Na Mwandishi Wetu
-DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya usambazaji wa mashine za EFD ya Checknocrats Ltd, imesema kuwa taarifa iliyotolewa kuhusu kuondolewa kwa mashine hiyo ilitaja jina la kampuni yao.
Kutokana na hali hiyo imesema licha ya wao kuwa wasambazaji wa mashine hizo, lakini ilishamaliza mkataba na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka mmoja uliopita na kwamba mashine zao bado zipo katika ubora na hazipo kwenye orodha hiyo.
Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Balraj Bhatt, alisema kuwa kutolewa kwa jina la kampuni yao kwenye orodha za mashine za EFD si sawa,
“Katika orodha ya majina ya mitindo ya mashine ya EFD moja ya mfano inaonekana kama “Checknocrats” ambayo ni jina la kampuni yetu si mfano wa mashine ya EFD,” alisema Bhatt katika taarifa yake.
Wiki iliyopita Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza uamuzi wa kuziondoa mashine za EFD ambazo zinadaiwa kuchezewa na watu wasiowaminifu na kuondoa taarifa sahihi na mauzo kama njia ya Serikali kupata mapato.