NA WINFRIDA MTOI
FEBRUARI 9, mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison  Mwakyembe, alimteua rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodger Tenga, kuwa mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Tenga ameziba nafasi ya Dioniz Malinzi, ambaye uongozi wake ulivunjwa na Mwakyembe Julai mwaka jana na Sekretarieti ya baraza hilo kuwa chini ya Mohamed Kiganja hadi sasa.
Uteuzi wa Tenga umepokewa kwa mikono miwili na wadau wa michezo, wakiamini kuna kitu kizuri atakifanya kutokana na utawala  wake bora wakati alipokuwa TFF.
Kipindi alichokuwa TFF, Tenga alifanikiwa kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinalikabili shirikisho hilo, huku akisimamia misingi aliyoamini kuwa itaboresha maendeleo ya soka la Tanzania.
Ikumbukwe kuwa, wakati Tenga anaingia madarakani TFF, alikutana na changamoto nyingi, ikiwamo watu kukata tamaa na uendeshwaji wa soka la Tanzania kutokana na migogoro iliyokuwa inaendelea iliyotokana na kutoelewana kwa viongozi chini ya waliomtangulia, kina Muhidin Ndolanga.
Lakini kiongozi huyo kwa muda mchache alioingia madarakani alianza kukabiliana na changamoto hizo kwa uhamasishaji na watu kurejesha imani yao na kupenda mpira.
Uwezo wa Tenga wa kusimamia utawala bora umemfanya aendelee kupendwa hadi sasa na kupewa nyadhifa mbalimbali katika sekta ya michezo kwa kuamini ataleta mabadiliko na mafanikio waliyotarajia.
Hivi sasa kiongozi huyo hakubaliki na Watanzania pekee, bali hata katika mashirikisho mengine ya soka ndani ya Afrika na nje wanaomtumia kwenye kamati tofauti za ushauri wa maendeleo ya soka.
Kwa kutambua umuhimu wa mawazo yake, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limempa Tenga Kamati ya Usimamizi wa Leseni za Klabu katika shirikisho hilo akiwa ndiye Rais wa kamati hiyo.
Hata kitendo cha kuteuliwa mwenyekiti wa baraza la michezo, ni baada ya Serikali kubaini uwezo wake mkubwa na kuamini mawazo yake yatasaidia kuimarisha kitengo hicho, ambacho ni mhimili mkubwa wa michezo hapa nchini.
Imani ya wengi baada ya uteuzi wake ni kwamba, ataweza kutatua matatizo yaliyopo ambayo yaliwashinda viongozi waliopita kulingana na uzoefu wake.
Tenga anafahamu vizuri mabadiliko ya uendeshaji wa sekta ya michezo kwa sasa duniani kote kutokana na kuhudhuria vikao vingi vya kimataifa vinavyohusu maendeleo ya michezo.
Zipo changamoto nyingi zinazohitaji utatuzi katika baraza la michezo, lakini MTANZANIA linakuletea chache ambazo endapo Tenga atafanikiwa kuzipatia ufumbuzi, michezo mingi itapiga hatua.
Sera ya michezo
Mabadiliko ya sera ya michezo ni kitu kilichopewa kipaumbele na serikali iliyopo madarakani, kwa sababu siku chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kupewa wadhifa huo, alikutana na viongozi wote wa sekta hiyo na kuzungumzia suala la kubadilishwa kwa sera.
Alitaka jambo hilo lifanyiwe kazi, kwa kuwa aliona ndiyo changamoto kubwa inayoikabili sekta ya michezo Tanzania na kushindwa kupiga hatua kwa sababu inayotumika ya zamani na inatambua michezo ni ridhaa wakati hivi sasa ni ajira.
Hivyo basi, kutokana na kutokamilika kwa suala hilo hadi sasa tangu Waziri Mkuu alizungumzie, Tenga ana jukumu la kuhakikisha katika wadhifa aliopewa anafanyia kazi jambo hilo, ili kwenda na dunia ya sasa inayotambua kuwa michezo ni ajira na sehemu ya kukuza uchumi.
Kupotea kwa baadhi ya michezo
Kama alivyofanya TFF baada ya kukuta watu wamekata tamaa na jinsi soka linavyoendeshwa na kuwarudisha katika mstari, ndicho anachotakiwa kurudisha michezo ya ndani iliyopotea.
Kuna vyama zaidi ya 50 vya michezo vipo kwenye orodha ya usajili ya BMT, lakini kati ya hivyo ni vichache vinavyoonyesha uhai kwa kuendesha mashindano na kukamilisha kalenda zao za matukio ya mwaka.
Lakini asilimia kubwa vipo tu kwa majina na michezo yake ni kama imepotea kutokana na kutokuwa na hamasa yoyote. Mfano mpira wa vinyoya (badminton) ulikuja kwa kasi miaka ya nyuma, ila kwa sasa umepotea, hakuna mashindano yoyote ya kuuhamasisha.
Tenisi nayo ilikuwa inakuja vizuri, ila kutokana na migogoro iliyoibuka kipindi cha utawala uliomaliza muda wake, ilipoteza mwelekeo, licha ya kupatikana uongozi mpya bado hawajafanya kile kilichotarajiwa.
Ipo michezo mingi iliyokuwa inavuma na imedorora na hata mashindano yakifanyika ni bora liende na ndiyo sababu ya kupata shida inapofikia kwenda kushiriki mashindano ya dunia kama Olimpiki.
Migogoro la ndani ya vyama
Vyama vingi vimekuwa na migogoro  isiyokwisha muda mrefu, hali inayorudisha nyuma maendeleo ya michezo. Kwa mfano ngumi za kulipwa zilipotezwa na hali hiyo.
Kuweka karibu shughuli za vyama na BMT
Hakuna ukaribu wa kati ya vyama vya michezo na BMT na hicho ndio chanzo cha kuvunjwa kwa uongozi uliopita uliokuwa chini ya Malinzi, kila mmoja anafanya shughuli zake mwenyewe hadi pale inapofikia kipindi cha kuhitaji kibali au kutokea tatizo.
Ukaribu wa vyama na baraza lenye mamlaka ya kuhakikisha shughuli zote za michezo zinakwenda, utawafanya BMT kubaini madudu yaliyopo na kuyafanyia kazi kwa haraka.
Udhamini
Kingine kinachochangia michezo kufa ni kukosekana kwa wadhamini wa kusapoti uandaaji wa mashindano ya mara kwa mara, kwa kuwa kila kinachofanyika hivi sasa kinahitaji fedha.
Soka linapiga hatua kwa sababu ya uwepo wa wadhamini, lakini michezo ya ndani imekuwa haipati nafasi hiyo, inachangiwa na viongozi waliopo kwenye vyama hivyo baadhi kukosa elimu ya kutafuta udhamini.
BMT na kamati zake inatakiwa kuangalia upya suala hilo linalorudisha maendeleo ya michezo na vipaji vingi kushindwa kuendelezwa kwa sababu ya ukata.