BAADA ya tetesi kwamba msanii wa hip hop, Rashidi Makwiro ‘Chidi Benzi’ aliyekuwa akipatiwa matibabu ya kuacha utumiaji wa dawa za kulevya katika Kituo cha Life and Hope Rehabilitation Organization kilichopo Bagamoyo ametoroka, Meneja wa Diamond, Babu Tale ameibuka na kukanusha tuhuma hizo.
Licha ya kukanusha tuhuma hizo, Babu Tale aliyeshirikiana na Kalapina kumpeleka katika kituo hicho msanii huyo, amekiri kumhamisha na kumpeleka kituo kingine ambacho hakutaka kukitaja kwa madai kwamba hadi atakapoitisha mkutano na waandishi wa habari.
“Chid Benzi hajatoroka kama watu wanavyofikiria, isipokuwa nimemhamisha, nimempeleka sehemu nyingine kutokana na sababu mbali mbali, lakini kwa sasa sipo tayari kuliongelea hilo hadi nitakapofanya mkutano na waandishi wa habari na kuelezea sababu za kufanya hivyo,” alisema Babu Tale bila kueleza siku atakayoitisha mkutano na waandishi.
Naye mmoja wa wasimamizi wa kituo hicho alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema, ni kweli msanii huyo hayupo kituoni hapo lakini amechukuliwa na Babu Tale huku akitaka aulizwe sababu za kumhamisha kituoni hapo kwa kuwa ndiye aliyempeleka.
“Hakutoroka ila amechukuliwa na Babu Tale, amempeleka kituo kingine sasa sababu za kufanya hivyo aulizwe Babu Tale kwa kuwa yeye ndiye anayejua sababu zake,’’ alieleza msimamizi huyo.