Na JONAS MUSHI -DAR ES SALAAM
SERIKALI ya China inakusudia kukiendeleza kwa kukijengea majengo mapya na kuweka miundombinu ya kisasa Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT) ili kiwe na hadhi ya chuo kikuu.
Mpango huo unahusisha vyuo vikuu vitano vya usafirishaji barani Afrika ambavyo vimo katika mpango wa Serikali ya China ya kujenga au kuendelezwa vyuo vya usafirishaji kwa hadhi ya chuo kikuu.
Mwakilishi wa Serikali ya China wa masuala ya uchumi na biashara, Lin Zhiyong ambaye jana alipotembelea NIT kilichopo Mabibo, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, alisema ujenzi wa majengo mapya katika chuo hicho unatarajia kuanza miaka mitatu ijayo na ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa China, Xi Jinping, aliyoitoa akiwa Afrika Kusini mwaka juzi.
Alisema licha ya ushindani wa kupata nafasi hiyo, Tanzania itapewa kipaumbele cha kwanza kwa sababu ya urafiki wa muda mrefu baina yake na China.
“Tumefurahi kuona jitihada zinazofanywa na NIT pamoja na mpango wa upanuzi wa chuo hiki, hivyo napenda kuwahakikishia kwamba Tanzania itapewa kipaumbele cha kwanza kati ya vyuo vitano vya usafirishaji vitakavyojengwa barani Afrika miaka mitatu ijayo.
“Kilichobaki ni chuo kiandae andiko la mradi huo na kililete katika ubalozi wetu, tutapitia na kuwapa utaratibu mwingine wa kufanya ili wataalamu wetu waje waanze ujenzi,” alisema Zhiyong.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk. Leonard Chamurino ambaye aliambatana na Zhiyong katika ziara hiyo, alisema kazi waliyonayo ni kuionyesha Serikali ya China utayari wa kuendeleza chuo hicho ili kiweze kutoa programu nyingi za usafirishaji kuanzia ngazi ya cheti hadi uzamivu.
Awali, mkuu wa chuo hicho, Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa, alieleza mpango mkakati wa kukipanua chuo hicho ili kuweza kutoa programu nyingi za mafunzo ya usafirishaji.
Alisema chuo kinakusudia kuwa na shule kuu tano za usafirishaji na uhandisi wa ndege zitakazotoa mafunzo kuanzia cheti hadi uzamivu na kwamba ili kutimiza azma hiyo ni lazima kuendeleza rasilimali watu na miundombinu.
Alisema chuo kina eneo la heka 46 lakini ni asilimia 30 tu ya eneo hilo iliyoendelezwa na kina mpango wa kununua heka 1,500 zilizopo Kijiji cha Masugulu, Bagamoyo mkoani Pwani.
“Tunataka tuendeleze hizi asilimia 70 ya heka 46 na tumetengeneza ramani ya ujenzi wa majengo mapya ya utawala, madarasa, makazi ya wanafunzi na viwanja vya michezo,” alisema Prof. Mganilwa.