24.6 C
Dar es Salaam
Thursday, December 2, 2021

Chama cha Jubilee katikati ya maendeleo na siasa za 2022

ISIJI DOMINIC

CHAMA tawala nchini Kenya, Jubilee, kinapitia katika mawimbi ya mtikisiko huku baadhi ya wanachama wengi wao wakiwa viongozi wa kuchaguliwa na wananchi wakielekeza nguvu zao kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Wengi tayari wameanza kujipanga ukizingatia huu ndiyo muhula wa mwisho wa uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta. Kwa wiki kadhaa sasa, kumekuwa na mgongano wa mawazo ndani ya Jubilee huku wengine wakitaka viongozi wa chama kuwatumikia wananchi kwa kutimiza ahadi walizozitoa na kundi lingini likimnadi Naibu Rais William Ruto kurithi kiti cha urais.

Mambo yalikuwa yanakwenda vizuri na awali Rais Uhuru mara kadhaa alishanukuliwa akisema baada ya miaka yake 10 kumalizika, atampisha Ruto naye aongoze miaka 10 mingine ikiwa ni kejeli kwa upinzani na hususani moja wa vinara wa Muungano wa NASA ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Odinga.

Hata hivyo, tukio la Machi 9, mwaka jana limebadilisha upepo wa siasa nchini Kenya na ule ukaribu wa Uhuru na Ruto unaonekana kupungua kiasi cha kukitikisa Chama cha Jubilee. Washirika wa Ruto wanatafsiri uhusiano wa Uhuru na Raila kama mpango wa kumuondoa Ruto kwenye azma yake ya kuwania urais 2022.

Moja ya makubaliano ya Rais Uhuru na Raila ambao walizika tofauti zao za kisiasa Machi 9, mwaka jana ilikuwa ni kupeleka maendeleo nchi nzima, kuhubiri amani na kuhakikisha hofu inaondoka kila kunapofanyika uchaguzi.

Mwezi uliopita Rais Uhuru alipata mapokezi makubwa alipoenda eneo analotoka Raila ambapo alipata kura chache uchaguzi uliopita na kuzindua miradi mingi ya maendeleo. Mapema mwaka huu, Rais Uhuru akiongozana na Raila walikuwa kaunti ya Mombasa ambapo pia alipata kura chache kutokana na tofauti zake na Gavana Ali Hassan Joho, lakini safari hii akapata mapokezi makubwa.

Kitendo cha Rais kushirikiana na wapinzani wake na kuzindua miradi ya maendeleo kimeonekana kuwakera baadhi ya wabunge wa Jubilee na moja wao ni Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria. Gatundu Kusini ni eneo  analotoka Uhuru.

Katika sherehe za Mkesha wa Mwaka Mpya, Kuria, alimshutumu Rais Uhuru na kusema Serikali yake imeitenga mikoa ambayo walimpigia kura na kupeleka maendeleo mikoa mingine. Ni kauli iliyomghadhabisha Rais Uhuru na kumwambia Kuria na washirika wake kwamba kwa sababu walimchagua wanapaswa kutambua jukumu la Rais ni kupeleka maendeleo kila pembe ya Kenya na si eneo moja tu.

Rais Uhuru ameungwa mkono na idadi kubwa ya watu ambao wamesisitiza wanakubali ushirikiano wake na kinara wa upinzani Raila ambao una malengo ya kuleta maendeleo huku akitaka wale wanaopiga siasa za 2022 kupuuzwa.

Wanaomuunga mkono Rais Uhuru wamehoji wale wanaotaka au wanasubiri wapelekewe maendeleo wanapaswa kujiuzulu kwa sababu wao kama viongozi ni jukumu lao kuhakikisha wananchi wa eneo lao wanapata maendeleo.

Ni dhahiri dalili za nyufa zinazoonekana ndani ya Jubilee huenda ukanufaisha vyama vyingine kama vile ODM na Amani National Congress (ANC) inayoongozwa na Musalia Mudavadi. Ndani ya Jubilee kumeibuka kambi ya ‘maendeleo’ inayounga mkono juhudi za Rais na kambi ya ‘tangatanga’ ambayo ni ya washirika wa Ruto wanaosemekana kufanya mikutano ya siasa nchi nzima kumnadi Naibu Rais kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,646FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles