24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema wapuuza kauli za Msajili

Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

NA GRACE SHITUNDU

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amepuuza kauli na maagizo yaliyotolewa juzi na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza.

Nyahoza alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari likiwemo gazeti hili kuwa Mbowe hawezi kuongoza tena chama hicho kwa muhula mwingine hata kama atashinda kwenye uchaguzi wa chama hicho.

Alisema hatua hiyo inatokana na chama hicho kukiuka katiba yake kwa kubadilisha kipengele cha ukomo wa uongozi kutoka ukomo wa mihula miwili hadi kutokuwa na ukomo wa uongozi.

Nyahoza alisema kuwa mabadiliko hayo ya katiba hayakufuata taratibu stahiki, ikiwa ni pamoja na kutopata baraka za Mkutano Mkuu.

Mbali na suala hilo, Nyahoza pia aliutaka uongozi wa chama hicho kuhakikisha Januari mwakani kinaitisha Mkutano Mkuu wa uchaguzi ili kuwapata viongozi wapya.

Akijibu kauli hizo jana, Mbowe alisema tamko lililotolewa na Msajili ni kituko na kichekesho kwa kuwa ukomo wa uongozi wa chama hicho ni uamuzi na utashi wa wanachama wenyewe.

Akizungumza kwa simu ya mkononi na MTANZANIA Jumatano jana, Mbowe alisema chama cha siasa kinaongozwa kwa demokrasia na kwamba ni utashi wa wanachama wenyewe kuweka ukomo wa uongozi.

“Msajili kuingilia mambo ya ndani yanayohusu ukomo wa uongozi wa chama mimi naita ni kichekesho na ni kituko, huo ni uamuzi wa ndani ya chama na siyo uamuzi wa Msajili.

“Chama cha siasa sio sawa na Serikali, sisi tunaongozwa na demokrasia, suala la katiba na kubadili baadhi ya vipengele ni la wanachama wenyewe ambao ndio wanaamua katiba yao iweje, mabadiliko au uamuzi katika chama unafanywa na wanachama katika vikao, inawezekana wachache wakayakataa mabadiliko hayo lakini wengi wakayakubali, hivyo yanatakiwa yaheshimiwe,” alisema Mbowe.

Aliongeza kuwa kila chama kina haki na mamlaka ya kuamua viongozi wao wakae muda gani madarakani, ambapo wanaweza kuamua kukaa miaka 10 au zaidi.

Alisema suala la yeye kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine ni suala binafsi ambalo linatokana na utashi wake ikiwa ataamua kugombea au la!

Aidha aliweka wazi kuwa sifa za kuwania nafasi hiyo kama katiba yao inavyotaka anazo, ambapo pia anaamini wanachama wanautambua mchango wake ndani ya chama katika kipindi chote alichokaa madarakani.

MNYIKA AMUONYA

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, alimuonya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuacha kutangaza mgogoro na Chadema.

Mnyika alisema anaamini Msajili anaingizwa kwenye mtego wa kutumika jambo ambalo linaweza kumuondolea sifa.

Akikosoa kauli ya Nyahoza, Mnyika alisema Msajili hana uwezo wa kumzuia Mbowe ama mwanachama yeyote wa chama hicho kuwania uongozi na kwamba chama chao hakiongozwi na matamko ya watu.

Alisema chama chao hakijakiuka kipengele chochote cha katiba wanayoitumia sasa, ambayo waliiboresha zaidi kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Agosti 13, 2006.

Alisema Mkutano Mkuu wa mwaka 2006 ulitumika kuboresha katiba, bendera, kadi pamoja na kuweka mikakati na mipango ya chama na kwamba mkutano huo uliidhinisha mabadiliko yote.

Mnyika aliongeza kuwa katiba yao ya mwaka 2006 kifungu cha 6.2 (c) kinatoa mamlaka kwa kiongozi kuwania uongozi na kuchaguliwa endapo ametimiza masharti yote.

“Ofisi ya Msajili haina uwezo wa kumzuia Mbowe au mwanachama yeyote wa Chadema kuwania uongozi kama ametimiza masharti, chama chetu kinaongozwa na taratibu kwa kufuata katiba yake, tunamuomba msajili kutoingia kwenye mtego wa kutumika.

“Akiendelea kufanya haya aliyoanza kuyafanya atakuwa ametangaza mgogoro na sisi na hatutamtambua kama ambavyo tulimfanyia mtangulizi wake, John Tendwa.

“Mwaka 2006 tuliandika katiba mpya, hata hivyo baadhi ya mambo ya katiba ya zamani tuliyapa nafasi na kipengele cha ukomo wa uongozi kiliridhiwa na Mkutano Mkuu baada ya kusambazwa kwa waraka wa mabadiliko ya katiba nchi nzima na mapendekezo yalifikishwa kwenye ngazi zote husika kabla ya kufikishwa kwenye Mkutano Mkuu ambao nao uliridhia,” alisema.

Aidha alisema kinachoendelea sasa hivi ni mikakati ya baadhi ya watu ndani na nje ya chama chao kuhakikisha wanawapindua viongozi wa juu wa chama hicho.

“Upo msemo unaosema, mpige mchungaji kondoo watatawanyika, tumeshazibaini mbinu zao, wameshindwa kwenye waraka wa mabadiliko, wameshindwa kwenye kuwachafua viongozi wetu sasa wanaitumia ofisi ya Msajili wa Vyama, nawahakikishia wahusika wa uovu huu hawatafanikiwa,” alisisitiza Mnyika.

Mnyika alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kujitokeza hadharani na kuzitolea ufafanuzi kauli zilizotolewa na msaidizi wake.

Alihitimisha kwa kusema kuwa ofisi ya Msajili isiwafundishe kazi kwani suala la kufanya ama kutokufanya uchaguzi ni la chama na kwamba mipango yao ni kufanya uchaguzi mwaka huu na si mwakani kama Nyahoza alivyotaka.

“Mwezi huu tutaanza uchaguzi wa viongozi wa majimbo na wilaya, mwezi Agosti tutafanya chaguzi za mikoa na mwezi Septemba tutafanya uchaguzi wa ngazi ya taifa, asitufundishe kazi na aepuke kutangaza mgogoro na sisi, kama hajui akamuulize Tendwa,” alihitimisha Mnyika.

Nyahoza katika mazungumzo yake na waandishi wa habari juzi alisema vyama vyote vya siasa nchini vinaongozwa na kufuata katiba walizojiwekea wenyewe.

Alisema ofisi ya msajili inafanya kazi kisheria ikiwa ni pamoja na kusimamia katiba za vyama hivyo na kutoa mwongozo na kwamba kama kuna baadhi ya vyama vinakwenda kinyume na katiba yake, ofisi hiyo inalazimika kuingilia kati.

Gazeti hili lilimtafuta Jaji Mutungi ili kuzungumzia suala hilo bila mafanikio kutokana na simu yake kutokuwa hewani kwa muda mrefu.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles