FREDRICK KATULANDA, MWANZA Na ABRAHAM GWANDU, ARUSHA
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema maandamano na mikutano itakayofanyika kuanzia Septemba mosi, mwaka huu kwa ajili ya kutekeleza operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) haina lengo la kumjaribu mtu yeyote bali inakusudia kupinga ukiukwaji wa misingi ya Katiba na uvunjaji wa sheria za nchi.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana alipofungua mkutano wa maandalizi ya Ukuta kwa viongozi wote wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini wakiwamo wabunge na madiwani na aligawa vifaa mbalimbali vyenye nembo za chama hicho vitakavyotumika katika maandamano na mikutano ya hadhara.
Alisema siku zote chama hicho kinatii maagizo yote yenye kuzingatia sheria na Katiba inayotolewa na viongozi wa Serikali, lakini si matamko kutoka kwa mtu mmoja yanayokinzana na Katiba.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema viongozi wote wa ngazi zote wana wajibu wa kuitetea na kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano waliyoapa kuilinda na aliwataka kuunga mkono harakati hizo.
“Hatumjaribu mtu yeyote, tunataka kufanya jambo moja tu, nalo ni kukemea wote wanaovunja misingi ya haki kwa kuvunja Katiba. Sisi viongozi wote kuanzia rais, wabunge na madiwani tuliapa kuilinda Katiba hivyo hatuwezi kukubali nchi kuongozwa kwa matamko ya mtu moja.
“Rais yeye chama chake kinafanya mikutano na kinaruhusiwa kufanya siasa lakini vyama vingine hadi mwaka 2020, hatuwezi kukubali maadamu hatuvunji sheria za nchi, tutaandamana kwa lengo la kuzuia utawala usiofuata Katiba,” alisema Mbowe.
Akielezea zaidi namna ambavyo uamuzi wa kufanya maandamano na mikutano ulifikiwa, Mbowe aliwaambia viongozi hao kuacha woga kwa sababu kazi wanayoifanya ni ya kupigania misingi ya haki, kufuata sheria na utawala bora.
“Uamuzi huu wa Ukuta ni wa kamati kuu ambayo ilikaa siku nne mfululizo na haikuwa kazi rahisi. Tulijadiliana sana na tukashangaa kauli ya rais wetu ya kupiga marufuku siasa, sijui alishauriwa na nani siku ile.
“Badala ya kuagiza polisi kuswaga na kupiga raia siku hiyo tunamtaka afute kauli yake. Tulidhani vijana wa chama chake wangefanya maandamano kuunga mkono kauli yake lakini cha kushangaza polisi ndio wanajitokeza kupambana na sisi,” alisema Mbowe.
Pia alisema wamealika vyombo na taasisi mbalimbali za kimataifa kwa lengo la kuja kushuhudia jinsi Serikali ikipambana na raia wake wanaofanya mambo yanayokubalika kikatiba.
“Kwa sababu tunajua polisi watapiga raia siku hiyo, tumealika watu kutoka nje wanaowakilisha taasisi, vyombo vya habari vya kimataifa ili washuhudie Serikali inavyowafanyia raia wake.
“Hatuwezi kukubali utawala wa awamu ya tano utumie nguvu za majeshi wakati ni utawala wa kidemokrasia, tabia ya kutia hofu vyombo vya dola, tabia ya kutia hofu vyombo vya habari, tabia ya kutia hofu wananchi ni tabia za madikteta na inaanza kidogo kidogo wote tuikatae nchini mwetu.
“Ukuta ndiyo kipimo cha kuwatambua wanaharakati na wapiganaji wa kweli au itakuwa siku ya kuwajua wale waliorukia gari njiani. Najua siku hiyo tutaumizwa, muwe na tahadhari lakini msiogope kulipigania Taifa ili lifuate misingi ya Katiba,” alisema Mbowe.
Alisema hata kama jeshi litasingizia kuwa hawatakuwa na askari wa kutosha wa kulinda maandamano yao, lakini halitawazuia kwa sababu watajilinda.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, amesema ataongoza maandamano ya Umoja wa Kupinga Udikteta (Ukuta) yanayotarajia kufanyika Septemba mosi, mwaka huu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.