CHID BENZ, NANDO WAMEONYESHA UKUBWA WA TATIZO

0
756

chidi-chidi

NA CHRISTOPHER MSEKENA

HABARI kubwa ya burudani wiki hii ni ile ya kusambaa kwa picha za watu maarufu kwenye sanaa ya muziki ambao ni rapa Rashid Makwilo ‘Chid Benz’ na mshiriki wa shindano la Big Brother, Ammy Nando.

Picha zile zilionyesha utofauti wa miili yao wakiwa wazima na mwonekano wao wa sasa baada ya kuathirika na dawa za kulevya. Ukweli ni kwamba, hali zao ni mbaya kiafya.

Mjadala mkubwa uliibuka kwenye mitandao ya kijamii huku watu mbalimbali maarufu wakitoa yao ya moyoni. Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ambaye alimtembelea mama mzazi wa Chid Benz na kupitia mtandao wa Instagram alitoa mtazamo wake juu ya suala hili la dawa za kulevya.

“Inasikitisha sana kuona wapo vijana wanaona wenzao wakiangamia na kuteketea kwenye hili janga lakini wanajaa jeuri, kiburi, tambo na kujipa upofu wa kutoona athari zake.

“Unaweza kuimba au ukafanya kitu kingine chochote na ukafanikiwa bila kutumia dawa za kulevya.

“Inasikitisha zaidi kuona kuna familia zinawalinda wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya, Taifa linapoteza viongozi, wachezaji, wasanii, walimu wakubwa wa leo na kesho wa nchi yetu,” aliandika Waziri Mwigulu.

Hali kadhalika mastaa kibao wa filamu na muziki walionekana kulizungumzia suala hili ambalo kiukweli limepoteza vipaji vingi vya muziki, ukiacha hao akina Chid Benz na Nando kuna Ferooz, Ray C na Daz Baba ambao waliwahi kuwika kwenye muziki lakini leo wamepotezwa na dawa za kulevya.

Tatizo kubwa ni kwamba jamii inalifanya siri jambo hili japokuwa haiwi siri tena baada ya mtu kuathirika. Watu wanaogopa kulizungumzia ndani ya familia zao.

Wazazi wanashindwa kuzungumza na watoto wao juu ya suala hili na matokeo yake tunapoteza watu waliokuwa na ndoto ya kufanya makubwa kwenye Taifa.

Tatizo la dawa za kulevya halipewi nafasi ya kujadiliwa kwenye jamii yetu. Mara nyingi suala hili huibuka pale ambapo watu maarufu kama hawa wasanii wanapoathirika.

Sidhani kama bila kusambaa zile picha mbaya za Chid Benz na Nando, ishu hii ingejadiliwa kwa mapana haya. Mastaa hawa ni sehemu ndogo mno ya jamii kubwa inayopotea kwenye janga hili.

Lazima kuwe na mikutano au kampeni endelevu za kutoa elimu kwa jamii juu ya janga la dawa za kulevya. Mfano wa zile kampeni za kupambana na Ukimwi ambazo zimezaa matunda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here