28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 15, 2024

Contact us: [email protected]

Chenge, Tibaijuka, Ngeleja kikaangoni leo

mnglFredy Azzah na Shabani Matutu, Dar es Salaam
KAMATI Ndogo ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Mwenyekiti wake Philip Mangula, leo inawahoji makada wa chama hicho waliopokea mgawo wa fedha za Escrow.
Makada ambao watawekwa kikaangoni kutokana na kupokea mgawo huo, ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Wiliam Ngeleja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge.
Uamuzi huo umekuja baada ya Kamati Kuu ya CCM (CC), iliyokutana wiki iliyopita visiwani Zanzibar ambapo pamoja na mambo mengine, iliagiza kuhojiwa kwa makada wake hao wenye nafasi ndani ya chama kama njia ya kujenga nidhamu, maadili na uwajibikaji kwa masilahi ya chama na umma.
Katika kikao hicho, makada hao waliopokea mgawo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira, watatakiwa kutoa maelezo ya kina kuhusu walivyopokea fedha hizo.
Mbali na hilo, vigogo hao ambao kila mmoja amefunguliwa faili na chama kupitia Idara ya Maadili ya CCM chini ya mkuu wake, Masudi Mbengula, watatakiwa kutoa utetezi huo huku swali kubwa likiwa kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu na chama kwa kukiuka maadili.
Profesa Tibaijuka ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu, anatarajiwa kuhojiwa huku makovu yake yakiwa hayajapona ya kufutwa uteuzi wake na Rais Jakaya Kikwete, wa uwaziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Desemba 22, mwaka jana baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka maadili ya uongozi.
Katika mgawo huo wa Escrow, Profesa Tibaijuka alipokea Sh bilioni 1.6, Chenge naye akipokea kiasi kama hicho, huku Ngeleja akipokea Sh milioni 40.4.
Chenge na Ngeleja wote ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), ambapo kwa mujibu wa mazimio ya Kamati Kuu iliyokaa Zanzibar, makada hao pamoja na Tibaijuka ikiwa watakutwa na hatia, suala hilo litafikishwa mbele ya Kikao cha KamatiFebruari mwaka huu na kupewa adhabu, ikiwamo kuvuliwa nyadhifa zao ndani ya chama.
Mwishoni mwa Desemba mwaka jana, Profesa Tibaijuka kupitia Katibu wake Kazi Maalumu, Nassoro Hussein, aliweka wazi kuwa hayuko tayari kujiuzulu wadhifa wake wa ujumbe wa CC wala NEC.
Ngeleja ambaye ni mjumbe wa NEC, pamoja na kuhojiwa na chama chake, lakini pia amekuwa na malumbano na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kuhusu uamuzi wa kujiuzulu uenyekiti wa kamati hiyo.
Hata hivyo, Makamu mwenyekiti wake, Godbles Blandes, aliweka wazi suala hilo na kusema kuwa hakuna uamuzi uliofikiwa na kamati wa kumtaka Ngeleja kujiuzulu hadi pale watakapopata maelekezo ya kikakuni kutoka kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amewashangaa wenyeviti wa kamati za Bunge walioshindwa kujiuzulu kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow, akisema hali hiyo inaonyesha wasiwasi kama Bunge linaweza kuisimamia Serikali.
Katika kikao cha Bunge kilichopita, baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, Bunge lilipitisha maazimio manane ambapo azimio namna nne lilitaka kuvuliwa nyadhifa zao za uenyekiti wa kamati za Bunge wabunge waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo.
Wenyeviti hao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Ngeleja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa.
“Mimi siku zote msimamo wangu ni utekelezaji wa maamuzi ya Bunge, Naibu Spika (Job Ndugai) ameshasema kwamba Spika (Anne Makinda) atafanya uamuzi, mimi kama mwenyekiti wa PAC ninasema maamuzi ya Bunge lazima yatekelezwe, na Bunge linatakiwa kuwa mstari wa mbele kutekeleza maazimio yake yenyewe.
“Ninashangaa wabunge ambao wanahoji maamuzi yao wenyewe, kama hatuwezi kusimamia maamuzi yetu wenyewe tutawezaje kuisimamia Serikali?” alihoji Zitto.
Kwa upande wake, Naibu Spika, Job Ndugai, aliliambia MTANZANIA kuwa hatima ya wenyeviti hao itatolewa wiki hii na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
“Spika atalitolea ufafanuzi wa kutosha tu, nisingependa kumtangulia kwa sababu juma hili linaloanza lazima atatoa maelezo na hata Bunge likianza atatoa maelezo ya utekelezaji wa maamizio ya Bunge, hili ni jambo ambalo tulipotoka ni mbali tunapokwenda ni karibu.
“Maamizio ya Bunge lazima yatekelezwe maana siyo ya Ndugai wala ya nani, ni suala la utekelezaji tu na utaratibu wa utekelezaji wake,” alisema Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles