29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

China yawasha moto upya maandamano Hong Kong

BEIJING, CHINA

BUNGE la China limesema mahakama za Hong Kong hazina mamlaka ya kuamua uhalali wa kikatiba wa sheria za mji huo, ikiwa ni pamoja na amri ya kuzuia watu kufunika nyuso wakati wa maandamano.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Kamati ya Bunge la China, ilisema suala la iwapo sheria za Hong Kong zinazingatia katiba linaweza kuamuliwa na Bunge la Umma.

Taarifa hiyo inakuja siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Hong Kong kutoa uamuzi juzi kuwa marufuku ya kufunika nyuso wakati wa maandamano ni kinyume na katiba.

Kiongozi wa Hong Kong, Carrie Lam, alipendekeza marufuku hiyo wakati wimbi la maandamano lilipoongezeka Oktoba, mwaka huu.

Taarifa hiyo ya Bunge la China inaweza kuchochea zaidi maandamano mjini Hong Kong ambako raia wana wasiwasi kuwa Serikali kuu ya China inaingilia uhuru wa mji huo wenye utawala wa ndani.

Katika uamuzi wa juzi, Mahakama ya Hong Kong ilibaini marufuku hiyo iliyotangazwa chini ya sheria za dharura inakiuka sheria ya msingi na inazuia haki za raia bila sababu ya msingi.

Majaji wawili, Godfrey Lam na Anderson Chow walisema utekelezaji wa marufuku hiyo unashindwa kuweka uzani kati ya haki za raia zinazopigiwa upatu na hatua zinazochukuliwa kuzuia haki hizo.

Vifunika nyuso vimekuwa vikivaliwa na waandamanaji ili kuzuia kutambuliwa pamoja na sababu za kiusalama kutokana na polisi kutumia kila wakati mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha ili kuwatawanya.

Amri hiyo ilihuishwa kutoka sheria ya hali ya hatari wakati wa utawala wa kikoloni wa Uingereza na waandamanaji wengi walikaidi kuitekeleza.

Mwanaharakati mashuhuri wa demokrasia mjini Hong Kong, Joshua Wong aliutaja uamuzi wa mahakama kuwa ushindi wa nadra wa kisheria kwa waandamanaji.

Polisi mjini Hong Kong juzi wamekivamia Chuo Kikuu kilichokuwa kikidhibitiwa na waandamanaji baada ya kushindwa usiku kucha kuingia eneo hilo.

Miale ya moto iliyotokana na mfululizo wa milipuko ilionekana kutoka ndani ya majengo pindi maofisa wa polisi wa kutuliza fujo walipoingia viunga vya chuo hicho mapema leo alfajiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles