23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Changamoto hizi kwa walimu ni zaidi ya madawati

maguNA BENJAMIN MASESE

KWA muda mfupi aliokaa madarakani, Rais Dk. John Magufuli amejitahidi kufanikisha mkakati wake wa kuwatoa sakafuni hadi kwenye madawati wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchi nzima.

Mbali ya kuwaondoa vumbini, pia amefuta baadhi ya michango shuleni na kutangaza elimu ya msingi na sekondari kuwa ya bure, kitendo ambacho hadi sasa kimeongeza idadi kubwa ya wanafunzi shuleni.

Hakika asiyepongeza mipango hiyo ya Dk. Magufuli, bila shaka atakuwa na jambo jingine.

Nikiwa kama mzazi mwenye watoto wanaosoma shule ya msingi, nampongeza Dk. Magufuli kwa namna moja au nyingine kwa kuwa awamu nne za utawala zimepita bila kufanikisha suala hilo, ikizingatia nchi ina rasilimali nyingi pamoja na misitu.

Kitendo cha wanafunzi kukaa kwenye madawati kimepunguza gharama kwa wazazi, kwani ilikuwa desturi kwa mtoto anapotoka shuleni lazima nguo zifuliwe, vinginevyo mzazi anapaswa kununua nguo pea tatu za kubadilisha kwa wiki.

Pia walimu wamepata unafuu wa kufundisha kutokana na kuwapo na utulivu wa wanafunzi darasani.

Pamoja na mafanikio hayo, lakini iko changamoto ya madawati hayo. Hii ni kwa upande wa wakuu ambao wamekuwa na malalamiko juu ya agizo lililotolewa kwamba, endapo dawati litaharibika, mwalimu mkuu ndiye atakayewajibika kwa kukatwa mshahara wake.

Malalamiko hayo ya walimu ni ya msingi kutokana na ukweli kwamba madawati mengi yametengenezwa chini ya kiwango.

Wengi ni mashahidi wa hili. Tumeshuhudia wakati madawati hayo yakitengenezwa yalikuwa yakikataliwa kutokana na kutokuwa na ubora.

Pia hivi karibuni, Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire, alisema madawati yaliyotengenezwa baadhi yapo chini ya kiwango kutokana na kutengenezwa kwa mbao nyepesi, kitendo kilichosababisa kuchanika ovyo.
Hatua ya madawati hayo kuanza kuvunjika yenyewe, imeleta hofu kwa walimu wakuu kuhofia kukatwa mishahara yao ambapo wameamua kusukuma mzigo huo kwa wazazi.

Baadhi ya wakuu wa shule wameamua kuweka utaratibu wao kwa kuwakabidhi walimu wa darasa husika ambao pia wameandika majina na kuwakabidhi wanafunzi watatu dawati moja.

Maelekezo kwa walimu wa darasa kwa wanafunzi hao, ni kwamba endapo dawati hilo litaharibika, atakayewajibika ni wazazi wa wanafunzi; wale watatu waliokabidhiwa dawati hilo.

Mpango huo umewekwa na walimu wakuu ikiwa ni kukwepa kukatwa mishahara yao na wengine wamefikia hatua ya kujutia nafasi hizo na kutamani kuwa mwalimu wa kawaida kutokana na kufanya kazi kwa hofu wakati wote.

Hofu nyingine waliyonayo walimu hao ni maelekezo waliyopewa na wakurugenzi wao ambayo hubadilika mara kwa mara, jambo ambalo wanaliona ni usumbufu kwao.

Kuna shule wakati wa mbio za mwenge zilipokuwa Mwanza, walielekezwa na wakurugenzi kuchangia Sh 20,000 kutoka kwenye fedha inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kugharamia elimu bure.

Lakini muda mfupi baada ya agizo la wakurugenzi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliibuka na kukataa mpango huo wa fedha za kugharamia elimu bure kutumika kwenye mbio za mwenge.

Cha kusikitisha kupitia wakurugenzi hao, walitoa maelekezo mengine kwa wakuu wa shule.

Inaelezwa kwamba wakurugenzi waliwaelekeza wakuu wa shule tena kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu, kwamba wahakikishe wanachangia Sh 20,000 kutoka vyanzo vyao vya mapato kwa ajili ya mwenge.

Katika mpango huo, inadaiwa baadhi ya walimu hao walilazimika kuchukua fedha zao mfukoni na kuchangia mbio za mwenge kwa kuwa shule nyingine hazikuwa na chanzo chochote cha mapato.

Kwa hali hii, walimu wakuu wako katika wakati mgumu sehemu za kazi kutokana na kupewa maagizo na wakurugenzi tofauti na kauli za viongozi ngazi za juu wanavyoelekeza.

Pia mwalimu mkuu kutakiwa kukatwa mshahara wake kutokana na kuharibika kwa madawati, si vizuri kwani madawati yenyewe ni mabovu, pia hakuna kitu kisichoharibika.

[email protected] 0683608958

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles