25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Chadema wataka Serikali itoe vitakasa mikono kwa wananchi

Faraja Masinde -Dar Es Salaam

SIKU moja baada ya mgonjwa wa kwanza wa maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19) kufariki dunia nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani kimeitaka Serikali kuwekeza zaidi kwenye huduma za afya kwa wakati huu ikiwa ni pamoja kurahisisha upatikanaji wa vitakasa mikono (Sanitizer).

Itakumbukwa mapema jana asubuhi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alitangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona hapa nchini ambaye ni mwanaume (47) kilichotokea katika kituo kilichoko Mloganzila huku hadi sasa kukiwa na maambukizi ya wagonjwa 19 nchini.

Kauli hiyo ya Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini, ilitolewa jana na Ofisa Habari wa Kanda hiyo, Grevas Lyenda wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Lyenda alisema Serikali inapaswa kutilia mkazo kuhusu ugonjwa huo.

“Kama taifa lazima tuwe ‘siriasi’ na huu ugonjwa kwani watu wanapoteza maisha kila siku na tumeshuhudia namna ambavyo majirani zetu, mfano Uganda na Kenya wanavyochukua hatua thabithi za kuhakikisha kuwa watu hawatoki.

“Lakini hapa kwetu bado ni changamoto, kwani watu wanajaa kila mahala, ikiwamo kwenye vyombo vya usafiri na sokoni.

“Tunaiomba Serikali iipe uzito kwelikweli suala la corona kwani tunaona namna ambavyo idadi ya wagonjwa wanavyozidi kuongezeka na hata leo (jana) kimeripotiwa kifo.

“Tungependa mgonjwa huyu awe wa mwisho, tunaona Kenya wenzetu wanagawa vitakatisha mikono bure na hata upatikanaji wake ni rahisi, lakini kwetu hapa huduma hii inazidi kuwa ghali kila kukicha,” alisema Lyenda.

Akitolea mfano, alisema baadhi ya maduka yanauza chupa ya kitakatisha mikono ya gramu 250 kwa Sh 10,000 huku ile yenye ujazo wa gramu 100 ikiuzwa Sh 7,500 jambo alilosema ni ngumu kwa kila mtu kuweza kumudu bidhaa hiyo ikilinganishwa na hali halisi ya ugumu wa maisha.

“Wito wetu ni kwamba hakuna kipindi Serikali inatakiwa kuwekeza kwenye masuala ya afya kama kipindi hiki. Kenya wameweza, wanagawa bure, sisi tunashindwa nini? Walau hata kuondoa tozo kwenye bidhaa zinazotumika kutengeneza vitakatisha mikono.

“Hivyo ni bora Serikali ikaona umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na kusaidia wazalishaji kupata vifungashio vya bei nafuu au hata bure ili kitakasa kinachouzwa 10,000/- kiuzwe hata 1,000/- na kile cha 7,000/- kiuzwe 500/- au hata kugawiwa bure kwa wananchi ili iweze kusaidia kupunguza maambukizi, hapo tutaonekana tuko ‘siriasi’,” alisema Lyenda.

Aidha, katika hatua nyingine chama hicho kilihoji namna viliko vifaa vya kusaidia kupambana na virusi vya corona vilivyotolewa na bilionea wa China, Jack Ma.

“Ni bora Serikali ikatwambia kuwa msaada huu wa vifaa tumevipeleka sehemu flani na upatikanaji wake uko hivi, ili kila Mtanzania aweze kujua utaratibu wa namna ya kuvipata kuliko kukaa kimya.

“Kwani pia tumepata taarifa kwamba vitakatisha mikono vinavyotumika kwenye magari yaendayo haraka jijini Dar es Salaam ni jiki na siyo vitakasa mikono vinavyohitajika,” alisema Lyenda.

Aidha, chama hicho Kanda ya Pwani kimewataka wanachama wake kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kutumia muda huo kupumzika na familia zao.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi jana idadi ya walioambukizwa walikuwa 697,243 huku idadi ya vifo ikifikia 33,257.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles