31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yaendelea na msimamo wake kwa kina Mdee…

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati kimesema kitaendelea kusimamia msimamo wake wa kutowatambua Wabunge 19 wa Chama hicho, ambapo kimedai kitafanya maandamano ya amani kuanzia wilayani Kongwa mkoni Dodoma kushinikiza Spika wa Bunge, Job Ndugai awaondoe wabunge hao bungeni.

Pia, kimesema huu ni wakati wa kukijenga Chama chao na sio wa kujiuliza ni kwanini aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu ameondoka ndani ya chama hicho.

Itakumbukwa, Aprili 30, mwaka huu Nyalandu alijivua uanachama wa Chadema pamoja na nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kati ambayo inajumuisha Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM) katika mkutano mkuu wa kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa chama hicho uliofanyika jijini hapa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatatu Mei 3, 2021, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Aisha Luja amesema hivi karibuni watafanya maandamano ya amani kuanzia wilayani Kongwa lengo likiwa ni kushinikiza Spika Ndugai awaondoe wabunge hao bungeni.

“Ili tupate haki yetu tutafanya maandamano ya amani kuanzia Kongwa.Ni vema Spika Ndugai kutumia vifungu vya sheria na kanuni alivyotumia kumuengua, Sofia Simba aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum mara baada ya kufukuzwa uanachama na chama chake pamoja na wabunge nane wa CUF azitumie sheria hizo katika kutenda haki,”amesema.

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti huyo amesema licha ya Nyalandu kuondoka chama chao kipo imara na wanasonga mbele na huu ni wakati wa kukijenga chama hicho sio vingine.

“Ni vema watanzania watambue kuwa msingi mkuu wa uimara wa Chadema ni tikadi na falsafa yake ya nguvu ya umma sisi kama Chadema tupo imara na tunasonga mbele kwani wapo wasafiri watakaoshuka katikati ya safari hata kabla ya kufika mwisho.

“Wenye moyo wa uthubutu na ujasiri pasi na kutanguliza maslahi binafsi ndio watakaoweza kufika mwisho wa safari hii ya machozi, jasho na damu. Hivyo huu ni wakati wa kukijenga chama chetu kwa wivu mkubwa ili kuweza kutimiza lengo letu la kuwakomboa watanzania,”amesema.

Alipoulizwa pengo la Nyalandu ndani ya Chadema, Aisha amesema wamepokea kama taarifa ya kawaida kwani wamewahi kupita Mawaziri Wakuu wastaafu na kwa sasa hawapo ndani ya chama hicho.

“Tumepokea kawaida sana Nyalandu sio mtu wa kwanza kuondoka kwetu hapa kulikuwa na Mawaziri pamoja na Mawaziri Wakuu wastaafu sasa Chadema inasonga mbele,” amesema.

Kuhusiana na kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema Kanda,amesema kwa mujibu wa kanuni na taratibu kwa sasa nafasi hiyo itashikwa na Makamu Mwenyekiti huku vikao vingine vikiendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles