26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

CHAVEZ KATIKA KASHFA YA KUMILIKI GENGE LA UNGA

 

Hayati Hugo Chavez

 

Na Luqman Maloto,

HUGO Chavez ni shujaa wa itikadi ya Ujamaa mpaka kifo kilipomchukua Machi 5, 2013. Watu wenye imani isiyoyumba ya falsafa zote za Mrengo wa Kushoto (Left-Wing), kwao Chavez alikuwa jemedari kinara dhidi ya Ubepari.

Chavez aliuchukia ubepari na aliijenga Venezuela kuwa Taifa la Kijamaa kupitia vyama vya Movement for the Fifth Republic kati ya mwaka 1997 mpaka 2007 kisha United Socialist Party kuanzia mwaka 2007 hadi roho yake ilipotengana na mwili wake.

Hata sasa, mwili wake ukiwa umepumzishwa kwenye makaburi ya Cuartel de la Montana, yaliyopo Caracas, Venezuala. Chavez anakumbukwa kama mwasisi wa Serikali ya Bolivarian.

Desemba 17, 1982, Chavez aliasisi Vuguvugu la Kimapinduzi la Wana-Bolivar-200 (Revolutionary Bolivarian Movement-200) ambayo kwa kifupi hutambulika kwa jina la MBR-200.

Vuguvugu hilo, Chavez alilianzisha kwa kushirikiana na maofisa wenzake wa jeshi, Felipe Carles na Jesus Hernandez. Jina Bolivar, walilitumia kama heshima kwa Simon Bolivar, ambaye alikuwa mtawala wa kijeshi na kisiasa, aliyefanya kazi kubwa kuasisi mataifa ya Venezuela, Bolivia, Colombia, Ecuador, Peru na Panama katika miongo minne ya mwanzo ya Karne ya 19.

Maono na nadharia za kiutawala za Bolivar ambaye alijulikana pia kama El Libertador, ndiyo sababu ya Chavez na wenzake kuita harakati zao kuwa Vuguvugu la Kimapinduzi la Wana-Bolivar.

Februari 4, 1992, Chavez akisaidiwa na Serikali ya Cuba, chini ya hayati Fidel Castro, walifanya jaribio la kwanza la mapinduzi ya kumwondoa aliyekuwa Rais wa Venezuela, Carlos Perez. Kushindwa kwa jaribio hilo, kulisababisha Chavez na wenzake wafungwe jela.

Novemba 27, 1992, jaribio la pili lilifanyika kumwondoa madarakani Perez, wakati Chavez akiwa jela. Vijana watiifu wa MBR-200, walipokea maagizo kwa Chavez, aliyesuka mpango akiwa jela. Hata hivyo, jaribio hilo pia lilikwama.

Julai 1997, MBR-200 walibadili jina na kujiita Movement for the Fifth Republic (MVR) ili kitambulike kuwa chama cha kisiasa, lengo likiwa kumwezesha Chavez kugombea urais katika Uchaguzi wa Rais wa Venezuela mwaka 1998.

Uchaguzi ulifanyika Desemba 6, 1998, Chavez alishinda kwa asilimia 63.5 dhidi ya aliyekuwa Gavana wa Jimbo la Carabobo, Venezeula, Henrique Romer.

Kuanzia hapo, Chavez aliamua kuifanya Venezuela kuwa nchi ya Ujamaa, akifuata nyayo za Castro wa Cuba ambaye alikuwa Mkomunisti kindakindaki na mfuasi wa falsafa za ‘manabii’ wa Ukomunisti, Carl Marx na Vladimir Lenin, yaani Marxist-Leninist.

Chavez alijitangaza kuwa Marxist kisha kutengeneza ushirika na Serikali za Kijamaa za Evo Morales (Bolivia), Rafael Correa (Ecuador) na Daniel Ortega wa Nicaragua.

Hiyo ndiyo sababu ukimgusa Chavez, unaweza kukutana na hasira za wafuasi wa itikadi za Mrengo wa Kushoto. Misimamo ya Chavez dhidi ya Marekani ambalo ni taifa kiranja la Ubepari duniani, ni jambo ambalo humfanya atetewe na Wajamaa kokote duniani.

CHAVEZ MUUZA UNGA

Sakata la Narcosobrinos nchini Venezuela ndilo ambalo lilifanya watu wengi kuamini kwamba kweli Chavez alikuwa muuza dawa za kulevya. Japokuwa enzi za uhai wake alikuwa akishutumiwa tu bila kuwapo kwa ushahidi wa kutosha.

Narcosobrinos ni maneno ya Kispaniol (Spanish au Castilian) yenye maana “Wapwa Wauza Unga”. Narco ni Wauza Unga na Sobrinos ni Wapwa.

Narcosobrinos ni maneno yaliyotumiwa na vyombo vya habari kutambulisha sakata la wapwa wa Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flores, waliokamatwa na kilogramu 800 za cocaine Novemba 10, 2015.

Wapwa hao wa Rais Maduro, wanaitwa Efrain Antonio Campo Flores na Francisco Flores de Freitas, walikamatwa na maofisa wa kikosi cha ujasusi cha kupambana na dawa za kulevya cha Marekani (DEA), walipokuwa Port-au-Prince, Haiti, wakijaribu kuingiza mzigo huo wa cocaine Marekani.

Novemba 18, 2016, wapwa hao wa Rais Maduro walikutwa na hatia. Maelezo yaliyotolewa mahakamani ni kuwa wapwa hao walikuwa wametumwa tu, kwamba wahusika ni Rais Maduro na mkewe Cilia ambaye ni Naibu Rais wa Bunge la Venezuela.

Ilielezwa kuwa fedha hizo za cocaine zilikuwa kwa ajili ya kusaidia familia ya Rais Maduro kuendelea kubaki madarakani. Ikaongezwa kuwa familia ya Rais Maduro inaongoza mtandao mpana wa unga ambao imeurithi na kuuendeleza kutoka kwa Chavez.

Mhariri wa Washington Post, Jackson Diehl, alipata kuandika habari kuhusu mtandao mpana wa dawa za kulevya kwenye Serikali za Amerika Kusini, akasema kuwa Chavez na timu yake ya Serikali ya Mapinduzi ya Bolivarian, walikuwa wanaongoza genge hatari la wauza unga.

Kwa mujibu wa Diehl, mtandao wa Bolivarian, ulianza kutengeneza fedha nyingi miaka 1980 walipoanza harakati za kuchukua madaraka nchini Venezuela, na kwamba fedha nyingi walizopata ziliwezesha Chavez kushinda Urais mwaka 1998.

Ilibainishwa kuwa mtandao huo wa Chavez una nguvu kuliko genge lolote la unga katika Bara la Amerika Kusini kwa sababu lenyewe linamiliki Serikali. Hata sasa baada ya Chavez kufariki dunia, mrithi wake Maduro anaendeleza ‘libeneke’.

DAWA ZINAONGOZA SERIKALI

Wauza unga wamekuwa wakiingia ndani ya Serikali nyingi na kusimika watawala wao. Zipo nchi marais wamedhaminiwa na mitandao ya dawa za kulevya, vilevile kuna marais wanaendesha magenge (cartels) ya dawa za kulevya kwa siri.

Suala la wauza unga kuwa na nguvu nyingi kwenye Serikali, mfano wake upo kwa bilionea raia wa Mexico, Joaquin Guzman ‘El Chapo’, anayeongoza genge la Sinaloa. Kila anapokamatwa hutoroka.

Bajeti ya El Chapo kutoroka jela inatajwa kufikia mpaka dola 500 milioni, yaani Sh1.1 trilioni. Kwamba akishawekwa ndani, maofisa wa Serikali ya Mexico na nyingine, wanamwaga fedha kama njugu, mwisho ulinzi unalegezwa halafu ‘mtu mzima’ anatoroka.

Hivi sasa Marekani wamemkalia kooni, kwani alipokamatwa tu Wamarekani walikwenda kuimarisha ulinzi na Januari 19, mwaka huu alihamishiwa Marekani ambako sasa ni wazi fainali yake imewadia.

Ukichunguza mtandao wa El Chapo unaona kuwa vituo vyake vya mauzo ni Marekani, Bara la Asia, Afrika Kusini, eneo la Magharibi ya Afrika, vilevile ana kituo Brazil. Kwa nguvu kubwa ya El Chapo Afrika, unaweza kubashiri kuwa na Tanzania kuna watu wake.

Siri kubwa ni kuwa wauza unga wana fedha nyingi. Biashara yao inawapa faida kubwa na utajiri wa haraka ndiyo maana wanakuwa na jeuri ya kuweka mapandikizi kwenye Serikali mbalimbali na wengine wanaongoza kabisa. Mfano hai ni Venezuela.

Kumradhi: Toleo lijalo tutaendelea na mfululizo wa simulizi za ukuu wa Mfalme wa Cocaine duniani, Pablo Escobar mpaka kifo chake. Tunaomba radhi kwa kushindwa kuendelea leo kutokana na sababu za juu ya uwezo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles