24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yawafukuza uanachama wabunge wanne

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewafukuza uanachama wabunge wake wanne, Joseph Selasini (Rombo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini), David Silinde (Momba) na Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) kwa kukiuka maagizo ya chama na kutoa maneno ya kejeli na kashfa dhidi ya viongozi na maagizo ya chama kwenye vyombo vya habari.

Aidha, kimemvua nafasi zake zote za uongozi ndani ya chama Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha kwa kushiriki kukiuka maagizo ya chama.

Uamuzi huo umetolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika leo Jumatatu Mei 11, ambapo amesema wabunge hao wamekuwa wakijitokeza kwenye vyombo vya habari na kutoa maneno ya kashfa na kejeli dhidi ya maagizo ya chama na viongozi.

“Selasini na Komu wamejipotezea sifa ya kuwa wanachama wao wenyewe kwa kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa hawakubaliani na falsafa ya Chadema wanakubaliana na falsafa ya chama kingine.

“Lakini bado wameendelea kutoa maneno ya kejeli na kashfa na kwa mazingira hayo, chama kimeazimia kuwafukuza uanachama na Kamati Kuu imemuelekeza Katibu Mkuu kumwandikia Spika juu ya uamuzi huu.

“Kuhusu Silinde na Lwakatare, si tu wamekiuka maagizo ya chama bali pia wamekuwa wakijitokeza kwenye vyombo vya hanbati na namna nyingine ya mawasiliano na kutoa maneno ya kashfa na kejeli dhidi ya maagizo ya chama na viongozi. Kamati Kuu ya chama imewafutia uanachama kwa kwenda kinyume na katiba, kanuni na maadili na miongozo ya chama.

“Aidha, Kamati Kuu imemjadili Mariam Msabaha, ambaye ameshiriki kukiuka maagizo ya chama wakati yeye ni Mjumbe wa Halmashauri ya chama alitakiwa kuwa mstari wa mbele kufuata maelekezo, hivyo amevuliwa nafasi zake zote ndani ya chama na atatakiwa ajieleze kuhusu ukiukaji huo alioufanya,” amesema Mnyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles