Na Grace Semfuko
-Dar es Salaam
BARAZA la Biashara la China-Afrika, limesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini, ipo haja kwa wawekezaji wengi wa China kuwekeza kwenye viwanda ili kuongeza tija kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Xian Ding, alisema kutokana na kuwepo kwa mazingira hayo, wamehamasisha wawekezaji wengi wenye mitaji mikubwa na wameshaanza kuonyesha nia.
Ding aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wa ziara ya wanafunzi wa Chuo cha Kilimo na Maliasili (CANRI) walipotembelea katika kiwanda cha uzalishaji wa chakula cha Mifugo cha Huatan kinachomilikiwa na Wawekezaji Raia wa China kilichopo Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
“Wafanyabiashara wengi wanapenda kuwekeza, wanajiuliza tukawekeze wapi, sisi tunawaambia waje Tanzania kwani kuna mazingira mazuri, kuna amani, kuna sera nzuri na pia kubwa zaidi sisi ni marafiki tangu enzi za Mwalimu (Julius) Nyerere na Mao Tsetung ” alisema Ding.
Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo Xu Zhixian alisema licha ya kuhamasisha wawekezaji toka China kuja kuwekeza nchini, pia wanahamisha wachina waliopo Tanzania kubuni miradi ya kuwekeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda cha Huatan, Cheng Meng Yan, aliwataka wafugaji kufuata kanuni za kisasa za ufugaji ikiwa ni pamoja na kuwa na uangalizi wa karibu wa mifugo.
Kwa mujibu wa Kituo cha uwekezaji Tanzania TIC, China inaongoza kwa kuweka mitaji mikubwa nchini kwa zaidi ya dola bilioni 5.8 duniani katika uwekezaji kuanzia mwaka 1990 mpaka 2017.
Ripoti zinaonyesha kuwa China ina miradi 723 ikitoa ajira 87,126 kwa thamani ya dola milioni 5 962.74, ikifuatiwa na Uingereza yenye miradi 936 iliyozaa ajira 274,401 kwa thamani ya dola milioni 5,540.07 na Marekani ikiwa na miradi 244 iliyozalisha ajira 51,880 kwa thamani ya dola Milioni 4,721.15.
Katika Ukanda wa Afrika Mashariki nchi inayoongoza kwa mitaji ni Kenya ikishika nafasi ya saba kwa kuwa na mitaji kwa kuwa na miradi 508 iliyozalisha ajira 50,713 yenye thamani ya dola Milioni 1,676.22.