23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Chadema yaja na operesheni Ukuta

Viongozi wakuu wa Chadema, wakiwa wameshikana mikono baada ya kutangaza katika mkutanao na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuzindua operesheni mpya ya Ukuta.
Viongozi wakuu wa Chadema, wakiwa wameshikana mikono baada ya kutangaza katika mkutanao na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuzindua operesheni mpya ya Ukuta.

ELIZABETH HOMBO NA JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimezindua operesheni mpya iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta).

Operesheni hiyo inakwenda sambamba na uzinduzi wa mikutano ya hadhara nchi nzima, ambayo itafanyika Septemba Mosi, mwaka huu.

Hayo yametokana na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa siku nne mfululizo jijini Dar es Salaam na kutoa maazimio matatu ambayo yatatekezwa na chama.

Pamoja na mambo mengine, chama hicho kimesema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini, kiliyodai kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Akitangaza uamuzi huo Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema Kamati Kuu imejadili kwa kina hali ya kisiasa nchini na kutoa maazimio hayo.

“Tangu kuanza kwa utawala wa awamu ya tano, kuna matukio mbalimbali ya kubinya demokrasia na kuua dhana ya utawala bora, na yapo makundi ambayo tayari yameshaumizwa, huku Watanzania wengi wakikaa kimya kwa sababu wao si sehemu ya kundi lililominywa.

“Kwa kuwa wewe tayari umeshafikiwa, hauna budi kujenga Ukuta ili kuzuia wengine wasidhurike na utawala huu. Kwa kuwa wewe hujafikiwa na ndiyo maana husemi wenzako wanapofikiwa, basi njoo tujenge Ukuta ili ukifikiwa awepo wa kusema,” alisema Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema suala la kujenga Ukuta halitachagua itikadi za chama wala dini.

Kutokana na hilo, aliwataka viongozi wa dini zote pamoja na Watanzania wapenda amani, kuungana na chama hicho kujenga Ukuta ili kuzuia uchumi kuporomoka.

“Njoo tujenge Ukuta kuzuia udikteta huu, tujenge Ukuta tuilinde Katiba yetu… Ukuta huu ni wa wananchi wote bila kujali dini, kabila, chama cha siasa au rangi,” alisema Mbowe.

Akizungumzia chimbuko la Ukuta, Mbowe alisema umetokana na Rais Magufuli kupiga marufuku safari zote za nje kwa watumishi wa umma, kuamuru Mahakama Kuu iwahukumu wafanyabiashara ambao wana kesi za kodi ili Serikali ishinde.

Alisema nyingine ni Serikali kuingilia Bunge na kupanga wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge, kuzuia matangazo ya moja kwa moja (live) ya Bunge kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) na vituo binafsi pamoja na wabunge wa upinzani kunyanyaswa na hata hotuba zao kufutwa kinyume na kanuni za Bunge.

Aidha Mbowe alisema sababu zilizowasukuma kuanzisha Ukuta ni pamoja na mabalozi na wanadiplomasia kuzuiliwa kukutana na viongozi wa kisiasa bila kibali cha Serikali, watumishi wa umma kufukuzwa ovyo bila utaratibu kwa kisingizio cha kutumbua majipu bila kufuata sheria na kanuni za utumishi wa umma na mawakili kuunganishwa kwenye kesi za wateja wao wanapokwenda kuwatetea.

Mbowe alitaja sababu nyingine kuwa ni Serikali kuendeshwa kwa matamko badala ya Katiba na sheria, Serikali kuwafukuza na kuwadhalilisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na mikutano ya kisiasa kupigwa marufuku.

Walimu kukatwa mishahara iwapo dawati litavunjika kwenye shule yake, kupotezwa kwa wana-CCM ambao watapinga kauli ya mwenyekiti au kuwa na maoni tofauti, unyanyasaji na udhalilishaji wa viongozi wa dini na wananchi wa Zanzibar ni miongoni mwa sababu alizotaja Mbowe.

“Historia inaonyesha duniani kote hakuna ambako utawala uliwahi kuushinda ukuta wa wananchi, na hii ndiyo nguvu ya umma, kila mmoja achukue hatua popote alipo kujenga Ukuta,” alisema.

Kuhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara Septemba Mosi, Mbowe alisema Kamati Kuu imeagiza ngazi zote za chama kuanzia ya msingi, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda, mabaraza na taifa kukaa na kufanya maandalizi ya mikutano hiyo nchi nzima.

Katika azimio jingine, Mbowe alisema Kamati Kuu imewataka wanasheria wote wa chama kuchukua hatua zote za kisheria kwa mambo yote yaliyotokea juu ya uvunjaji wa Katiba.

“Kamati Kuu imeagiza wanasheria wote wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama, Tundu Lissu, kuangalia haki kupitia mahakama na kuhoji tafsiri ya vifungu vya sheria vilivyovunjwa,” alisema Mbowe.

Kutokana na maazimio hayo, Mbowe alisema inawezekana wasiwe salama, lakini wameamua kumweleza Rais Magufuli mambo anayoyafanya kwa sababu washauri wake wameshindwa.

“Wote kama taifa tuna wajibu wa kuchukua hatua, na pale tunaponyamazishwa na kukubali tutakuwa tunaharibu nchi.

“Inawezekana pengine washauri wake hawamwelezi, sisi tunamweleza na inawezekana tusiwe salama na hatimaye nchi hii haitakuwa salama.

“Tangu Uchaguzi Mkuu ulipokwisha hatujawahi kufanya mkutano hata mmoja, lakini rais yeye anaona kwake ni halali. Sisi tukikaa hivi hatutajenga taifa la demokrasia.

“Rais hajanyimwa kufanya kazi zake, yeye si malaika, tutamkosoa tu pale atakapokosea na kumpongeza pale anapofanya vizuri,” alisema Mbowe.

Alipoulizwa itakuwaje mikutano hiyo ikipambana na nguvu ya dola, alisema tangu Chadema ilipoanzishwa mwaka 1992, ilipitia hatua mbalimbali zenye maumivu mengi na haikuwa fadhila ya mtu.

“Wako waliopoteza maisha wakipigania chama hiki, wengine wamekuwa walemavu, wengine wamepata madhila mengi, hivyo ujenzi huu wa demokrasia si kwa faida yetu lakini kwa faida yenu, watoto wenu na watoto wa watoto wenu.

“Tunatambua uwepo wa dola, sasa tukisema tuiogope dola halafu taifa liporomoke? Maswali mliyouliza waandishi wa habari yamejaa hofu… tumejenga taifa lenye woga na hofu, yaani kwa kuwa mtu mmoja kasema basi tutulie tu?” alihoji Mbowe.

Alisema waliamua kukaa kimya tangu Novemba mwaka jana, huku wakiwazuia vijana kutofanya maandamano, lakini bado watawala hawakuliona hilo.

“Sisi tumesaidia kuwepo amani ya nchi hii, maana tangu uchaguzi wa mwaka jana tumekuwa tukiwazuia vijana wetu kutofanya maandamano, tukakaa kimya kwa lengo la kuipa muda Serikali hii, lakini tunaona ubabe tu.

“Hatujawa waoga na hatutakuwa waoga, ila tunafanya kila jambo kwa tahadhari, tukiendelea kukaa kimya tutakuwa hatujautendea haki wajibu wetu kama viongozi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles