CHADEMA ARUSHA YAPITISHA MGOMBEA NAFASI YA NAIBU MEYA

0
695

Na JANETH MUSHI,

-ARUSHA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Arusha kimempitisha aliyekuwa Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Viola Likindikoki, kugombea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili.

Katika uchaguzi huo uliofanyika mjini hapa juzi, wagombea wengine walikuwa ni Ally Bananga ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini na Prosper Msofe ambaye ni Diwani wa Kata ya Daraja Mbili.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha, Derick Magoma, alisema kuwa Viola ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu alishinda kwa kupata kura 16, Msofe alipata kura tisa na Bananga alipata kura saba.

Alisema baada ya kumaliza taratibu za uteuzi ndani ya chama, watapeleka jina lake katika mamlaka husika kwa ajili ya taratibu nyingine za uchaguzi.

“Baada ya uchaguzi kufanyika na kamati tendaji kukaa imeridhia kumpitisha Viola kuwa mgombea wa nafasi ya Naibu Meya katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018, baada ya kutumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu,” alisema.

Kwa upande wake, Viola, aliwashukuru madiwani hao kwa kumchagua katika kuwania nafasi hiyo katika kipindi cha pili  na kuwaomba ushirikiano ili heshima ya madiwani irudi kutokana na umoja wao.

“Yamkini kule nyuma kuna malengo sikuweza kufikia kwa asilimia 100 kwa sababu mbalimbali lakini niahidi mbele yenu tusisubiri wakati wa uchaguzi ndiyo tunaelezana udhaifu, kama Viola kuna sehemu siendi vizuri ni vizuri uniambie, tujengane kutoka mwanzo ili tuweze kuwasaidia wananchi na kuharakisha maendeleo,” alisema.

Naye Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, alisema kwa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri na naibu meya atakayechaguliwa atahakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati.

“Tutashirikiana kuhakikisha shughuli za maendeleo ya wananchi zinaendelea kwa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri ya jiji ila wale wanaofikiri uchaguzi ndani ya Chadema ni mvurugano au mgawanyiko, wameshindwa chama chetu kiko imara,” alisema na kuongeza:

“Nipongeze chama changu kwa kuonyesha demokrasia ya hali ya juu ambayo vyama vingine havipo, kwa sasa mmeona ndani ya vyama vingine, CCM inakoelekea, Chadema ndiyo kitakuwa chama cha demokrasia halisi katika nchi yetu, umoja wetu ni muhimu katika chama.”

Awali, Chadema ilikuwa na madiwani 24 katika Halmashuari ya Jiji la Arusha ila kwa sasa wamebaki 23 wa kata, tisa wa viti maalumu baada ya Diwani wa Kata ya Muriet, Credo Kifukwe, kujiuzulu nafasi yake hivi karibuni huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa na diwani mmoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here