufuli nitamuongoza kupanda Mlima Kilimanjaro au hata Rais wa Marekani,” anasema Chombo.

Chombo anatoa ushauri kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kupanda Mlima Kilimanjaro badala ya kuona utalii huo ni wa watu kutoka nje ya nchi.

“Watanzania wanatakiwa kutambua kuwa hii ni haki yao ndio maana hata gharama hazilingani na za wageni kutoka nje ya nchi…waje kuona zawadi waliyopewa na Mungu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles