24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yafunguliwa kesi kila kona

1

Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani

JESHI la Polisi nchini limewatia mbaroni viongozi na makada 58  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kuzuiwa mikutano ya hadhara.

Kati yao, viongozi 51 ni wa Kanda ya Ziwa Viktoria na  Serengeti  ambao wamekamatwa na kuhojiwa na wengine kufikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali tangu  chama hicho kilipotangaza kuanza maandalizi ya Operesheni Ukuta inayotarajiwa kuanza Septemba mosi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa wa Operesheni Kanda ya Ziwa Victoria wa Chadema, Tungaraza Njugu alisema kanda yake pekee wamekamatwa viongozi 34, akiwamo yeye, Mratibu wa Kanda, Meshark Nicas na Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Geita, Upendo Peneza.

Alisema hali ni mbaya zaidi wilayani Chato  mkoani Geita ambako viongozi wamezuiwa kuendelea na shughuli zote za chama ikiwa ni pamoja na kuingia ofisi za chama kufanya kazi.

Alisema  Katibu wa Chadema, Wilaya ya Chato, Sayi Mboje maarufu ‘Nange’ amekuwa akikakamatwa mara kwa mara.

“Mkoa wa Geita ulianza mapema kamatakamata hii. Katibu wa Wilaya ya Geita yeye amezuiliwa kabisa kuendelea na kazi ofisini sawa na yule wa Chato. Anatakiwa kila siku kufika polisi tangu Agosti 23, mwaka huu na wala hawajampeleka mahakamani,” alisema.

Alitaja idadi ya viongozi waliokamatwa na maeneo yao kuwa ni  wilaya za Karagwe, Kyerwa na Bukombe ambako viongozi wanne kila wilaya.

Alisema katika Wilaya ya Nyang’wale, viongozi na wajumbe wa Kamati ya Utendaji 14 walikamatwa.

Kwa   Kanda ya Serengeti, viongozi waliokamatwa ni 17 akiwamo Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na wenzake 19 ambao walifikishwa  katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi na kusomewa mashtaka ya uchochezi na kunyimwa dhamana.

“Kanda ya Serengeti kuna kesi mbili, ipo ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na wenzake 19 na kule Maswa kuna kesi ya Ofisa wa Kanda, Frank Buberwa  na wenzake 16 walikamatwa wakiwa kwenye vikao vya ndani kwa mujibu wa Katiba,”alisema.

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema kamatakamata hiyo imeendelea Kanda ya Kati mikoa ya Dodoma, Morogoro  na Singida ambako viongozi saba wanashtakiwa kwa uchochezi.

“Mpaka sasa Mwenyekiti  wa Bawacha Jimbo la Ulanga, Ignasia Mzenga yuko ndani na utakumbuka hata kada wetu Arcardo Ntagazwa alikamatwa na kuachiwa akiwa na viongozi wenzake,”alisema Makene.

Alisema Kanda ya Magharibi mikoa ya  Kigoma,Tabora na Katavi viongozi wengi wamefunguliwa kesi  za uchochezi.

“Pale Kigoma viongozi watano, akiwamo Mwenyekiti wa Wilaya ya Konkoo na wenzake wamekamatwa, lakini Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora na wenzake wanne wamefunguliwa kesi,”alisema.

Alisema katibu wa chama hicho Mkoa wa Katavi na wenzake wanne wamefunguliwa kesi.

Kwa Kanda ya Kaskazini, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anaendelea kushikiliwa na polisi kwa siku ya tatu, alisema.

Alisema Meya wa Jiji la Arusha, Lazaro Bukhay alikamatwa na wenzake wikiwa Wilaya ya Siha. Pia Katibu wa Chadema  Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alikamatwa na kuhojiwa na jeshi hilo.

Polisi

Wiki iliyopita jeshi la polisi lilipiga marufuku vikao vyote vya ndani vya vyama vya siasa kutokana na matukio ya uhalifu yanayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishina Operesheni na Mafunzo, Nsato Marijan wakati akizungumzia tukio la mauaji ya askari wanne katika eneo la Mbande, Mbagala.

“Mikutano ya ndani inatumika kuhamasisha watu kuvunja sheria za nchi na kupambana na askari kuanzia sasa jeshi la polisi linapiga marufuku mikutano ya ndani pia,” alisema.

Alisema viongozi wa siasa wakiwa kwenye majukwaa wamekuwa wakiwahamasisha  wafuasi wao kuwashambulia askari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles