Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amelitaka Shirika la Bima la Taifa (NIC) kushirikiana na wadau kuhakikisha elimu ya bima inamfikia kila mtu ili kufikia malengo ya Serikali ya asilimia 90 ya Watanzania kuwa na bima pamoja na uelewa ifikapo 2030.
Chalamila ametoa agizo hilo Oktoba 13, wakati akifungua semina ya siku moja ya Mawakala wa Bima nchini (IAAT) iliyoandaliwa na NIC kwa kushirikiana na Mamlaka wa Bima (TIRA).
Amesema NIC inajukumu kubwa la kuhakikisha inahamasisha mawakala wa Bima kutoa elimu kwa jamii na kuhakisha watu wanajiunga katika bima zao ili kusaidia uelewa mpana wa shughuli za bima katika maisha ya kila siku.
“NIC kaeni na wadau wenu mbalimbali mjadili ili kuhakikisha Bima inakuwa muhimu kwa kila Mtanzania aifikirie kama anavyofikiria kula,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa semina hiyo inajadili mpango utakaowezesha kufikia 2030 kila Mtanzania anakuwa na uelewa sambamba na kumiliki bima.
Chalamila amewataka TIRA kujikita kwenye kuwezesha mawakala na siyo kuishia kwenye udhibiti pekee.
Aidha, Chalamila amewapongeza Mawakala wa bima kwa kupiga hatua kwenye bima ya afya na kuwataka wajitahidi kuboresha kwenye bima za magari.
Upande wake Mwenyekiti wa Chama cha mawakala wa Bima nchini(IAAT), Sayi Daud ameiomba Serikali kuondoa tozo mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kwa mawakala hao.
“Ombi letu kwako mkuu wa mkoa tunaomba uzungumze na almashauri watuondolee kodi ya mabango lakini pia kodi ya huduma ambayo kimsingi ilitakiwa itolewe na makampuni,” amesema Daud.
Naye Meneja Ukaguzi TIRA, Frank Shangali amesema sekta ya Bima inatoa ajira zaidi ya 2,000 zinazozalishwa kwa wanafunzi wanaotoka vyuoni kila mwaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bima za Maisha NIC, Hadbert Polepole ambae amemuwakilisha Mtendaji Mkuu wa NIC, amesema wamekua wakifanya kazi na mawakala kwa miaka 60 sasa na kazi hiyo imekuwa na tija kwa taifa.
Amesema NIC imeweza kufikia jamii kupitia mawakala hao hivyo muunganiko wao umekuwa ni tija na fursa.
“NIC tunaendelea kufanya kazi na mawakala lakini pia kuongeza mawakala wapya ili kufikia malengo ya Serikali kuhakikisha sekta ya bima inakua,” amesema Polepole.
Naye Meneja Biashara NIC, Kafiti Kafiti amesema NIC ndio shirika kiongozi katika mashirika ya Bima kwani inazaidi ya mawakala 700 katika bima za maisha na za ajali na magari.