30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yawaangukia tena Ukawa

Nape Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye

NA FREDY AZZAH, DODOMA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimempa kibarua kingine Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, kuendelea na mazungumzo ya kusaka mwafaka na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili kunusuru mchakato wa Katiba mpya.

Pamoja na hatua hiyo, CCM imesema imesikitishwa na hatua ya kuvunjika kwa mazungumzo yaliyohusisha viongozi wake na wale wa CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu (CC) ya CCM kilichofanyika mjini Dodoma juzi, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema pamoja na kutopatikana kwa mwafaka, wameazimia Bunge Maalumu la Katiba liendelee na vikao.

Alisema hatua ya Kinana kuendelea kukutana na vyama pamoja na wadau wengine, itasaidia kuendelea kupata maridhiano kuhusu kuendelea mchakato wa Katiba mpya kwa mujibu wa sheria.

“Kamati Kuu inaendelea kuwasihi Watanzania wote kuendelea kushikamana na kuvumiliana pale wanapopishana kimtazamo juu ya hoja mbalimbali za Katiba kwa amani, utulivu na Utanzania wetu ni muhimu kuliko tofauti zetu za kimtazamo,” alisema Nape.

Alisema CCM inaridhishwa na juhudi za Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), pamoja na vyama vinavyounda Ukawa kutafuta mwafaka wa kisiasa kwa lengo la kuimarisha amani, utulivu, mshikamano na kuaminiana kati ya wadau mbalimbali.

“Kamati Kuu inaunga mkono juhudi za TCD za kuendeleza mashauriano kati ya vyama na ndani ya vyama kwa lengo la kupunguza mivutano, kujenga uaminifu, ustahimilivu na umoja kati yao,” alisema.

Mawaziri wafyekwa ziara ya JK

Akizungumzia utoro wa mawaziri katika Bunge Maalumu la Katiba, Nape alisema mkakati wa CCM hivi sasa ni kupunguza idadi kubwa ya mawaziri kwenye ziara za Rais Kikwete.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza utoro na hata kuwafanya wengi wao kuhudhuria vikao vya kamati za Bunge la Katiba.

“Mbali na mawaziri, pia CCM itawabana wabunge wasiokuwa na sababu za msingi kutohudhuria vikao hivyo, ili waweze kushiriki,” alisema Nape.

Alisema ziara ya Rais Kikwete iliyoanza mjini Morogoro jana, itakuwa na mawaziri wachache, lengo likiwa kuwafanya wengine wahudhurie vikao vya kamati za Bunge la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma.

“Hatuwezi kufanya shughuli za Serikali zisimame, lakini tutaangalia namna ya kupunguza zile zisizo za lazima ili mawaziri waweze kuhudhuria hivi vikao, hata leo rais anaanza ziara Morogoro, lakini idadi ya mawaziri kwenye ziara yake imepunguzwa ili wengine wafanye kazi ya Bunge la Katiba.

“Kuna taarifa za wabunge wetu kutohudhuria, lakini kwa kiasi fulani wana sababu, ila tutaangalia kama sababu zenyewe ni za msingi,” alisema Nape.

Alisema kuwa kuna kamati za kusimamia na kuangalia mahudhurio ya wajumbe hao na kuwa zitashughulikia suala hilo.

“Ni vigumu kuhudhuria kwa asilimia 100, lakini tutaangalia namna nzuri ya kufanya ili wasio na sababu za msingi wahudhurie hivyo vikao,” alisema.

Nape alisema Kamati Kuu ya CCM imewataka wajumbe wote kuhakikisha wanahudhuria vikao vyote vya kamati na kuijadili rasimu kwa mapana huku wakitanguliza mbele masilahi ya taifa kama njia ya kupata Katiba inayotarajiwa na Watanzania walio wengi.

Wiki iliyopita, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad, alisema kwa kiasi kikubwa wajumbe wa Bunge hilo kutoka Tanzania Bara wakiongozwa na mawaziri wamekuwa watoro kwenye vikao vya kamati.

Alisema hali hiyo hufanya kuchelewa kuanza vikao kwa baadhi ya kamati kutokana na akidi kutotimia.

Kauli ya Ukawa

Akizungumza na MTANZANIA jana kuhusu msimamo wa kurudi kwenye mazungumzo na CCM, mwenyekiti mwenza wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema umoja huo una nia ya dhati ya kutetea masilahi ya taifa.

Alisema kama kweli CCM imekubaliana  kusaka mwafaka, wao wako tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo ili waweze kujadili mustakabali wa nchi na si masuala ya kisiasa.

“Tupo tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu Ukawa inafanya kazi ya kutetea masilahi ya wananchi, na kwamba hatufanyi kazi kwa masilahi ya vyama vyetu,” alisema Mbatia.

Aliongeza Katiba si jambo la lelemama, bali ni suala la utashi ambalo kila mmoja anapaswa kulitambua, hivyo basi CCM wanapaswa kuwa makini kwa kutanguliza masilahi ya wananchi kwanza na kuweka kando ya chama chao.

Mbatia alisema Ukawa hawajawahi kukataa mazungumzo na CCM yanayolenga masilahi ya wananchi, hali ambayo inaweza kusaidia kupatikana kwa mwafaka wa suala hilo.

“Kama CCM wamekaa chini na kujadili suala hilo ni sawa, kwa sababu linaweza kuleta mwafaka wa upatikanaji wa Katiba mpya, hivyo basi wanapaswa kuondoa itikadi ya chama kwenye kikao hicho,” alisema.

Katibu wa Ukawa ndani ya Bunge, Julius Mtatiro, alisema kuwa ili waweze kufikia mwafaka wa suala hilo, CCM inapaswa kusitisha vikao vya Bunge Maalumu la Katiba waweze kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

Alisema bila ya kufanya hivyo, hakutakuwa na majadiliano yatakayozaa matunda kwa sababu wanaingia kwenye mvutano ambao utarudisha nyuma mchakato wa Katiba.

“Ili tuweze kufikia mwafaka, CCM wanapaswa kusitisha vikao vya Bunge Maalumu la Katiba na kurudi kwenye meza ya mazungumzo, hapo ninaamini tunaweza kuingia kwenye maridhiano,” alisema Mtatiro.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. CCM msidanganye wananchi, kama mngekuwa na nia ya kutafuta maridhiana no vyama vya upinzani katika katiba mpya, mngesimamisha mchakato. Sasa kama Ukawa wakikubali kurudi bungeni, mtaanzia wapi kujadiliana rasimu hiyo ambayo mmeshaichanachana? Huu ni usanii, watanzania mnaendelea kufanyiwa usanii na CCM kwamba ,” ati katika kipindi hiki tuvumiliane katika mitazamo yetu ili kuendelea kudumisha” amani, utulivu na mshikamano”. Je ni mamani gani CCM wanayoongelea waidumishe, machakato huu haujaleta amani, bali chuki, matusi, madharau, ubabe, na vitisho. Je hivi ndivyo viashiria vya manai? Kama nchi itatumbukia katika Vita basi CCM hamtakwepa lawama hizo milele.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles