30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

CHIPSI MAYAI INAPANDA, BONGO MUVI INASHUKA!

ILI ufanikiwe inakupasa uwe mbunifu. Huwezi kufanikiwa katika jambo lako ukiendelea kubaki na mawazo yaleyale. Lazima ukubali kujifunza, kuchukua ujuzi na kuutumia ili uzidi kupaa kimafanikio.

Huko nyuma muziki ulitamba mbele ya Bongo Fleva, lakini mwanzoni mwa mwaka 2000, upepo ukabadilika na filamu kuwa juu. Lakini kwa sasa filamu zimeshuka na muziki kurudi kwenye hadhi yake ya awali.

Wasanii wa muziki na hasa Bongo Fleva wanatamba zaidi ya wenzao wa Bongo Muvi hivi sasa. Kuna mahali walikosea hawa Bongo Muvi na kelele zinapigwa kila kukicha, wakati wakifanya makosa na hata sasa baada ya kushuka thamani.

Enzi uigizaji ukitamba, watu walikuwa na ratiba ya vipindi vyote vya kwenye runinga. Makundi kama Nyota Ensemble ‘Mambo Hayo’, Fukuto Arts Promotion ‘Rangi ya Chungwa’, Kaole Sanaa Group ‘Maisha’  na Chemchem Arts Group ‘Kidedea’ yalikuwa yakitamba.

Achana na makundi hayo, pia kulikuwa na makundi kutoka nchini Kenya waliokuwa wakirusha michezo yao runingani kama Tausi, Vioja Mahakamani na wasanii wengine kutoka Kenya.

Kimsingi makundi haya yaliibua mastaa wengi waliopata kutamba kuanzia mwaka 2005 na kuendelea kwenye soko la filamu za Kibongo. Baadhi wanaendelea kutesa mpaka sasa.

Waigizaji wakawa na mafanikio makubwa, wakawaacha mbali kabisa wale wa muziki. Ushindani ulikuwa mkubwa sana kwa wasanii wetu.

Ukisikia filamu mpya imetoka, huna shaka, unanunua haraka maana unajua watu watakuwa wameumiza vichwa kuhakikisha wanapiku kazi zilizotangulia au zilizopo sokoni wakati huo.

Lakini cha kushangaza, ghafla tu filamu zimeshuka thamani. Filamu zilezile zilizokuwa zikiuzwa kwa Tsh. 5,000 mwaka 2005, leo miaka 12 baadaye zinauzwa kwa Tsh. 3,000.

Kuna hoja eti uchumi umeshuka, ndiyo maana sinema zimeshushwa bei ili Watanzania wengi wamudu kununua. Huu ni utetezi usio na mashiko kabisa.

Ikiwa mwaka 2005, bei ya chipsi mayai (kwa maeneo ya kawaida kabisa) ilikuwa Tsh. 1200, leo hii ni Tsh. 2500, iweje bei ya filamu ishuke?

Haihitaji akili nyingi kufikiri, ukweli hapa ni kwamba filamu zimeshuka viwango. Filamu mbovu nyingi. Sababu hiyo imefanya walaji wa filamu kupungua baada ya kuona ubabaishaji kila siku.

Huu ndiyo ukweli ambao wadau, wasanii na watayarishaji wa filamu wanatakiwa kuufanyia kazi.

Mashabiki hao waliowakimbia ndiyo wale ambao wanapenda kuangalia tamthilia za wasanii kutoka mataifa mengine kiasi cha ninyi kuamua kupinga uingizwaji wa tamthilia hizo nchini.

Angalieni tatizo lilipo. Huko nyuma mlizingatia yote ya muhimu; hadithi zilikuwa nzuri, zenye ubunifu na kuvutia. Waongozaji wenye uwezo na wasanii waliovaa uhusika vema.

Leo hii wameridhika, soko linaporomoka kila siku. Ni wakati wa kushtuka. Anzeni kujitathimini mjue mlipokosea ili mjirekebishe.

Njia za kuelekea kimataifa zilikuwa tayari wazi, hata sasa hazijajifunga bado. Shtukeni muendelee. Bongo Fleva inazidi kuchanja mbuga.

Wadau wamemisi zile raha za filamu za kuvutia. Stori za kipekee kama Fungu la Kukosa nk. Ni hapo tulipomfahamu Riyama. Acheni lawama, msimtafute mchawi, ni kubadili gia angani tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles