BAADA ya Chelsea kupokea kichapo cha mabao 3-1 juzi dhidi ya Southampton, kocha Jose Mourinho amesema endapo klabu hiyo itamfukuza basi itakuwa imefanya kosa kubwa.
Mourinho amesisitiza kuwa yeye ni kocha sahihi wa kuifundisha klabu ya Chelsea japokuwa imepoteza baadhi ya michezo. Chelsea imeanza vibaya msimu huu katika michuano ya Ligi Kuu nchini England na Ligi ya Mabingwa, lakini anaamini kuwa bado ana nafasi ya kufanya vizuri.
“Hiki ni kipindi kigumu kwa klabu ya Chelsea, endapo itachukua maamuzi ya kunifukuza kazi basi watakuwa wamefanya kosa kubwa la kumfukuza kocha bora ambaye hawatopata tena.
“Ujumbe ni kwamba, matokeo haya ni kosa la kocha, lakini tunatakiwa kuwa pamoja ili kuweza kuirudisha timu. “Sina uhakika kama tutaweza kutetea ubingwa wa ligi kutokana na pointi ambazo tumeachwa na timu ambayo inaongoza ni nyingi, lakini tutahakikisha tunapigania nafasi za juu,” alisema Mourinho.
Hata hivyo, kocha huyo amesema hana mpango wa kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya anayoyapata. “Kwanini nijiuzulu? Siwezi kufanya hivyo kwa kuwa Chelsea haiwezi kupata kocha bora zaidi ya mimi, kuna makocha wengi duniani wazuri lakini sio bora hivyo siwezi kuondoka.
“Nina sababu mbili za kunifanya niendelee kubaki hapo, moja kwa sababu ninaipenda klabu hii na pili ni kazi yangu,” aliongeza Mourinho.