Na Clara Matimo, Mwanza
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Viktoria kimesema ili kuwaamsha wananchi, kukijenga chama kuanzia ngazi ya chini, kusajili wanachama wapya na kuwaamsha wananchi kutetea maslahi ya taifa lao, kitaendesha oparesheni maalum iliyopewa jina la ‘Grassroot Fortification (GF)’ kuanzia Julai 10, mwaka huu katika mikoa ya Mwanza, Geita na Mara.
Hayo yameelezwa Julai Mosi, 2023 na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Grayson Wanzagi katika mkutano na waandishi wa habari ambao umeandaliwa na Baraza la uongozi wa chama hicho mkoa ukihudhuriwa na baadhi ya waliogombea nafasi za ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kwenye ofisi za kanda hiyo zilizopo Nyegezi, Mwanza.
Wanzagi amesema lengo ni kuuhisha chama ngazi ya chini kwenye msingi katika kutimiza dhana ya ‘Chadema ni Msingi’ kwa kukipeleka chama chini kwa wananchi ngazi ya familia, vitongoji, kaya ili na faida yake ni wananchi wapate nguvu ya kupaza sauti yao na kulitetea taifa lao, kulileta taifa pamoja na kupambania katiba mpya.
“Tunataka tutume ujumbe kwa wabunge wote wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) kwa kwenda majumbani kwao na ofisini kwao kuwaambia hiki walichofanya siyo sahihi kwa sababu Watanzania hatuko tayari kufanywa watumwa wa mataifa mengine na kuingizwa kwenye mikataba ya kinyonyaji.
“Tunataka kuwatoa watanzania utumwani ili tuwapeleke kwenye nchi ya ahadi, tunataka kuwafanya Watanzania wamiliki keki yao ya taifa na siyo waishie kushuhudia watu wengine wakila keki ya taifa lao,” amesema Wanzagi na kuongeza:
“Kama tungekuwa na katiba bora na yenye ridhaa ya wananchi leo tungekuwa tunapiga kura ya kutokuwa na imani na wabunge wote waliopitisha mambo ya hovyo bungeni, waliopitisha tozo zinazowaumiza wananchi ama ubinafisishaji wa bandari zetu huku ni kuuza utu na mamlaka ya Watanzania,” amesema.
Mwanachama wa chama hicho, Sijaona Karoli ambaye aligombea ubunge wa Ukerewe mwaka 2020, amesema: “Pamoja na kulalamika, kupinga nini ambacho kitaokoa nchi hii, ndiyo maana tumekuja na GF (Grassroot Fortification) ili kupata katiba mpya ambayo ndiyo itakuwa suluhisho la mambo yote haya,” Sijaona.
Kuhusu bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni, Karoli amesema: “Tunachokiona tunakwenda kuongeza ugumu kwa wananchi na mzunguko mdogo wa fedha tunalitaka bunge kupitia upya kwenye baadhi ya mambo yanayowagusa wananchi kwa sababu tulitegemea bajeti hii ilete suluhisho kwa maskini na wananchi wa kawaida, badala yake inekwenda kuongeza ugumu wa maisha, tunaomba bunge kuridhia lipitie upya,” amesema Karoli.
Naye, Viktoria Benedict ambaye aligombea ubunge Jimbo la Sengerema, amesema oparesheni hiyo ni mwendelezo wa programu ya +255 #KatibaMpya inayowataka Watanzania wote kushiriki mchakato wa katiba mpya, huku akiwaomba Watanzania kuhudhuria mikutano ya hadhara ya chama hicho ili kupata elimu na kuhamasika kudai katiba.
“Chama chetu kimekuja na mfumo wa GF kwenda mpaka ngazi ya chini Kwa wananchi, ni mpango mahususi wa kuliunganisha taifa tunawafuata wananchi chini kuona namna ya kulikomboa taifa. Tunataka kuwasajili wanachama kuanzia msingi kwenye familia mpaka juu, tunawaomba wananchi wote twende tukalikomboe taifa letu kwa kujisajili kwa wingi na kuhamasishana tudai katiba mpya,” amesema Benedict.
Amesema Katiba mpya ni hitaji kuu la wananchi kutokana na mabadiliko na kukua kwa kasi kwa teknolojia, uchumi, utandawazi, mabadiliko ya tabianchi, uoto wa asili na ardhi vinavyolazimisha kuingia kwenye uhitaji wa katiba mpya.