Na NORA DAMIAN
-DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza polisi wamlinde mjane Swabaha Mohamed ambaye alijitokeza mbele yake na kueleza madhila ya kudhulumiwa haki zake za mirathi, Chama cha Wajane nchini (TAWIA) kimeibuka na kusema kuwa hadi sasa kuna kesi 269 za mirathi zilizoko katika mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa chama hicho, Rose Sarwatt, alisema kesi 23 tayari zilitolewa uamuzi lakini baadhi yake zimekatiwa rufaa na zinaendelea katika mahakama mbalimbali jijini humo.
Alisema kuna kesi zaidi ya 300 za mirathi ambazo zinatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.
“Tunampongeza Rais kwa kitendo chake cha kiungwana alichokifanya kwa mjane mwenzetu jana (juzi), tupo katika dhiki kubwa tunamwomba aweke ulinzi kwa wajane wote. Watu wamekosa hofu ya Mungu kila mtu amekuwa anaangalia mambo yake mwenyewe, wamesahau maandiko ya Mungu yanayosema mteteeni mjane na dini iliyo safi ni kumsaidia mjane katika dhiki yake,” alisema Sarwatt.
Chama hicho pia kimeiomba Serikali kuanzisha mahakama ya familia itakayosimamia kesi zote za masuala ya familia zikiwamo za mirathi ili kuondoa msongamano wa kesi mahakamani.
Kulingana na chama hicho kesi moja ya mirathi imekuwa ikichukua wastani wa miaka miwili hadi mitano kukamilika hali waliyodai inasababisha mjane kupoteza muda na kutumia fedha nyingi kuendesha kesi.
“Sheria ya mirathi ifanyiwe marekebisho imepitwa na wakati, tunaomba ipatikane sheria rafiki kwa mjane na mtoto yatima.
“Mume anapofariki inaonekana kama mwanamke mjane hana tena uwezo wa kujisimamia na kuisimamia familia yake jambo ambalo si kweli, mwanya huo umezalisha watu wanaoitwa wasimamizi wa mirathi kutoka kwa familia ya marehemu na wengi wamekuwa wakiangalia masilahi yao bila kujali kuna mjane na watoto yatima,” alisema Sarwatt.
Chama hicho kiliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kuandika wosia ili kuepusha migogoro ya kifamilia pindi inapotokea mmoja wa wanafamilia amefariki dunia.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Mashariki, Mariam Aswile, alisema mila na desturi zimekandamiza wajane kwa muda mrefu na kusababisha kuwa na wakati mgumu kiuchumi, kiafya, kiakili na kisaikolojia.