27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Chadema: Tutaingia mtaani mchana kweupe.

AGATHA CHARLES

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kinaandaa ratiba ya kuanza mikutano ya hadhara mchana peupe huku wakijikita katika sera pasipo kupambana na mtu.

Wakati wakisema hayo, Jeshi la Polisi nchini limepokea taarifa hiyo kwa tahadhari wakisema hakuna mtu anayekatazwa kufanya mkutano kwenye eneo lake, kinachotakiwa ni kutoa taarifa mapema.

Kauli ya Chadema ilitolewa na Katibu Mkuu wake, Dk. Vicent Mashinji, alipokuwa akijibu moja ya maswali ya waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho, ambao ulitoa maazimio matatu ya Kamati Kuu iliyoketi Februari 9 hadi 10.

Dk. Mashinji, akijibu swali lililolenga kujua iwapo Chadema imeacha kufanya mikutano ya hadhara wakati CCM ikiendelea kufanya katika maeneo tofauti, alisema si kwamba Chadema imerudi nyuma kufanya mikutano ya hadhara, bali walikuwa wametingwa na majukumu mengine lakini wanaandaa utaratibu.

“Tumeona CCM huko Karatu wamefanya mikutano ya hadhara na kukashifu. Sisi tulishaamua tutafanya mikutano ya hadhara na mchana peupe kwani kufanya mikutano si jinai.

“Tunaandaa ratiba, niwatake wapenda demokrasia duniani kupinga kuingiliwa. Tuna sera zetu, hatutakuwa na muda mchafu wa kupambana na watu,” alisema Dk. Mashinji.

Polisi

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP Ahmed Msangi, ambaye alisema hakuna zuio la mtu kufanya mikutano katika eneo lake ili mradi tu afuate utaratibu.

“Ukifuata taratibu sijawahi ona mikutano imezuiwa. Kwa hiyo ilimradi wafuate utaratibu, watoe taarifa mapema. Mtu hazuiwi kufanya mkutano kwenye eneo lake ili mradi kuna usalama,” alisema Msangi.

Kamati Kuu

Akizungumza kuhusu ajenda na maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi kwa siku mbili mwishoni mwa wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema walijadili hali ya siasa na mambo mengine na kufikia maazimio matatu.

Alisema maazimio hayo ni pamoja na kufungua kesi mahakamani kupinga Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa iliyopitishwa na mkutano wa bunge uliopita.

Alisema suala la muswada huo lilijadiliwa kwa kina na wanasheria, vyama vya siasa na asasi nyingi za kidemokrasia, lakini muswada huo umekuja kunyonga demokrasia kinyume na maelekezo ya Katiba ya nchi.

Profesa Safari alisema Chadema na wadau wengine wa demokrasia, walifanya jitihada za kuzuia kupitishwa muswada huo ikiwamo kufungua shauri Mahakama Kuu wakimtumia Wakili Fatma Karume (Rais wa Chama cha Mawakili (TLS), kuzuia muswada huo chini ya ibara ya 30 ya Katiba Jamhuri ya Muungano.

Alisema shauri hilo lilikataliwa kufunguliwa kukiwa na pingamizi kuwa linapingana na kifungu cha 18 kifungu kidogo cha sita cha sheria hivyo ilishindikana.

“Tutarudi tena kufungua kesi mahakamani kupinga sheria yenyewe ikishatangazwa na gazeti la Serikali. “Tutafungua si chini ya ibara ya 30 bali tayari sasa Katiba imeshakiukwa. Nafikiri shauri hili litasikilizwa na naamini kama majaji watakuwa weledi vipengele vingi ambavyo shahiri dhahiri vinapingana na Katiba vitawekwa sawa sawa,” alisema Profesa Safari.

Alisema suala la pili kujadiliwa katika mkutano huo ni ufisadi.

“Ajenda ya ufisadi ilikuwa ya kwetu lakini CCM iliichukua na wanajigamba kuwa wamefanikiwa. Lakini Kamati Kuu imeona sivyo. Kamati Kuu imeona kuna viashiria vya ongezeko la ufisadi nchini. Mfano ushahidi wa kwanza ni upotevu wa Sh trilioni 1.5 ulioibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kutoka hesabu za 2016/17,” alisema Profesa Safari.

Profesa Safari alisema katika kikao kilichopita Mbunge wa chama hicho, Catherine Ruge, alitoa hoja ya upotevu halisi wa kipindi hicho cha 2016/17 kuwa si Sh trilioni 1.5 bali ni Sh trilioni 2.4.

Suala la tatu ambalo nalo lilijadiliwa na Kamati Kuu ni umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi itakayosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Profesa Safari alisema suala hilo limejadiliwa kwa kina na kuona kuwa kuna haja ya kuboresha Tume ya Uchaguzi ili iwe inahakikisha uchaguzi huru na wa haki.

“Maana yake ni kubadilisha vifungu vya Katiba vinavyohusiana na Tume, kubadilisha sheria za uchaguzi mfano sheria ya uchaguzi ya mwaka 2002.

“Ile sheria ya uchaguzi inayosimamia uchaguzi wa Rais, wabunge na kanuni za uchaguzi wa Rais na wabunge, zilingane na uchaguzi huru na wa haki,” alisema Profesa Safari.

Alisema jambo lingine ni kurekebisha sheria za chaguzi za Serikali za Mitaa na kanuni zake.

 “Chadema imeazimia kuandaa rasimu ya kuboresha Tume ya Uchaguzi pamoja na sheria zake zote. Itakapokuwa tayari, itajadiliwa na Kamati Kuu kwa kina na kuiwasilisha mbele ya wadau wote wa demokrasia ikiwamo CCM haraka ili tuwe na mjadala wa kitaifa.

“Tukubaliane kuwa sheria hizo zinarekebishwa kuhakikisha mshindi wa kweli anatangazwa iwe Rais, mbunge au diwani,” alisema Profesa Safari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles