29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema waonyesha video ya ujangili

Na Mwandishi Wetu

Mchungaji Peter Msigwa
Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa

, amewaonyesha waandishi wa habari video inayoonyesha jinsi wanyamapori wanavyouawa kinyama.

Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alionyesha video hiyo jana alipokuwa akizungumza na wanahabari hao jijini Dar es Salaam.

Video hiyo ambayo Mchungaji Msigwa alisema ni ya saa mbili, alianza kuionyesha kuanzia saa 4:29 hadi saa 4:43 asubuhi.

Katika video hiyo iliyorekodiwa na Kampuni ya Uwindaji ya Green Mile Safaris Limited aliyosema inamilikiwa na mmoja wa wanafamilia wa Mfalme wa Abudhabi, wawindaji wanaonekana wakiwaua wanyama kwa kuwapiga risasi baada ya kuwafukuza kwa kutumia magari.

Miongoni mwa wanyama wanaoonekana wakiuawa katika video hiyo ni pamoja na nyumbu, nyati na tandawala weupe na weusi.

Wakati wakiwaua wanyama hao kwa kutumia bunduki na silaha nyingine zinazojiendesha zenyewe, wawindaji hao ambao ni Waarabu walionekana wakizungumza Kiarabu huku wakishangilia pindi wanapoua wanyama na wakati mwingine wakionekana kupongezana baada ya kuwaua.

Pamoja na kuwaua wanyama hao na kuwapakia katika magari yao, pia walionekana wakikamata wanyama wadogo ambao haikujulikana walikowapeleka.

Miongoni mwa wanyama wadogo waliokamatwa ni mtoto wa ngiri na wa pundamilia ambaye alikamatwa baada ya kuzingirwa na wawindaji hao.

Pamoja na kuua wanyama, pia wawindaji hao walionekana wakiua ndege mbalimbali kwa risasi wakiwamo kanga.

Baada ya uwindaji huo kufanyika, video hiyo ilionyesha wawindaji wakichuna ngozi za wanyama waliowaua huku wakining’iniza nyama za wanyama hao.

Akizungumzia video hiyo, Mchungaji Msigwa alisema video hiyo ilirekodiwa mwaka 2012 katika Hifadhi ya Taifa ya Selous na kwamba ilikuwa ikitumiwa na Kampuni ya Green Miles Safaris Limited kutangaza biashara ya uwindaji wa wanyamapori duniani.

“Hii video niliiwasilisha katika Bunge la Bajeti lililopita nikitaka Serikali iiangalie na kueleza namna ya kuchukua hatua za kukabiliana na ujangili.

“Kwa bahati mbaya hakuna kilichofanyika, kwa hiyo nimeamua kuwaambia waandishi wa habari jinsi wanyama wetu wanavyowindwa kinyemela wakati Serikali ikiendelea kukaa kimya.

“Katika video hii wanyama wa kike wanauawa kinyama, watoto wa wanyama wanakamatwa na mkiendelea kuiangalia mtaona kuna magari ya watu binafsi yako mbugani na yanawinda wanyama.

“Hii kampuni inaonekana inamilikiwa na Mtanzania aitwaye Salum Awadh, lakini tulipoifuatilia kimataifa tukakuta inamilikiwa na Abdallah Ahmed wa Abudhabi,” alisema Mchungaji Msigwa.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, Kampuni ya Miles Safaris Limited, imekuwa ikiwakimbiza na kuwakamata watoto wa wanyamapori kinyume cha kifungu cha 19 (1) cha sheria za wanyama pori.

“Pia kampuni hiyo ilishazuiwa na mahakama kuwinda wanyama hapa nchini baada ya kuonekana ikikiuka sheria, lakini kwa kupitia mlango wa nyuma ilipewa kibali na Mkurugenzi wa Wanyamapori.

“Kampuni hii imekiuka kifungu 24 (2) cha sheria namba tano ya uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 2009 inayozuia kuwakimbiza, kuwasumbua na kuwajeruhi wanyama.

“Kampuni hii pia imekuwa ikiwaruhusu watoto chini ya miaka 18 kuwinda ndege ambao hawajaidhinishwa kuwindwa na watalii na hili linaonekana katika video ambapo kuna mtoto anaonekana akiwinda.

“Pia kampuni hii imekiuka kifungu namba tano (1) ambacho kinazuia watu kukamata watoto wa wanyama bila kibali cha kufanya hivyo,” alisema.

Kutokana na hali hiyo aliitaka Serikali ichunguze kampuni zote za uwindaji, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, awawajibishe watendaji wazembe wizarani kwake na kampuni zote zinazokiuka sheria za uwindaji ziadhibiwe.

“Naitaka pia Serikali iisimamishe Kampuni ya Green Miles Safaris Limited kuendelea na shughuli za uwindaji nchini na pia Serikali iharakishe kutoa ripoti ya operesheni tokomeza,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles