27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Changamoto wanazokumbana nazo wagonjwa selimundu

Aveline Kitomary

SELIMUNDU (sickle cell) ni ugonjwa unaorithiwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine, hutokana na tatizo kwenye chembechembe nyekundu za damu. 

Ugonjwa huu unaendelea kuongezeka hapa nchini kutokana na wazazi wa pande zote mbili kushindwa kupima vinasaba (DNA) kabla ya kuoana au kuzaa. 

Ikiwa wazazi wote wawili wanachembechembe za sickle cell wanaweza kumzaa mtoto mwenye ugonjwa huo. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, zaidi ya watoto 1,000 duniani huzaliwa wakiwa na selimundu kila siku. 

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, zinaonyesha kuwa hapa nchini watoto takribani 11,000 huzaliwa na ugonjwa wa sickle cell kila mwaka, ambao ni sawa na watoto nane kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa. 

Takwimu hizo zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa sickle cell huku nchi inayoongoza duniani ikiwa ni Nigeria. 

Nchi humo, watoto 20 hadi 30 kati ya 1,000 huzaliwa na tatizo hilo, nchi inayofuata ni India ambayo inaonyesha kuwa watoto 14 kati ya 1,000 wanaozaliwa na selimundu na nchi ya tatu ni DRC Kongo ambapo watoto 13 kati ya 1,000 huzaliwa na ugonjwa kila mwaka. 

Takwimu za wizara ya afya zinaonesha kuwa sasa Tanzania ina wagonjwa zaidi ya 200,000 wenye sickle cell, takribani watoto saba kati ya 100 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki nchini kutokana na tatizo hilo. 

Asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania 100 wana vinasaba vya ugonjwa huu, yaani wana uwezekano wa kupata watoto wenye ugonjwa huo iwapo watakuwa na wenza wenye vinasaba vya selimundu,” anasema. 

CHANGAMOTO WAGONJWA WA SELIMUNDU 

Zipo changamoto kadhaa zinazowakabili wagonjwa wa selimundu kulingana na mazingira wanayoishi. 

Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Selimundu, Arafa Said, anataja changamoto kubwa kuwa ni gharama za matibabu ambazo wengine wanashindwa kuzimudu. 

“Kuna gharama za matibabu kutokana na ada ya kumwona daktari kliniki na dawa muhimu za selimundu hii inawafanya wengine kukosa matibabu kwa kipindi kirefu na kurudisha nyuma mahudhurio ya kliniki kwa wale wasio na bima. 

“Kingine kuna uchache wa wataalamu kwa mfano ni hospitali chache ukienda unamkuta mtaalamu ambaye mgonjwa anapaswa kumwona hivyo, kupata matatizo mengi kama kuharibika kwa viungo, shida ya kifua kubana, maambukizi ya bakteria na mengineyo,” anabainisha Arafa. 

Anasema changamoto nyingine ni vifurushi vya bima ya afya kuwa vya bei ghali na kuwa na kikomo hivyo kushindwa kulipa baadhi ya huduma. 

“Pia kunachangamoto ya vipimo, wagonjwa wengi wanalalamika kupimwa damu tu wanapohudhuria kliniki, ukosefu za vipimo vya moyo pia ni changamoto. 

“Wapo wagonjwa wanaoshindwa kwenda Muhimbili kutokana na gharama za usafiri,” anafafanua Arafa. 

 Arafa anasema wanaendelea kusisitiza uboreshaji wa huduma za selimundu kama uwapo wa vifaa, kuongezwa kwa wataalamu wenye ujuzi na kukuza uelewa wa selimundu. 

“Kingine ni uwapo wa vipimo vya awali kwa wajawazito na watoto, kuboreshwa kwa bima za watu wenye selimundu na uongezwaji wa huduma maeneo ya vijijini 

ili kila mmoja aweze kujua vinasaba vyake tuweze kuvunja mnyororo wa selimundu,” anashauri. 

UHUSIANO SELIMUNDU NA MAGONJWA YA MOYO 

Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohammed Janabi, anasema ugonjwa wa selimundu unaweza kusababisha matatizo ya moyo. 

Anasema hali ya kuwa na selimundu huweza kufanya moyo kuwa mkubwa baada ya damu kuwa kidogo. 

“Pia upo wezekano wa kuharibika kwa valvu za moyo na kunapokuwa na damu chache inabidi moyo uende kasi zaidi ili uweze kuzungusha damu iliyopo hali hii huleta madhara. 

“Lakini lingine ni aina ya chembechembe za damu kuwa hazipo kwenye umbo la kawaida inaweza kugandisha damu na ikiingia kwenye moyo na kuziba unaweza kupata tatizo, kwahiyo changamoto zinazotokea kwenye damu huweza kuleta athari kwa moyo. 

“Zile changamoto zinazotokea kwenye damu ndio zinaleta athari kwenye moyo kwahiyo sickle cell husababisha ugonjwa wa moyo, lakini moyo wenyewe hauwezi kusababisha tatizo hilo,” anabainisha Profesa Janabi. 

Anaeleza kuwa sio wagonjwa wote wa selimundu wanapata magonjwa ya moyo,bali wapo wanaoweza kupata. 

“Karibia kila siku tunaona mgonjwa wa sickle cell kwenye kliniki ya magonjwa ya moyo,” anasema. 

MATIBABU SELIMUNDU NA MOYO KUUNGANISHWA 

Kufuatia hatua ya wagonjwa wengi wa selimundu kupata tatizo la moyo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) kwa kushirikiana na Chuo kikuu kishiriki cha Muhimbi(MUHAS) wameamua kuanzisha kliniki ya pamoja ya magonjwa hayo. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Profesa Janabi anasema kliniki hiyo itasaidia kurahisisha huduma za matibabu kwa wagonjwa hao. 

“Tumekuwa tukijaribu kuanzisha hii programu kwa miaka miwili sasa na dhumuni kubwa ni kwamba kama mnavyofahamu selimundu mtu huwa anazaliwa nayo lakini pia inaweza kumsababishia kupata matatizo ya moyo. 

“Kilichokuwa kinatokea huko nyuma ni kwamba kunakuwa na kliniki ya MUHAS inayofanyika Hospitali ya Muhimbili na wakigundua mgonjwa anatatizo la moyo anaambiwa aje hapa kwenye taasisi kwaajili ya kupangiwa tarehe ya kuonwa. 

“Tarehe anaweza kupangiwa mwezi mmoja hata miwili tukashauriana madaktari na wataalamu wa program ya MUHAS kwamba, haya magonjwa yanaingiliana kwanini tusifanye kliniki moja akawepo daktari wa moyo na wa selimundu, vipimo vikafanyika kwa siku moja anapokuja mgonjwa,” anaeleza Profesa Janabi. 

Anasema ufanyika wa vipimo sehemu moja itasaidia kupunguza muda wa matibabu na kuondoa usumbufu kwa wagonjwa. 

“Watafanyiwa vipimo vyote vya moyo, damu na dawa kutolewa itawarahisishia badala ya kwenda kwenye kliniki mbili na kwa siku mbili tofauti watapata huduma sehemu moja. 

“Tunataka ifiki siku yale magonjwa yanayoingiliana kuwe na kliniki moja ambayo mgonjwa wa figo na moyo ambaye anamatatizo yote mawili ya moyo na kisukari watibike kwa siku moja na sehemu moja. 

Profesa Janabi anaeleza kuwa matibabu ya sehemu moja yatasaidia wataalamu kuweza kujadiliana ili kuweza kutoa huduma haraka. 

“Wataalamu wa magonjwa ya damu na moyo wanapokutana kumjadili mgonjwa wanaweza kujua ni namna gani wanaweze kumsaidia nah ii itaendelea kuboresha tafiti mbalimbali kuhusu magonjwa hayo,”anafafanua Prof Janabi. 

UNYANYAPAA WAPINGWA KWA WENYE SELIMUNDU 

Kwa upande wake mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Ayoub Kibao, anasema unyanyapaa kwa watu wenye ugonjwa wa selimundu haufai. 

“Unyanyapaa kuhusu hili haufai na natia wito uanachwe kabisa lakini lingine watu wapime vinasaba kabla ya kuoana hii itasaidia kutokuzaa watoto wenye selimundu. 

USHAURI WA PROFESA JANABI 

Akitoa ushauri kuhusu gharama za matibabu, Profesa Janabi anasema watatumia mifumo mbalimbali ya kuchangisha fedha kwaajili ya matibabu. 

“Mfano hapa JKCI tunafanya CRDB Marathon, kuna Clouds hizo zote ni kwaajili ya kuchangia gharama za matibabu kwa wale ambao hawawezi, hii pia tukifanya kwa wagonjwa wa selimundu itafaa kupunguza gharama. 

“Lakini pia hapa JKCI huwa tunasamehe kiasi cha Sh milioni 120 hadi 130 kwa mwezi kwaajili ya wasioweza kulipia matibabu na hii hatuwezi kuiachia serikali tu tunafanya na njia zingine za kuingiza kipato,” anaeleza Profesa Janabi. 

Anashauri wagonjwa kuhudhuria kliniki kila inapohitajika na kuzingatia masharti ya matumizi ya dawa zao za kinga. 

“Gharama hazikwepeki lakini tunawashauri watu kuwa na bima ya afya kwa sababu dawa ziko kwenye bima kama tunavyofanya kwa magonjwa ya moyo, kwa wale ambao hawana uwezo kuna taratibu zetu za kufuata,” anamaliza. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles