33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema mtegoni

  • Mbowe njiapanda bungeni, mahakama yaamuru wabunge wanne wakamatwe

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

HATUA ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kusema  Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe mtoro, inamweka njiapanda kiongozi huyo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa ujumla.

Akiwa bungeni jijini Dodoma juzi Spika Ndugai alisema  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakosa nafasi za mara kwa mara za kuuliza maswali kwa Waziri Mkuu kwa sababu ya utoro wa kiongozi wake.

Ndugai alisema hata kama kiongozi wa kambi hiyo asipokuwapo bungeni siku nyingine, anapaswa kuwapo Alhamisi kwa sababu ni siku ya maswali kwa Waziri Mkuu na kwamba hata mbunge awe wapi ikiwa Spika hana taarifa zake anahesabiwa kuwa ni mtoro tu.

Kauli hiyo ya Ndugai inaonekana kumweka Mbowe na chama chake njiapanda  kutokana na kuchukua hatua kwa sababu kama hizo kwa  wabunge wawili wa chama Chadema,  Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki).

Lissu na Nassari walivuliwa ubunge wao mapema mwaka huu kwa sababu ya utoro, uamuzi ambao ulifikiwa baada ya kiongozi huyo wa Bunge kusikika mara kadhaa akitahadharisha kuhusu ofisi yake kutokuwa na taarifa zao.

Kabla ya wabunge hao kuvuliwa nyadhifa zao tayari kilikuwa kimepoteza wabunge wengine sasa saba tangu ufanyike Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Wabunge hao ni wale waliokihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa maelezo kuwa wanakwenda kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli katika kuliletea Taifa maendeleo.

Ikiwa Mwenyekiti huyo wa Chadema atavuliwa ubunge kwa kosa la utoro  chama hicho kitakuwa kimepoteza jumla ya wabunge 10 katika kipindi cha miaka minne tu baada ya Uchaguzi Mkuu.

Kauli ya sasa ya Spika kuhusu Mbowe imewashtua baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifuatilia mwenendo wa maamuzi ya Ndugai  kwa sababu mazingira ya mkasa huo yanaendana na yale yaliyosababisha kuvuliwa ubunge Lissu na Nassari.

Juni 28, mwaka huu Spika Ndugai alitangaza kumvua ubunge Lissu huku akitoa sababu mbili zilizosababisha kufikiwa uamuzi huo kuwa ni kutoonekana bungeni bila Spika kuwa na taarifa ya rasmi na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni.

Itakumbukwa kuwa Lissu amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7 mwaka 2017, baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu ambao hadi sasa vyombo vya dola havijawabaini akiwa jijini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge na kulazimika kusafirishwa kwenda Nairobi kwa matibabu zaidi kabla ya kuhamishiwa nchini Ubeligiji na kufanyiwa upasuaji zaidi ya mara 20 hadi sasa.

Kabla ya uamuzi huo, Spika Ndugai alitahadharisha kuwa atasitisha mshahara na malipo yote na mbunge huyo mpaka atakapopata taarifa zake rasmi kuhusu mahali alipo na anafanya kitu gani, kwa sababu hata ofisi ya Bunge haina taarifa zozote.

Ndugai alikaririwa wakati huo akisema anachokifanya Lissu kinatakiwa kuangalia kipekee kwani hayupo jimboni kwake, Bungeni wanapofanyia kazi, hospitalini, nchini mwake na Spika hana taarifa zake na wala yeye mwenyewe kumwandikia kwamba yupo mahala fulani.

Kauli hiyo ya Ndugai ilikuja siku chache baada ya mwanasiasa huyo kuhojiwa na vyombo mbalimbali vya habari vya nje ya nchi likiwamo Shirika la Habari la Uingereza kupitia kipindi chake cha Hard Talk.

Kabla ya kuvuliwa ubunge,  Januari mwaka huu Lissu kupitia mitandao ya kijamii alieleza kuwa amepata taarifa za kuwapo mpango wa kumvua ubunge.

Tukio la Lissu kuvuliwa ubunge lilitanguliwa na lile la Machi 29, mwaka huu ambapo aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, alivuliwa wadhifa huo baada ya kushindwa kuhudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge.

Mikutano hiyo ni pamoja na ule wa 12 ulioanza Septemba 4 hadi 14 na ule wa Novemba 6 hadi 16, 2018 pamoja na mkutano wa Januari 29 hadi 9.

Kutokana na mbunge huyo kupoteza sifa ya kuendelea kuwa mbunge, Spika Ndugai aliiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akiieleza kuwa jimbo hilo lipo wazi hivyo iendelee na mchakato wa kuitisha uchaguzi.

Taarifa ya kuvuliwa ubunge wa Nassari ilieleza kuwa uamuzi huo umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 71(1) (c) inayoeleza kuwa mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa  kuwa ibara hiyo pia imefafanuliwa katika kanuni ya 146 (1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, kuwa ‘kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge na kwamba mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Katika sakata hilo Nassari alikiri kutohudhuria vikao hivyo huku alieleza kuwa alitoa taarifa katika Ofisi ya Spika wa Bunge ambapo Januari 29, mwaka huu alimwandikia Spika barua kumtaarifu kwamba asingeweza kuhudhuria mkutano wa 14 wa Bunge kutokana na kuwa nje ya nchi akimuuguza mke wake aliyekuwa na matatizo ya uzazi.

Taarifa zilizoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari wakati huo mbunge huyo aliwasilisha taarifa yake ya kutohudhuria mkutano huo kwa barua pepe baada ya kuwasiliana na msaidizi wa Spika Ndugai na kumshauri kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine Novemba 15 mwaka jana alitoa orodha ya mawaziri na wabunge watoro ambapo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Dk Agustine Mahiga, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba.

Mwingine ni aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, wakitajwa kuwa vinara wa kutohudhuria vikao vya Bunge.

Katika orodha hiyo Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, aliorodheshwa kuwa mbunge mtoro zaidi kuliko wote bungeni na kwenye kamati za Bunge huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mku Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akiongoza kwa kuwa na mahudhurio bora kuliko wabunge wote.

Lema alitajwa kwenye orodha ya watoro, wakati ambapo upande wa utetezi ulidai kuwa mbunge huyo alikuwa gerezani wakati fulani kwa takribani miezi minne na zaidi akiandamwa na kesi kadhaa mkoani Arusha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles