30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

CHENGE: NITAMPA TAARIFA SPIKA UKAMATAJI WABUNGE

Na MAREGESI PAUL, DODOMA

MWENYEKITI wa Bunge, Andrew Chenge, amesema atampa taarifa Spika wa Bunge, Job Ndugai, juu ya tabia ya polisi kuwakamata wabunge  wanapokuwa na makosa.

Amesema ingawa polisi wanajua taratibu za kukamata watuhumiwa, wanaweza wasiwakamate wabunge  vikao vya Bunge vinapokuwa vikiendelea, badala yake wakawakamata wakati mwingine kwa sababu wanajua makazi yao.

Chenge alitoa taarifa hiyo bungeni jana alipokuwa akijibu mwongozo wa Mwenyekiti ulioombwa na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema).

Katika maelezo yake, Chenge alisema kuna haja pia ya kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na Bunge kwa kuwa mihimili hiyo ina majukumu yanayofanana.

“Mheshimiwa Heche nimekusikia ingawa hukueleza kwa undani, lakini najua suala hili lilianza jana na Naibu Spika akalitolea ufafanuzi.

“Ushauri wangu katika hili, kuna haja ya kuwa na uhusiano mzuri kati ya Bunge na Serikali, lakini pia nakuomba Heche umwandikie Katibu wa Bunge umweleze mapendekezo yako ili yafikishwe katika Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa mjadala zaidi.

“Baada ya hapo, uongozi wa Bunge unaweza kujadiliana na Serikali kwa sababu kama polisi wanamhitaji huyu, wanaweza kusema tunamhitaji huyu na wakaamua kumkamata wakati mwingine kwa sababu wanajua tunapoishi.

 “Naelewa suala hili ni zito, kwa hiyo nitalifikisha kwa Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mwongozo wangu,” alisema Chenge.

Awali, Heche alisema kama Bunge halitachukua hatua  wabunge wanapodhalilishwa, utafika wakati Bunge litaanza kudhalilishwa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge ni chombo kinachoheshimika   duniani kwa sababu ndicho chombo kinachotunga sheria na kupitisha bajeti ya Serikali.

“Lakini sasa heshima ya Bunge inaanza kupotea kwa sababu  kama mbunge mmoja mmoja anapoanza kupoteza heshima, utafika wakati Bunge zima litapoteza heshima.

“Hii tabia ya wabunge kukamatwa kamatwa ovyo, tena bila taarifa ya Spika, haipendezi na hata wakuu wa wilaya wanawanyanyasa sana wabunge huko majimboni.

“Kwa hiyo, naomba mwongozo wako mheshimiwa mwenyekiti ili uniruhusu niwasilishe hoja yangu Bunge liijadili,” alisema Heche.

Juzi, wabunge wa upinzani walitoka nje ya Bunge wakionyesha kutoridhishwa na majibu ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson, aliyoyatoa   alipojibu taarifa ya kukamatwa kwa wabunge wa upinzani iliyowailishwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Katika taarifa hiyo, Zitto aliwataja wabunge wa Chadema, Godbless Lema wa Arusha Mjini aliyeko mahabusu katika Gereza la Kisongo mkoani  Arusha kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali anayetumikia kifungo cha miezi sita katika Gereza la Ukonga Dar es Salaam na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakati Dk. Tulia akijibu taarifa hiyo, alisema kanuni za Bunge zinataka Spika wa Bunge apewe taarifa za kukamatwa mbunge aliyetenda makosa ya madai na kama siyo makosa ya madai, hakuna haja ya spika kupewa taarifa.

Wakati huo huo, Zitto aliwaambia waandishi wa habari jinsi alivyotoka bungeni juzi usiku baada ya kupata taarifa za kusubiriwa na polisi nje ya Bunge ili wamkamate kutokana na maneno ya uchochezi anayodaiwa kuyatoa wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.

“Nilitoka hapa bungeni saa sita kasoro usiku baada ya ushauriano kati yangu, Katibu wa Bunge na Spika ambaye alikuwa amewasiliana na IGP.

“Baada ya ushauriano huo, IGP alimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma na kumweleza walichozungumza na Spika. Kwa kifupi sitakamatwa tena wala mbunge yeyote hatakamatwa kienyeji kama ambavyo imekuwa ikifanyika na badala yake utaratibu utakuwa ukifuatwa kwa spika kupewa taarifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles