23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

CECAFA yaiondoa Yanga Kagame

Marcio Maximo
Kocha mpya wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Marcio Maximo

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limeiondoa timu ya Yanga kwenye michuano ya Kombe la Kagame, kutokana na kupeleka kikosi cha timu ya vijana, jambo ambalo ni kinyume na kanuni, hivyo imeiteua Azam FC kuchukua nafasi yake.

Katika michuano hiyo iliyoepangwa kuanza Jumamosi hadi Agosti 23, jijini Kigali, Rwanda na Yanga ilipangwa kufungua pazia kwa kucheza dhidi ya wenyeji Rayon Sports, iliyokuwa nayo Kundi A sambamba na timu nyingine za KMKM ya Zanzibar, Coffee ya Ethiopia na Atlabara ya Sudan Kusini.

Yanga, inayonolewa na Mbrazil, Marcio Maximo, ilipanga kutumia kikosi cha vijana kushiriki michuano hiyo kikiwa chini ya kocha msaidizi, Mbrazil Leonardo Neiva na Kocha Msaidizi wa timu B, Shadrack Nsajigwa, jambo ambalo limekataliwa na waandaaji CECAFA na kuitoa.

CECAFA imesema baada ya majadiliano na Yanga kupitia Shirikisho la Soka nchini (TFF), klabu hiyo ilipewa muda hadi juzi iwe imetekeleza matakwa ya kikanuni, ili iruhusiwe kushiriki michuano hiyo, lakini haikufanya hivyo.

Wakati CECAFA ikiitoa Yanga, imefanya uamuzi mwingine wa kuiteua Azam FC, iliyoshika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2012/2013 kuchukua nafasi hiyo, ambayo tayari imethibitisha ushiriki wake.

Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa timu hiyo, Jemedari Said, alisema wamepata barua rasmi ya CECAFA ya kuombwa kushiriki michuano hiyo na kuridhia uamuzi huo, huku akidai watapeleka muziki wote wa kikosi cha kwanza na wataondoka leo kuelekea Kigali.

“Tumetumiwa barua ya kushiriki Kagame baada ya Yanga kuondolewa na sisi tumekubali, hivyo tutapeleka kikosi chetu cha kwanza, hata wale walioko timu ya taifa ‘Taifa Stars’ nao watajumuika,” alisema Said.

Timu hiyo ina baraka zote za TFF na itaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, James Mhagama, kuelekea Kigali.

Ushiriki wa Azam kwenye mashindano hayo utaiongezea kasi kwenye maandalizi yao ya msimu ujao na kutimiza malengo ya kocha wao, Mcameroon Joseph Omog, kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wachezaji wapya waliosajiliwa na Azam; Mhaiti, Leonel Saint- Preux, Ismail Diara raia wa Mali, Frank Domayo (majeruhi) na Mrundi Didier Kavumbagu, wataungana na wachezaji wengine wa zamani wa timu hiyo kupata nafasi ya kushiriki Kagame, lakini kuna taarifa kuwa washambuliaji Diara na Gaudence Mwaikimba wameachwa kwenye safari hiyo.

Kauli uongozi wa Yanga

Akizungumzia kuondolewa kwenye michuano hiyo, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema hadi jana jioni walikuwa bado hawajapokea barua rasmi.

“Sisi hatujapata barua rasmi ya kuondolewa na tunasikia taarifa tu kwenye vyombo vya habari, tutaendelea na maandalizi ya michuano hiyo kama kawaida mpaka tutakapopewa barua rasmi ya kutolewa,” alisema Kizuguto kwa njia ya barua pepe.

Kauli ya Kizuguto imeonekana kuendana na kocha Neiva, anayekinoa kikosi cha Yanga kwa ajili ya Kagame aliyesema kuwa ataendelea na programu yake ya michuano hiyo, licha ya CECAFA kukaa kimya juu ya uthibitisho wa timu yake.

Neiva agawa majukumu

Licha ya kuondolewa kwenye michuano hiyo, Neiva amegawa majukumu ya kikosi hicho, ambapo amemchagua kiungo, Nizar Khalfan, kuwa nahodha wa kikosi cha Kagame, huku akiwachagua Said Bahanuzi, Omega Seme na Khalfan kuwa wapigaji penalti na faulo kwenye mechi.

“Hao ndio nawapa mafunzo ya kufanya mambo hayo. Omega, Bahanuzi na Nizar watapiga penati na faulo, huku Nizar akiwa nahodha wa kikosi, nitaendelea kuwapa mafunzo hapa na hata tukifanikiwa kwenda Rwanda kwenye michuano,” alisema Neiva.

Kikosi cha Yanga kilichokuwa kimepangwa kushiriki michuano hiyo kinaundwa na wakongwe Ally Mustapha ‘Barthez’, Nizar Khalfan, Rajabu Zahir, Said Bahanuzi, Hussein Javu, Omega Seme na Oscar Joshua, pamoja na wachezaji vijana; Issa Ngao, Said Ally, Pato Ngonyani, Amos Abel, Ben Michael, Shaban Idd, Hamis Issa, Juma Kayanda, Frank Sheneiba, Juniro Rick, Frank Gerald, Sospeter Maiga na Said Ndutu.

Shabiki Simba apewa dozi Loyola

Katika mazoezi ya jana yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Loyola, jijini Dar es Salaam, shabiki mmoja anayedaiwa kuwa ni wa timu ya Simba, ambaye jina lake halikuweza kufahamika, alipewa kichapo na mashabiki wa Yanga.

Shabiki huyo, aliyetolewa nje ya mazoezi hayo kwa nguvu baada ya kushambuliwa na mashabiki hao, alifanya kosa la kuvaa jezi ya Simba. Baadhi ya mashabiki walisikika wakisema: “Apigwe huyo, mtoe! mtoe! usituchezee kabisa sisi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles