25.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

CHINA KUJENGA CHUO CHA USAFIRISHAJI

Balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Younging

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

CHINA kwa kushirikiana na Tanzania inatarajia kujenga chuo kikubwa zaidi cha usafirishaji nchini, lengo likiwa ni kusaidia kusukuma jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo na kuzalisha wataalamu kwenye nyanja hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Balozi wa China nchini, Dk. Lu Younging wakati wa hafla ya fursa za ajira iliyofunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kukutanisha kampuni za China, lengo likiwa ni kutoa ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu ikiwa ni awamu ya pili.

Balozi Younging alisema ni jambo la faraja kuona Serikali ya Tanzania ikiweka nguvu kwenye sekta ya elimu na kwamba vijana wengi wanaendelea kupata fursa ya kujiunga na elimu ya juu.

“Serikali zetu mbili zinashirikiana kujenga chuo cha elimu ya ujenzi mkoani Kagera ili kufundisha watu wenye vipaji kwa lengo la maendeleo ya ujenzi nchini.

“Pia kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli kwa sasa, tumekubali kushirikiana katika kujenga chuo kikubwa cha usafirishaji nchini kwani tumepata mafanikio makubwa katika sekta ya uwekezaji na biashara,” alisema Balozi Younging.

Akizungumzia fursa za ajira, alisema wanatambua kuwa hilo ndiyo lengo la kutoa elimu, hivyo hawana budi kushirikiana katika kuhakikisha kuwa wahitimu wanapata ajira ili kuboresha uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.

“Licha ya kwamba ni kazi ya Serikali kuhakikisha inatoa ajira kwa wahitimu, lakini pia sisi tutashirikiana na Tanzania kwenye eneo hili la ajira kupitia makampuni yalipo hapa, hivyo mimi na Serikali yangu tutaendelea kuwa mabalozi wazuri kuwaalika wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, aliishukuru Serikali ya China juu ya mpango huo, huku akiwasisitiza wahitimu na walioko vyuoni kuwa wabunifu kutokana na hali ya soko la ajira ilivyo kwa sasa.

“Tunaamini kuwa hii ni fursa ya kipekee ambayo wahitimu mnapaswa kuitumia vizuri ili kupata ajira ambayo itapunguza changamoto kubwa iliyopo licha ya ukweli kuwa Serikali imekuwa ikifanya kila linalowezekana kuhakikisha inapungua.

“Hivyo kama ilivyo nia ya Serikali ni kuona wahitimu wakipata ajira, pia tunaamini kuwa kuanza kufundishwa kwa lugha ya kichina hapa nchini itasaidia Watanzania wengi kujiajiri kwani dunia ya sasa inahitaji watu wenye ubunifu na wenye kujua vitu mbalimbali ikiwamo lugha,” alisema.

Aliongeza kuwa hiyo ni fursa hadhimu ambayo inatakiwa kutumiwa vyema na wahitimu wote na kwamba kama Serikali wanatarajia kuona vijana wengi wakipata ajira.

Akizungumzia fursa hiyo ya ‘Job Fear’, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk. Leonard Akwilapo, alisema ni nafasi nzuri kwa wahitimu wa vyuo kukutana na kupata fursa za ajira.

“Hii ni awamu ya pili kwani mwaka jana pia ilifanyika na wahitimu wengi kupata fursa za ajira ndani na nje ya nchi, hivyo hata mwaka huu tunatarajia wengi watapata nafasi ya kuhojiana na waajiri na hatimaye kupata ajira.

“Pia ni changamoto kwa walioko shuleni kuongeza bidii katika masomo yao na kuongeza stadi za kutosha ili kuajirika ndani na nje ya nchi kwani hii imetusaidia kama Serikali kupunguza makali ya ajira,” alisema Dk. Akwilapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles