BRUSSELS, UBELGIJI
MAJADILIANO magumu yanatarajia kugubika mkutano wa kilele kati ya Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini hapa.
Ni kinyume na mkutano wa kilele kati ya China na viongozi wa Afrika Septemba 2018 ambao vyombo vya habari vya China viliuita ‘mkutano wa familia’, ndoto za pamoja na urafiki wa kudumu”.
Licha ya miezi kadhaa ya maandalizi, Umoja wa Ulaya hautarajii kupata kile inachotarajia kutoka China, ambapo ni pamoja na kuheshimiwa haki za binadamu, biashara ya haki na uwezekano wa kuwekeza.
Mtaalam wa masuala ya China kutoka taasisi ya Mercantor ya Taaluma za China mjini Berlin, Ujerumani, Mikko Huotari anasema:”Matarajio ni finyu mno.’
“Kuna hali jumla inayojitokeza katika mkutano kama huu wa kilele na China, huwezi kuashiria mapema matokeo yatakuwa ya aina gani. Na yadhihirika kuna uwezekano mkubwa hata taarifa ya pamoja kutotolewa mwishoni mwa mkutano.”
Ingawa mada kama mabadiliko ya tabia nchi, siasa ya nje na usalama mtandaoni zinatarajiwa kujadiliwa, kipaumbele katika mkutano huu wa 21 wa ni kuhakikisha watu wanatendeana sawa katika shughuli za biashara na uwekezaji.
“Inamaanisha ikiwa kampuni za China zinafaidika na masoko wazi ya Ulaya, hali iwe vivyo hivyo kwa kampuni za Ulaya nchini China.
Haki za binadamu bado ni mwiba katika uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya, China na Umoja wa Ulaya hawakubaliani bado kuhusu suala la haki za binaadam.