Na Norah Damian, Mtanzania Digital
Ubalozi wa China kwa kushirikiana na Shirika linalohudumia wanawake na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu (FCC) wametoa msaada wa vyakula, sare za shule na dawa kwa wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko.
Masaada huo wenye thamani ya Sh milioni 18 unajumuisha sare za shule, sare za michezo, mchele, maharage, mafuta, ngano, sabuni za kufulia, dawa za binadamu na sufuria.
Akizungumza Novemba 25,2022 wakati wa kukabidhi msaada huo, Balozi wa China, Chen Mingjian, amesema China na Tanzania ina historia ndefu ya urafiki na msaada huo ni mwendelezo wa kudumisha ushirikiano wao.
Naye Mkurugenzi wa FCC, Emmanuel Wiso, amesema shirika hilo lililoanzishwa mwaka 2019 limekuwa likihudumia wanawake na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wakiwemo wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kuhakikisha wanakuwa salama.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mchanganyiko, Sezaria Kiwango, amesema shule hiyo ina wanafunzi 616 na kati yao wenye ulemavu ni 141.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo wana vitengo vine vya wenye ulemavu ambavyo vina wanafunzi wasioona (65), ualbino (6), viziwi wasioona (15) na ulemavu wa akili (55).
Mwalimu huyo ameomba wasaidiwe vifaa vya Tehama kurahisisha ujifunzaji kwa watoto, mashine ya kufulia nguo na gari la shule.