Berlin, Ujerumani
Chama cha Kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU cha Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kimepata pigo la kihistoria katika chaguzi za majimbo mawili muhimu.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotolewa na maafisa baada ya kura zote kuhesabiwa kufuatia chaguzi za jana Jumapili, chama cha CDU kilipata asilimia 24.1 ya kura katika jimbo la kusini magharibi la Baden-Wuerttemberg na kujikingia asilimia 27.7 ya kura katika jimbo jirani la Rhineland-Palatinate.
Winfried Kretschmann wa chama cha Kijani ameshinda awamu ya tatu kama waziri mkuu wa jimbo la Baden-Wuerttemberg akipata asilimia 32.6 ya kura. Waziri mkuu maarufu wa chama cha Social Democratic SPD, Malu Dreyer ataendelea kuliongoza jimbo la Rhineland -Palatinate baada ya kushinda asilimia 35.7 ya kura.
Katibu mkuu wa chama cha CDU Paul Ziemiak amesema matokeo hayo yanaashiria ghadhabu inayoongezeka, hali ya kutoelewa na kukosa uvumilivu miongoni mwa wajerumani kuhusu usimamizi wa janga la corona huku uungwaji mkono wa chama hicho katika ngazi ya kitaifa ukiporomoka.