24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema wameshindwa na falsafa ya Ustahamilivu wa Kisiasa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MIONGONI mwa mataifa ya Kiafrika yaliyojenga misingi imara ya ustahamilivu ni Tanzania. Katika nyanja zote za kisiasa, kijamii na kiuchumi kuna funzo kubwa limeachwa na waasisi wa taifa hili.

Ndiyo maana panapotokea mtu au kikundi cha watu kikikosa ustahamilivu kwenye maeneo fulani si ajabu kuulizana mtu huyo anatokea wapi, hata kufikia kutilia shaka utaifa wake.

Haya ni mambo tuliyoshuhudia wazee wetu wakiyaishi. Si kitu cha paukwa pakawa au hadithi za kufikirika, ni kitu halisi.

Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza Tanzania, Julius Nyerere katika mambo aliyoyapigia kelele kwenye miaka ya awali ya uhuru wa Tanganyika ni umoja na mshikamano.

Hizi ni tunu ambazo Watanzania hatuwezi kujiweka mbali nazo kwa namna yoyote ile.

Hakuna sababu ya kutoa maelezo marefu juu ya umuhimu wa umoja, ushirikiano na kustahamiliana ambavyo Mwalimu Nyerere alivipigania sana.

Kwa mfano akiwa jijini Rio De Janeiro nchini Brazil mnamo Juni, 1991 Mwalimu Nyerere alipata kusema: “Demokrasi sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuiagiza. Demokrasi inapaswa kuendelezwa kulingana na nchi yenyewe.”

Vilevile akiwa jijini Accra, Ghana mnamo Machi 6, 1997 alipata kusema: “Umoja hautatufanya kuwa tajiri, lakini unaweza kuwezesha kuiepusha Afrika na watu wa Afrika kutoheshimiwa na kudhalilishwa.”

Tubaki hapo kwenye maneno ya Mwalimu Julius Nyerere wakati tukitafakari kile ambacho Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kukifanya kwa Tanzania kupitia falsafa maarufu ya 4R, ambayo inagusia mambo mtambuka juu ya maendeleo ya taifa lolote la Tanzania.

Maridhiano (Reconciliation), Mabadiliko (Reforms), Ustahamilivu (Resiliance) na Kujenga upya (Rebuilding).

Machi 8, 2023 ni tarehe ambayo haiwezi kutoka kwenye vichwa vya watu hasa wanaofuatilia siasa za Afrika, si Tanzania pekee. Hii ni baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuonekana katika mkutano wa chama kikuu cha upinzani nchini – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ilikuwa ni mkoani Kilimanjaro katika mkutano ulioandaliwa na Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo waliomba Rais Samia awe mgeni rasmi, bila hiyana aliridhia.

Kwa mshangao mkubwa wachambuzi na wafuatiliaji wa siasa za Tanzania na ukanda huu wa Afrika Mashariki waliona hicho hakikuwa kitendo cha kawaida, lakini Rais Samia aliridhia na hakutaka kuwakilishwa alikwenda mwenyewe na kuhutubia.

Akizungumza katika mkutano huo Rais Samia aliwapa tumaini wanachama wa Chadema juu ya ujio wa Katiba Mpya lakini alisema kweli kuwa hilo si jambo mara moja, linahitaji mchakato wa muda mrefu.

Mengi aliyozungumza yalionekana kuwafurahisha wanawake hao wa Chadema (BAWACHA), kiasi cha kuamua kumpa tuzo ya kutambua mchango wake kwa kuboresha demokrasia nchini.

Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu alizungumza kauli yake maarufu katika mkutano huo: “Nimesimama hapa bila kuwa na hofu ya kukamatwa na Polisi wala kurushiwa mabomu, Mama pokea Baraka nyingi za Mungu. Mwenendo wako mwema, umeboresha demokrasia na haki nchini, maisha yetu ya awali katika serikali ya mtangulizi wako yalijaa hofu, kuwasiliana ilikuwa shida, kutengamana, kutekwa, kunyanyaswa, kuteswa na vilio.”

Hata hivyo, siku za hivi karibuni baada ya tukio lililotokea Mbeya baada ya mvutano wa Jeshi la Polisi na wafuasi wa Chadema, viongozi na wanachama wa chama hicho wamekuwa wakitangaza sifa mbaya za Rais Samia, bila kutoa maelezo ya kutosha. Haijulikani ndani ya mwaka mmoja ubaya huo ameutoa wapi.

Siasa ni ustahamilivu, kustahamiliana ndio sifa ya mwanasiasa yeyote mahiri. Hakuna mwanasiasa anayeendesha shughuli zake bila misukosuko wala kuvutana.

Katika falsafa ya Rais Samia (4R), ipo R moja inazungumzia Ustahamilivu (Resiliance).

Kwa dhati aliamua kuiweka R hii kwa sababu alijua mwanadamu ni mbinafsi, siku zote anapenda kuvutia kwake. Ndiyo sababu ya vita na vurugu zote duniani.

Ubinafsi unamfanya mwanasiasa siku zote aone yeye yuko sahihi na si vinginevyo. Chochote unachofanya lazima uangalie mustakabali mpana wa taifa.

Makosa yanafanywa na wanasiasa kwa kuamini kuwa wanafanya shughuli za kisiasa ili kujinufaisha kiuchumi, kujijenga kitaasisi lakini pia kuangalia namna gani wataendelea kupata faida za kichama kwa muda wote.

Wakati, sababu kubwa ya kuanzishwa vyama vya siasa ni kujua mustakabali wa nchi na wananchi wake. Hiki ndicho kitu cha kwanza kwa mwanasiasa wa kweli.

Zipo taarifa za kweli kutoka vyanzo vyetu kuwa BAWACHA wanajipanga kufanya maandamano makubwa nchini kushinikiza serikali kufuata kile wanachotaka, bila kuangalia mustakabali wa nchi na wale wanaowangoza.

Katika maandamano hayo ambayo inaaminika yatafanyika hivi karibuni, wanapanga kutangaza hadharani kumpokonya tuzo Rais Samia ambayo walimkabidhi katika mkutano wao wa Machi 8, 2023 mkoani Kilimanjaro.

Lengo ni kuionyesha dunia kuwa Rais Samia hakustahiki tuzo hiyo. Hii ni dhahiri kwanza; Chadema kupitia Bawacha hawajui thamani ya heshimwa waliyopewa na Rais Dk. Samia kuhudhuria kikao kile.

Pengine zaidi hawajui pia kuwa ndani ya chama chake (CCM), Rais Samia alitumia ushawishi wake kuwaelewesha wanachama wa chama hicho kikongwe barani Afrika (CCM), kuwa alichkusudia kukifanya kuhudhuria mkutano wa Bawacha si kitu kibaya katika siasa.

Kwa sababu siasa si uadui. Siasa si kuchukiana wala kupeana majina mabaya. Kukubali mwaliko ni ishara ya ukomavu na ustahamilivu wa kiwango cha kipekee. Ambacho kinataka kupongezwa badala ya kubezwa.

Hata hivyo, wanachodhamiria kukifanya Bawacha ni kujivua nguo. Baada ya Rais Samia kuamua kuwavika nguo wao wanazivua na kujiweka wazi kuonyesha namna gani si waungwana.

Ishara ya ubinafsi inawagubika Chadema katika hili. Wanaonyesha kwa kiwango gani hawana ngozi ngumu na pengine siasa si uwanja wao.

Kwa sababu kitendo cha kutaka wapate wao kila siku ni kuonyesha dhahiri hawana muda wa kusikiliza ya wengine, wanataka kuiaminisha jamii kuwa wao ndio watoto wa pekee wa Tanzania na wanachotaka kukifanya lazima wasikilizwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles