Na Kulwa Mzee, Dodoma
IMEELEZWA kwamba Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM) ataendelea kuwa Mwenyekiti wa Bunge mpaka atakapoitwa na kuhojiwa kuhusu mchanga wa dhahabu wa makinikia.
Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema hayo jana baada ya Rais John Magufuli kuagiza watu wote waliotajwa kwenye kamati ya pili ya makenikia kumtaja Chenge kuwa miongoni mwa viongozi walioisababishia hasara nchi kwenye sekta ya madini.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge, alisema hakuna kanuni inayomzuia Chenge kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bunge kwa sasa.
“Kwa sasa hapana, ataachia nafasi hiyo atakapoitwa kuhojiwa, akishathibitika ndiyo atatoka kwenye nafasi ya uenyekiti,” alisema.
Akizungumzia kuondolewa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge, Mary Mwanjelwa kwenye nafasi hiyo wakati kuna tuhuma za rushwa, alisema alifanya mabadiliko ya kawaida ambayo kwa mujibu wa kanuni anaruhusiwa.
“Kipindi kile kamati ya Mwanjelwa ilihusishwa na rushwa lakini mabadiliko nilifanya ya kawaida hayakuhusu hizo tuhuma,” alisema.
Mwanjelwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, aliondoka kwenye nafasi hiyo na ile ya uenyekiti wa bunge baada ya kamati yake kutuhumiwa kwa rushwa kisha kuhojiwa na Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Utaratibu unaeleza kwamba Ofisi ya Spika ikishapata taarifa ya mbunge au kiongozi fulani wa Bunge kuhitajiwa na chombo cha dola na spika akatoa ruhusa hiyo, mbunge huyo ataachia madaraka yake na kubaki na ubunge tu.
Mwenyekiti wa Kamati ya pili ya makanikia iliyohusisha wanasheria na wachumi, Profesa Nehemiah Osoro alisema wakati taifa likipitisha sheria na mikataba ya ovyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa Andrew Chenge.
Pamoja na Chenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge anayeshughulikia Kamati ya Sheria Ndogo, Mwanasheria Mkuu mwingine wa Serikali alikuwa Johnson Mwanyika, na Manaibu Wanasheria Wakuu, Felix Mrema na Sazi Salula.