* Wasisitiza hawatatishika, hawataogopa kutekeleza operesheni Ukuta, wampelekea Mutungi tamko lao akalisome vizuri
Na Asifiwe George, Dar es Salaam
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakiogopi mtu yeyote likiwemo Jeshi la Polisi na kusisitiza kuwa operesheni yao ya Ukuta waliyoiandaa kuifanya nchi nzima iko pale pale.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, alisema hawatatishika, hawataogopa na pia hawatatetereka kufanya operesheni hiyo kwasababu lengo lao ni kukataa udikteta na ukandamizwaji wa kisiasa.
Alisisitiza na kurejea kile kile walichokisema tangu mwanzo kwamba Septemba mosi mwaka huu ni siku maalumu ya kukataa udikteta na ukandamizwaji wa kisiasa nchini.
Mwalimu alisema wako imara, sawasawa na wanajiamini kweli kweli kwasababu wanachokidai ni haki yao na ni wajibu wao kisheria na kisiasa.
“Azma na shabaha yetu ya kujenga ukuta iko pale pale na vikao vya vyama tayari vimeshaanza kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini vyenye lengo la maandalizi ya operesheni Ukuta.
“Anayefikiri kwamba Ukuta huu ni wa Maalim Seif, Mbowe au Chadema, amepotoka, ukuta huu ni wa wananchi wote ambao wanataka kuondoa harufu kali ya udikteka, pia wapo wenzetu wa CCM kama wanataka tunawakaribisha waje tuungane nao kudai haki ya kidemokrasia,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Lusige Baregu, alisema tuhuma za uchochezi ukiziendekeza kwa mtu ni ngumu sana na zinahitaji ushahidi.
Profesa Baregu alimtaka Jaji Mtungi kurejea tamko la Chadema na kulitafakari ndipo aangalie kauli za kutoa katika vyombo vya habari.
“Hatuna lengo la kufanya uchochezi, waliopo CCM ambao wanaguswa na tamko letu kama wale waliotishiwa kwamba wangetolewa wanaruhusiwa kuungana nasi na tunawakaribisha na msimamo wetu uko pale pale wa kufanya operesheni Ukuta nchi nzima,” alisema Profesa Baregu.
Naye Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema, alisema hawana muda wa kumjibu Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi, bali ni vyema akafuata sheria na Katiba ya vyama jinsi inavyoeleza.
“Sina imani kwamba Msajili ana tamko letu na kama amelipata atakuwa amelisoma katika vyombo vya habari hivyo leo hii (jana) nitamtuma mtu apeleke tamko hilo ili aainishe maneno ya matusi na uchochezi yaliyopo katika tamko hilo,” alisema.
Siku moja baada ya Chadema kutangaza mikakati mitatu ya kupinga ilichokiita ukandamizaji wa haki na demokrasia, Jaji Mutungi ambaye ni mlezi wa vyama vya siasa pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliibuka wakikituhumu chama hicho kikuu cha upinzani kutoa kauli walizoziita kuwa ni za kichochezi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Jaji Mutungi alisema tamko la Chadema limejaa uchochezi, kashfa na kuhamasisha uvunjifu wa amani na kwamba kifungu cha 9(2)(f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu viongozi au wanachama wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Wakati Jaji Mutungi akisema hayo, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, alisema kauli zilizotolewa na Mbowe zimejaa upotoshaji na uongo uliokithiri na kusisitiza kuwa Serikali haijazuia mikutano ya hadhara kwenye majimbo.