Changamoto za mazingira SADC kujadiliwa Arusha

0
1063

Eliya Mbonea -Arusha

JUMUIYA ya Mendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), inakabiliwa na changamoto tisa za Hifadhi ya mazingira zinazovuka mipaka ya kiutawala ya nchi.

Kuwapo kwa changamoto hizo kunawaleta pamoja Mawaziri wa Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi za SADC mjini Arusha ili kuendeleza majadiliano ya kutafuta ufumbuzi na mikakati ya pamoja ya kuhifadhi mazingira.

Akiwasilisha mada ya Programu ya Hifadhi ya Mazingira SADC kwa wanahabari, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha(AICC), Ofisa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Thomas Chali alizitaja changamoto hizo kuwa ni uharibifu wa ardhi.

Alisema changamoto nyingne ni kutopatikana kwa maji safi na salama kwa wakazi wa mijini na vijijini, uchafuzi wa mazingira, upotevu wa makazi ya viumbe-pori na bioanuai.

“Uharibifu wa makazi ya viumbe wa majini na uharibifu wa misitu, taka za kieletroniki, matumizi ya kemikali yasiyo salama na Mabadiliko ya tabianchi,” alisema Chali.

Aliutaja wajibu wa nchi wanachama kuwa ni kutumia sheria za ndani, kwa masuala yanayovuka mipaka ya nchi moja kwenda nyingine kushirikiana kwa nchi wanachama kuhakikisha malengo ya itifaki yanazingatiwa.

Alisema nchi wanachama zimepewa fursa kushirikiana kwa njia ya mtengamano na kutumia sheria za ndani hali ambayo haitaathiri mfumo wa sheria wa ndani ya nchi katika kusimamia masuala ya mazingira.

Alisema tayari Serikali imekwishaanza utekelezaji masuala ya mazingira nchini kuwa ni pamoja na kuwapo kwa Sera ya Mazingira ya mwaka 1997, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 na kanuni zake pamoja na mikakati mbalimbali ya kiuhifadhi mazingira (vyanzo vya maji).

Mikakati mingine iliyotajwa ni, mkakati wa Taifa wa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, mkataba wa mabadiliko ya tabianchi na mikataba mingine.

 “Utekelezaji wa miradi ya kuhimili mabadiliko ya mabadiliko ya tabianchi, mradi wa mabasi ya mwendo kasi, miradi ya kufua umeme kwa njia ya maji, miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika maeneo kame.” Alisema Chali na kuongeza:

“Ujenzi wa ukuta wa Bahari wa mita 950 katika Barabara ya Barack Obama na Chuo cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam (mita 480), Ujenzi wa ukuta wa Pangani upande wa Kaskazini wenye urefu wa mita 950, Ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua Dar es Salaam na ujenzi wa kuta mbilli katika kisiwa Panza -Pemba,” alisema.

Mkutano huo wa Mawaziri wa Mazingira, Maliasili na Utalii wa SADC unatarajiwa kuanza Oktoba 21 hadi 25, mwaka huu mjini Arusha ukitanguliwa na  na mikutano ya wataalamu wa sekta ya Wanyamapori ulioanza juzi na jana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here