Kenya
Gavana wa zamani wa Baringo nchini Kenya, Benjamin Cheboi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Ustawi wa Kilimo (ADC).
Aidha, aliyekuwa Gavana wa Isiolo, Doyo Godana ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi mjini Eldoret.
Uteuzi huo umefanywa leo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambapo amewateua wakuu wapya 106 wa mashirika mbali mbali ya serikali, Ikulu imethibitisha.
Katika uteuzi huo pia, Rais Kenyatta amemteua Meja Mstaafu Julius Karangi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hazina ya Hospitali (NHIF) huku Peter Kinyua akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Shirika la Misitu (KFS).
Wengine na nyadhifa zao mpya kwenye mabano ni; Mudzo Dzili (Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Unyunyizaji Maji Mashamba, aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Uchaguzi, Lilian Zaja (Kamishna katika tume ya Udhibiti wa Kawi) na Carol Omondi (Bodi ya Kampuni ya Mafuta). Wakuu hao watahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.