CHADEMA YAJIHAMI MADIWANI KUHAMA

1
1184

Na PENDO FUNDISHA -MBEYA


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya, kimeitisha kikao cha dharura cha madiwani wake, baada ya kuzagaa taarifa kuwa baadhi ya madiwani hao wana mpango wa kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph China, alisema lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kutaka kuwasikia madiwani ambao wanatajwa kutaka kuhamia CCM.

“Taarifa hizi zilienea kwamba, madiwani wanahama na kujiunga na CCM kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli, chama tuliamua kuitisha mkutano wa dharura na kuwahoji wahusika wote ambao majina yao yanatajwa,” alisema.

Alisema taarifa zilikuwa zinaeleza kwamba madiwani hao walitarajia kujiunga na CCM siku ya mkutano wa CCM uliofanyika jijini Mbeya juzi ukiongozwa na Katibu Mwenezi, Humphery Polepole.

“Mimi kama kiongozi wa chama, sikutaka kuona aibu hii inanikuta, niliamua kuitisha mkutano wa dharura na kuwaeleza ukweli madiwani kwamba miongoni mwenu kuna watu wanataka kujiunga na CCM, hivyo tuelezane humu ndani na sababu za kuondoka tuzifahamu kwani tabia za kuwajaribu wananchi waliotupa dhamana sisi hatuzitaki,” alisema.

Alisema baadhi ya madiwani ambao majina yao yalihusishwa na kuhama, walikanusha madai hayo na kuweka bayana sababu za wao kuhusishwa na tuhuma hizo.

Alisema madiwani hao ambao majina yao yamehifadhiwa, walieleza sababu za wao kuhusishwa na tuhuma hizo lakini hawana mpango wowote na kwamba wamekiomba chama kiwasaidie kuwaeleza wananchi ukweli.

“Huu ni mkakati wa chama, ni bora madiwani wakasubiri 2020 ndio waondoke lakini si ujinga huu, ni kweli tuliwahifadhi kwa muda hadi Polepole alipoondoka ndiyo tukawaachia,” alisema.

1 COMMENT

  1. Ingekuwa vizuri kutambua kwamba yapo mambo mbadala ambayo ni mazuri na yanayoweza kuwaletea mabadiliko ya maisha haraka kuliko wanavyofanya walioko madarakani. Wafundisheni watu maarifa ya kufanya vitu na kujifungua kiataifa na kimataifa. Kwa mfano mdogo tu ,hivi kwa nini asilimia tisini ya Watanzania wanavaa nguo iliyoshonwa nje ikiwa ni pamoja na nguo za ndani. kushona tu kunatushinda kiasi hicho hata kama tukiagiza vitambaa. Kwenye hizi nchi zetu siasa inayotakiwa ni ya kuwaondolea wati matatizo yao.Fanyeni utafiti na kuja na njia mbadala ya kufanya mambo, na yale yaliyo ndani ya uwezo wenu tekelezeni kwani watu hawaachi kuona jambo linalowafaa.

Leave a Reply to peter msangi Cancel reply

Please enter your comment!
Please enter your name here