LONDON, ENGLAND
MABINGWA wa Ligi Kuu nchini England, Chelsea, wamekamilisha uhamisho wa kiungo wa klabu ya Monaco na timu ya Taifa ya Ufaransa, Tiemoue Bakayoko.
Uhamisho wa mchezaji huyo umekamilika kwa kitita cha pauni milioni 40, ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 114 za Kitanzania. Mchezaji huyo amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano kuitumikia klabu huyo ya Stamford Bridge.
Kocha wa Chelsea, Antonio Conte, alimtaka Bakayoko kuwa miongoni mwa wachezaji ambao anawania saini zao katika kipindi hiki cha usajili, ili kuweza kuboresha safu yake ya kiungo kuelekea msimu mpya wa Ligi, hivyo usajili huo unaweza kumfanya kiungo wa timu hiyo wa muda mrefu, Nemanja Matic, kuondoka kwa kuwa hatakuwa na nafasi tena.
Japokuwa Bakayoko amejiunga na kikosi hicho, lakini hajaitwa kwenye kikosi cha timu hiyo katika michezo ya kirafiki ya maandalizi ya msimu mpya kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti.
Mchezaji huyo, ambaye anapenda kutumia jezi namba 14, alitumia mtandao wa klabu hiyo ya Chelsea kuonesha furaha yake ya kujiunga na klabu hiyo katika kipindi hiki cha majira ya joto.
“Nina furaha kubwa kufanikisha uhamisho wangu na kujiunga na klabu kubwa kama hii. Nimekuwa nikikua na kuiangalia Chelsea, hivyo kujiunga na kikosi hiki kwangu ni sehemu kubwa ya mafanikio, nilikuwa naipenda tangu nikiwa na umri mdogo.
“Kwa sasa ni kuangalia jinsi gani nitafanya kazi yangu vizuri na kocha mwenye uwezo mkubwa pamoja na wachezaji wenye majina makubwa,” alisema Bakayoko.
Bakayoko amekuwa mchezaji wa tatu kujiunga na klabu hiyo wakati huu wa majira ya joto, baada ya klabu hiyo kufanikiwa kuzipata saini za aliyekuwa kipa wa Manchester City, Willy Caballero na beki wa AS Roma, Antonio Rudiger.