33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CHADEMA WAMLIPA BARUA KAIMU JAJI MKUU

Na ELIZABETH HOMBO

-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemuandikia barua Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kikimtaka aingilie kati mwenendo wa baadhi ya mahakimu kuwanyima dhamana viongozi na wanachama wa chama hicho waliofunguliwa kesi za uchochezi.

Pia kimemuomba Kaimu Jaji Mkuu huyo kuwa Mahakama iwe huru kama inavyoelekezwa kwenye Katiba na kuhakikisha inalinda uhuru wake kwa kuamua masuala ya dhamana bila shinikizo au hofu ya viongozi wa  siasa.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa  Abdallah Safari alisema katika barua hiyo wameainisha kesi tano ambazo mahakimu waliwanyima dhamana wanachama wao bila sababu za msingi.

“Kamati Kuu tumeamua kumwandikia barua Kaimu Jaji Mkuu na bahati nzuri ni mwanafunzi wangu, kwa hiyo tumeandika kuhusu baadhi ya mahakimu kutokutoa dhamana.  Kuna barua ambayo nimeiandika kama Makamu Mwenyekiti tukilalamika vitendo hivyo kwamba visiendelee.

“Tunaomba Mahakama zetu zilinde uhuru wake kwa kuamua masuala ya dhamana bila shiniko au hofu yoyote kama yalivyofanya Mahakama ya Zimbabwe na Afrika Kusini.

“Mahakama ya Zimbabwe bila kumwogopa Rais Robert Mugabe iliamua kuwa wapinzani wana haki ya kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, na Mahakama ya Afrika Kusini bila kumhofu Rais Jacob Zuma iliamuru rais huyo achunguzwe,”alisema.

Akinukuu sehemu ya barua hiyo mbele ya waandishi wa habari, Profesa Safari alisema: “Chadema kinaleta malalamiko yake dhidhi ya baadhi ya mahakimu ambao wanalenga kuwakomoa viongozi na wanachama wa chama chetu ambao wamefunguliwa kesi za uchochezi na mikusanyiko haramu”.

Katika barua hiyo chama hicho kilieleza kuwa kesi za uchochezi zimekuwa nyingi kutokana na amri ya Rais Dk. John Magufuli ya kukataza vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara.

“Na sasa hata baadhi ya mikutano ya ndani inakatazwa na viongozi wa siasa kama wakuu wa wilaya na mikoa pamoja na Jeshi la Polisi. Katika kadhia hii baadhi ya mahakimu wanawanyima dhamana au wanawawekea masharti magumu ya dhamana,”alisema Profesa Safari.

Akitaja kesi tano ambazo zimeorodhesha kwenye barua hiyo, Profesa Safari alisema ni pamoja na kesi ya Jinai Na. 173 ya mwaka 2017, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji na wenzake nane walishtakiwa.

Alisema nyingine ni kesi ya Jinai Na 96 ya mwaka 2017, Mahakama ya Wilaya Mbozi, Jamhuri v. Mussa Mwenengo na wenzake Harun Mwangaya walifikishwa mahakamani Julai 19 mwaka huu wakishtakiwa kufanya vurugu.

Alisema katika kesi hiyo wanachama hao walinyimwa dhamana hadi Julai 24 mwaka huu.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vicent Mashinji  alisema: “Tunapitia hatua ambazo si nzuri sana na sisi watu wa imani tunaambiwa mtu akikukosea unajaribu kutafuta ufumbuzi.

“Tumekuwa tukizungunza ila ndugu zetu hawatusikii. Kuna matumizi mabaya   ya dola na dola ikitumika vibaya   huko tuendako si kuzuri”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles