26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema wamshangaa Sumaye

Andrew Msechu –Dar es salaam

BAADA ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kutangaza kujivua uanachama wa Chadema kwa kile alichodai ni figisu alizofanyiwa kwenye uchaguzi wa kumtafuta Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, chama hicho kimeeleza kushangazwa na sababu alizotoa kiongozi huyo.

Sumaye aliyewahi kuwa Waziri Mkuu  mwaka 1995 hadi 2005, katika uchaguzi huo wa Kanda ya Pwani alipigiwa kura 48 za hapana kati ya 76.

Akizungumzia uamuzi huo wa Sumaye, Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema hajaona mantiki katika sababu zote zilizotolewa na kiongozi huyo.

Mrema alisema inaonekana wazi Sumaye alikuwa akitafuta mahala pa kutokea baada ya kubanwa na familia na marafiki zake, ambao huenda waliona njia pekee ya kurejeshewa mashamba na baadhi ya mali zake anazodai zilichukuliwa ni kujitoa katika chama hicho.

Alisema pamoja na uamuzi aliouchukua ili kufurahisha familia na marafiki zake, ajue kwamba wanaobaki upinzani wanabaki na maumivu makali, lakini wataendelea kupigania lile wanaloliamini.

KUHUSU DEMOKRASIA

Mrema alisema anashangazwa na kauli ya Sumaye kuwa hakuna demokrasia ndani ya Chadema, chama ambacho wanachama wake wanaamini kuna demokrasia pana inayotekelezwa kwa vitendo.

Alisema Sumaye amekuwa mwanachama wa CCM kwa miaka yake yote, hadi alipotoka na kuhamia Chadema miaka minne iliyopita, lakini haamini kwamba Chadema kuna demokrasia ya kutosha tofauti na huko katika chama chake cha awali.

“Huyu amekuwa CCM miaka yake karibu yote, atuambie kama anaamini kuwa CCM ndiko kuna demokrasia. Huko ambako hatujawahi hata kusikia kuwa kuna mtu anaruhusiwa kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti wa chama.

“Huku yeye mwenyewe ameshuhudia demokrasia pana na ameweza hata kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti, ambayo tayari alishairejesha na ameamua mwenyewe kuiacha wakati ikiwa bado ndo inakaribia kwenye hatua ya mwisho ya mchakato ambayo ni kwenda kwenye sanduku la kura.

“Sasa labda angetuambia anataka demokrasia ya aina gani, anataka kama ya kule CCM au anataka ipi, tunamweleza tu kuwa akumbuke alipoingia huku alikutana na demokrasia yetu ambayo ni pana,” alisema Mrema.

TATHMINI YA TABIA YA SUMAYE

Mrema alisema katika kutathmini tabia ya Sumaye, siku zote amekuwa mtu wa kutafuta mtu wa kumlaumu, asiyependa kujitathmini na kukubali ukweli katika ushindani wa kisiasa.

Alisema anakumbuka alipokuwa akiwania kuteuliwa na CCM kuwania urais mwaka 2005, aliposhindwa alitoka hadharani na kuanza kuwalaumu Rais mstaafu Jakaya Kikwete na timu yake, akidai walimchafua katika vyombo vya habari.

Mrema alisema kama haitoshi, alipokwenda kuwania ubunge kisha kushindwa na Mary Nagu, aliibuka na kuelekeza lawama kwa Edward Lowassa na Nagu akidai kuwa wamemfanyia hujuma ili asipate nafasi hiyo.

“Lakini zaidi kama utakumbuka, mwaka 2015 alijitokeza kuomba ridhaa ya CCM kuwania urais kupitia chama hicho. Aliposhindwa alijitokeza na kumlaumu Rais mstaafu Mkapa (Benjamin) na Kikwete akidai kuwa wamekuja na jina la mgombea wao mfukoni. Kwa hiyo hatushangai kwa haya tunayoyasikia leo (jana),” alisema Mrema.

Alisema kuhusu utaratibu uliotumika kupiga kura ambazo Sumaye analalamikia kuwa zilinuia kumwondoa kwenye nafasi ya uenyekiti wa kanda, alidai si kweli kwa kuwa siku zote Chadema imekuwa na utaratibu huo.

Mrema alisema utaratibu huo ulitumika pia Sumaye alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani mwaka juzi, ambao yeye alipita, lakini kura zilikataa kumpitisha aliyekuwa akiwania uwakilishi wa vijana, John Kirenga.

Alisema Sumaye si wa kwanza kupitia utaratibu huo kwa kuwa hata Mchungaji Peter Msigwa aliwahi kunusurika kuukosa uenyekiti wa Kanda ya Nyasa ambapo japokuwa alikuwa mgombea pekee, kura 42 zilimkataa na alibahatika kupita kwa ushindi finyu wa kura 58.

Mrema alisema anakumbuka wakati Msigwa akikabiliana na suala hilo, Sumaye alikuwa akisimamia uchaguzi kwa mtindo huo huko Mkuranga na sasa anashangaa kuona anatoa malalamiko baada ya yeye kushindwa, kupitia utaratibu aliokuwa akiujua na aliokuwa akiusimamia.

Alisisitiza kuwa huo ni utaratibu wa kidemokrasia unaotumiwa na chama hicho na hakuna anayeweza.

Akizungumzia kauli za Sumaye, Mrema alisema; “hatuna taarifa za makundi kwenye chama chetu labda kama yeye alikuwa na kundi.

“Sumaye alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama, alikuwa na nafasi ya kutoa taarifa hiyo na kama kweli ipo ingefanyiwa kazi.”

Hata hivyo Mrema alisema Sumaye kuondoka Chadema na kama mwanachama yoyote ameacha pengo kwenye chama hicho, na kwamba watatafuta namna ya kuziba pengo hilo.

“Sababu kubwa aliyoitoa kuhusu kuondoka kwake Chadema ni shinikizo kutoka kwa familia yake, kwa hiyo sasa anakwenda kupumzika na wajukuu. Sisi tunamtakia kila la heri katika maisha yake na mapumziko mema,” alisema Mrema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles