30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

CHADEMA YALAANI MBOWE KUHUSISHWA DAWA ZA KULEVYA

Na PATRICIA KIMELEMETA – DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelaani hatua ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kutajwa miongoni mwa wafanyabiashara wanaohusishwa na dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vicent Mashinji, amesema kitendo cha kutangaza hadharani kiongozi huyo kuhusishwa na biashara ya dawa hizo, kimekidhalilisha chama chao kwa sababu Jeshi la Polisi lilikuwa na uwezo wa kumhoji na kufanya upekuzi nyumbani kwake kabla ya kumtangaza.

Alisema kutokana na hali hiyo, inaonesha wazi Serikali imedhamiria kuua upinzani, kikiwamo Chadema kwa viongozi wake kuhusishwa na uuzaji wa dawa za kulevya.

“Ikumbukwe Mbowe anaongoza chama kikubwa cha upinzani chenye wanachama zaidi ya milioni tatu, uchaguzi wa mwaka 2015 kilipata kura zaidi ya milioni sita… Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda alikuwa na uwezo wa kuwaambia polisi wamwite na ‘kumsachi’ kuliko kutumia utaratibu wa kumtangaza hadharani.

“Tunalaani na kuamini kilichofanyika ni miongoni mwa mikakati ya kukidhohofisha chama ili kipoteze taswira ya upinzani kwa kuwataja viongozi wake kushiriki kwenye suala hilo, leo Mbowe… kesho hauwezi kujua ni nani… yawezekana nikawa mimi,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kutumia utaratibu wa kudhalilisha viongozi wa Chadema kwa kutumia mwamvuli wa Serikali ili waweze kukichafua chama hicho, jambo ambalo linapaswa kupingwa.

Dk. Mashinji alisema kitendo kilichofanyika ni mwendelezo wa udhalilishaji kwa kutumia mamlaka za Serikali ili waweze kuwakandamiza viongozi wa upinzani, jambo ambalo litaendelea kupingwa na kila mwananchi mwenye mapenzi mema.

Alisema kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limeshindwa kutii sheria kwa kutumia mamlaka waliyonayo kumwita na kumhoji, badala yake wanatumika kisiasa ili kumchafua.

“Chadema itaendelea kulaani suala hilo kwa sababu linaendeshwa kisiasa, bila ya kutumia taratibu za kisheria,” alisema.

Alisema kwa sababu suala hilo ni binafsi, anaamini Mbowe anaweza kulizungumzia yeye mwenyewe kwa undani zaidi ili wananchi waweze kujua ukweli wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles